Kili Stars, Zanzibar Heroes tunalisubiri Kombe la Chalenji

Muktasari:

  • Mashindano hayo makubwa kwa ukanda huo unaosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), yamerejea baada ya kukwama kwa miaka miwili.

MICHUANO ya Kombe la Chalenji inayozikutanisha timu za soka za taifa za nchi za Afrika Mashariki na Kati, itaanza kesho Jumapili katika taifa jirani la Kenya.

Mashindano hayo makubwa kwa ukanda huo unaosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), yamerejea baada ya kukwama kwa miaka miwili.

Katika kivumbi hicho, Tanzania itawakilishwa na timu mbili; Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar Heroes.

Tayari vikosi vyetu vyote vipo huko kwa ajili ya michuano hiyo ambapo Kilimanjaro Stars itafungua dimba kesho kwa kuumana na Libya na Zanzibar itashuka uwanjani Jumanne kuvaana na Rwanda.

Ni matumaini ya Watanzania kwamba timu zao hizo zinaweza kuwa na ushiriki mzuri na hata kutwaa ubingwa, huku jicho zaidi likiwa kwa kikosi cha Kilimanjaro Stars ambacho historia inaibeba kwani imeshawahi kufanya hivyo zaidi ya mara moja.

Mara ya mwisho Tanzania Bara kutwaa ubingwa huo ilikuwa mwaka 2010 katika mashindano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kuifunga Ivory Coast bao 1-0 la penati ya Shadrack Nsajigwa. Ivory Coast ilishiriki kwa tiketi ya timu mwalikwa.

Bara pia ilifanya hivyo mwaka 1994 katika mashindano yaliyofanyika Kenya huku Zanzibar ikiwa na rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara moja.

Kwa rekodi hizo ndio maana Watanzania wana matumaini kiasi ijapokuwa uwezekano upo mikononi mwa wachezaji wetu kuweza kuhimili na kuushinda upinzani wa timu nyingine.

Hata hivyo, wakati timu zetu hizo zikiwa huko, tunaamini wachezaji wa Zanzibar wangeweza kujazwa morali zaidi ya ushindani kuanzia nyumbani walipoanza safari yao.

Kwa maendeleo ya sasa ya kidunia, ni matarajio ya wengi kwamba kwa timu ya taifa inayosafiri kutoka nchi moja kwenye nyingine, inapendeza zaidi inapotumia usafiri wa ndege.

Kwa timu kama Zanzibar ambayo haina ushiriki mwingine wa peke yake kwenye mashindano kama ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ama lile la dunia (Fifa), kwenda kwao Chalenji ni fursa pekee inayopaswa kutumiwa kuwajaza morali zaidi wachezaji wake.

Kusafiri kwa basi kama ilivyofanywa kwa Zanzibar Heroes kunaweza kusiwe na athari kiufundi kutoka na uwepo wa muda wa kutosha wa kumpumzika, lakini tunaamini kisaikolojia ambalo pia ni jambo muhimu kwa timu, kusafiri kwa ndege kungeweza kuwaongezea hamasa.

Mwanaspoti hatuamini kama mamlaka za soka za Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi (SMZ), walishindwa kabisa kuiweka timu yao katika daraja moja la hadhi ya timu ya taifa.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba, timu hiyo imechukuliwa kama kitu cha kawaida na kusafiri kupitia Tanga kwenda Mombasa hadi Kakamega itakapokuwa ikishiriki mashindano hayo.

Ni safari ndefu na ya siku mbili njiani. Ni safari ambayo itawapa uchovu mkubwa wachezaji pamoja na viongozi wengine wa msafara huo.

Ni ajabu kusema Zanzibar imekosa fedha za kuisafirisha timu hiyo ya watu 34 kwa ndege kwenda Kenya. Wakati Zanzibar inahaha kusaka nafasi ya mashindano ya Afrika na dunia, tunaamini ingepaswa kutumia wakati huu kuonyesha ni namna gani ilinavyoweza kujipanga kufanya mambo yake kwa kiwango cha kuvutia.

Ikumbukwe timu hiyo itakapomaliza mashindano ya Chalenji, haina kitu kingine inachofanya mpaka mashindano hayo yatakapoandaliwa tena mwakani.

Ni wazi safari ya basi ina madhara makubwa kiufundi kwani wachezaji wanafika wakiwa wachovu, hivyo mwalimu kushindwa kutekeleza programu zake kwa kiwango stahiki.

Unaweza kusema mechi yao ipo mbali, lakini mechi inaanzia mazoezini, hivyo inawezekana kukawa na athari wameipata wachezaji kwenye mazoezi yao huko Kenya ambayo inaweza kuwa ijmechangiwa na uchovu wa safari. Athari hiyo inaweza kuwa na gharama siku ya mchezo.

Lakini pamoja na hayo, Mwanaspoti tunachukua nafasi hii kuwaomba Watanzania kuzitakia kila la heri timu hizo mbili.