Karibu Namungo, KMC, Singida United zipo huku

Muktasari:

  • Timu ilikuwa ina uhakika inafanya mazoezi bila shida yoyote, kucheza mechi za nyumbani katika eneo ambalo wamelizoea, pia wingi na mwitikio wa mashabiki waliojitokeza kuipa nguvu timu hiyo kila ilipokuwa inacheza hapo.

KATIKA vijiji vyote vya Lindi huenda muda huu unaposoma Wino Mweusi wakazi wa maeneo hayo wanasherehekea mafanikio ya timu yao ya Namungo FC.

Timu hiyo kutoka Luangwa Lindi imefanikiwa kupanda daraja na msimu ujao itacheza Ligi Kuu Bara na wakazi wa maeneo hayo kupata fursa ya kuziona timu kubwa za Simba, Yanga, Azam na nyingine nyingi.

Namungo kimsingi walikuwa na kila sababu ya kupanda Ligi Kuu Bara kutokana na kikosi chao, pia mbali na kuwa ni timu ya Ligi Daraja La Kwanza lakini walikuwa wakipata mahitaji sahihi.

Uwanja wa nyumbani unaojulikana kama Majaliwa Stadium, ni moja ya sababu zilizochangia Namungo kupanda daraja. Uwanja wao ni mzuri hasa sehemu ya kuchezea na hii ilionyesha dalili za mapema za wao kupanda.

Timu ilikuwa ina uhakika inafanya mazoezi bila shida yoyote, kucheza mechi za nyumbani katika eneo ambalo wamelizoea, pia wingi na mwitikio wa mashabiki waliojitokeza kuipa nguvu timu hiyo kila ilipokuwa inacheza hapo.

Kimsingi, hilo ni moja ya mafanikio makubwa kwao ambayo waliwapiga bao hata Simba na Yanga na ilitosha kuona ni dalili moja wapo kuwa timu yenye malengo ya kupanda TPL.

Kabla ya msimu kuanza walifanya usajili wa maana wa wachezaji wenye uwezo walioisaidia timu muda wote kuwa katika nafasi za juu kwenye msimamo chini ya Kocha Fulgence Novatus ambaye baadae walimtimua.

Pia walicheza mechi za kirafiki na Simba na Yanga, huku usafiri ukiwa ni wa kujitegemea. Pia wachezaji na benchi la ufundi walipata mahitaji yao hasa ya kiuchumi kwa wakati tofauti na tulivyozoea kusikia malalamiko ya kiuchumi kwa timu nyingi nchini.

Usajili walioufanya dirisha dogo pia uliwasaidia, ingizo la wachezaji kutoka timu za Ligi Kuu kama Azam, Mbaraka Yusuph, Oscar Masai na wengine ambao waliongeza nguvu na kuziba mapungufu yaliyoonekana mzunguko wa kwanza hadi kutimiza malengo yao.

Baada ya kuona mambo hayaendi katikati ya msimu, mabosi wa klabu hiyo waliamua kuachana na Kocha Novatus na kumchukua aliyekuwa kocha wa Biashara United, Hitimana Thiery ambaye aliifanikisha timu hiyo kupanda Ligi Kuu.

Hata hivyo, yote hayo yamefanikiwa kutokana na nguvu ya kipesa kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wadau wengine ambao walikuwa bega kwa bega na timu hiyo.

Namungo wameweza kufika Ligi Kuu lakini huku kuna njia mbili ambazo wanatakiwa kuchagua ya kwanza ni KMC au ile ya Singida United.

Iko hivi, kikosi cha KMC kilipanda ligi msimu uliopita lakini wameonekana kufanya usajili wa wachezaji wa maana na wenye uwezo na kuboresha benchi la ufundi ambalo mpaka hivi leo imeonekan ni timu yenye ushindani na uwezo inapokuwa uwanjani.

KMC wapo katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, wapo kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ambalo watacheza na Azam, lakini wameendelea kuishi kwa utulivu na kutokuwepo na matatizo ya kiuchumi katika kikosi chao.

Mbali ya ligi kukosa mdhamini KMC wameonekana kuishi vizuri na kuendelea kuimarika mechi baada ya mechi pengine ni kutokana na uwezo wanaonesha wachezaji wao wazoefu kama Juma Kaseja, Ally Ally, Yusuph Ndikumana na wengine.

Namungo wamependa njia ya kwanza ya kuwafanya kuendelea kuwa vizuri kama vile ambavyo mlionekana mkiwa ligi daraja la kwanza ni hii ambayo mpaka wakati huu imeonekana kuisaidia KMC kuwa katika nafasi za juu kwenye msimamo na si kuonekana timu ambayo imekuja kutembea Ligi Kuu kama zinavyofanya timu nyingine.

Njia ya pili ni ile ya Singida United, ambayo ilipanda daraja kwa kishindo na kufanya uwekezaji wa kutosha.

Singida ilisajili wachezaji wa maana wa kigeni kama Tafadzwa Kutinyu na wazawa kama Mudathir Yahya ambao wote sasa hivi wapo Azam, pamoja na kuimarisha benchi la ufundi kwa kumchukua kocha kutoka Yanga, Mdachi Hans Van Pluijm.

Singida ilitisha kiuchumi kutokana na udhamini mkubwa na iliweza kuwa na wadhamini wasiopungua kumi ambao wote walitangaza kupitia jezi ya timu hiyo na kupata mafanikio kwa kumaliza nafasi za juu kwenye ligi pamoja na kucheza fainali ya FA ingawa ilipoteza kwa kufungwa na Mtibwa Sugar mabao 3-2.

Hata hivyo, tangu msimu huu uanze imekuwa ni timu yenye matatizo mengi, ikiondokewa na makocha pamoja na wachezaji muhimu. Pigo zaidi ni kuondokewa na wadhamini waliokuwa wakijitoa kuisaidia timu hiyo.

Kwenye msimamo wa ligi hawapo kwenye nafasi nzuri wakiwa nafasi ya ya 11 na alama zao 40, hii ni tofauti na wadau wengi walivyofikiria itafanya maajabu baada ya kuwa timu yenye nguvu kiuchumi.

Hapa ndipo nakumbuka kuwaambia Namungu ilikuwa na kila sababu ya kupanda Ligi Kuu, lakini kuna njia mbili za kupita, ilikopita KMC au ilikopita Singida United. Ni wao tu kuamua.