NINAVYOJUA : Kanuni ya usajili iangaliwe upya kwa faida ya soka letu

Muktasari:

  • Huko nyuma kulikuwepo na kanuni ziliwahi kupitishwa kwa kuamini zitafaa kutumika kwenye ligi yetu, mwishowe zikabadilishwa.

Inawezekana tunafanya mambo kifikra zaidi kuliko inavyotakiwa kiuhalisia. Hapa nazungumzia katika kuhamisha mawazo kuwa vitendo.

Huko nyuma kulikuwepo na kanuni ziliwahi kupitishwa kwa kuamini zitafaa kutumika kwenye ligi yetu, mwishowe zikabadilishwa.

Mfano mzuri ni ile kanuni ya kadi tatu za njano. Badala ya mchezaji kukosa mchezo unaofuata, angeweza kucheza mechi kadhaa, kisha aamue kupumzika kwenye mechi atakayopenda ili tu kuitumikia adhabu yake.

Hili ni wazo lililotengenezwa bila ya kufanyiwa utafiti wa kutosha na kwa msukumo fulani ikapitishwa na kamati ya utendaji ili itumike.

Pia ilikuwepo kanuni moja iliyotaka kutumika ya kulazimisha klabu kuwatumia kwa lazima wachezaji wa kikosi cha pili angalau wasizidi watano kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, pamoja na lengo zuri, lakini kwa dunia ya sasa, hii sio sawa kwani mchezo unahitaji zaidi matokeo na kocha anajua ni wachezaji wapi awatumie na anaweza pia kuwapanga vijana kutokana na mahitaji husika na si lazima.

Ilikuwepo pia kanuni ya usajili wa wachezaji kutoka nje ya nchi. Hii ilitaka wachezaji wapatao 10 kwa klabu moja na itumie wachezaji wasiozidi watano.

Hata hivyo, kanuni zote hizo zimekuwa zikitumika kwa msimu mmoja tu kisha kubadilishwa kana kwamba watu huwa hawafanyi kwanza utafiti wa kutosha kabla ya kuzitekeleza kanuno hizo.

Ingewezekana kwa kanuni hizi mpya kufanyiwa kwanza majaribio kwenye ligi za chini au mashindano yoyote madogo, kama zinaweza kutekelezeka ndipo sasa ziingizwe kwenye michuano mikubwa kama Ligi Kuu.

Zipo nyingine za kuiga tu kutoka kwa mataifa mengine hasa yale yaliyoendlea kisoka, hata hivyo, yafaa kuziangalia kwanza kanuni hizo zinaendana na mazingira halisi ya nchi yetu.

Kuna masuala ya kuangaliwa kama, wachezaji wamekuzwa vipi, wanacheza kwa staili gani na iwapo kanuni itapitishwa itafanikiwa hivyo vyote kwa pamoja ndipo itajulikana kama kanuni itafanya kazi.

Ni wazi kwa sasa huko kwa wenzetu, Ulaya, Amerika ya Kusini na Asia, dirisha dogo la usajili limeshafunguliwa na linatarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu.

Ni sawa na nchi nyingine za Afrika kama Afrika Kusini, Zambia na Misri ambazo ligi zao zinandelea lakini zinaendelea pia na kufanya usajili wa kuimarisha vikosi vyao na zoezi hili huwa rahisi hasa kwenye kuhamisha wachezaji wa nchi nyingine kutokana na nchi zote kuwa katika kipindi cha usajili.

Hata hivyo, hapa nchini dirisha limeshafungwa siku nyingi, ni wazi hakuna namna kama unataka kumsajili mchezaji uliyemwona yupo vizuri na nchini kwao dirisha limefunguliwa.

Kumleta nchini itakuwa vigumu, labda tu uingie naye mkataba wa kumfanya akae tu nchini au umtoe kwa mkopo kwenye nchi ambazo zina nafasi ya kusajili na kuwatumia.

Dirisha la usajili nchini lilifunguliwa Juni 15, hadi Julai 25, mwaka jana ikiwa ni mwezi mmoja tu, uwe umekamilisha kila kitu kinachohusu usajili.

Kumbuka kiuhalisia, nchi yetu mara nyingi wachezaji husajiliwa baada ya kupitia michujo inayofanywa na makocha na si chini ya mwezi mmoja watatakiwa kufanya mazoezi kisha wapate majaribio ya michezo kadhaa, ndipo kocha aridhike na mchezaji husika.

Hata ikitokea mchezaji anasajiliwa kutoka timu nyingine, bado kuna taratibu nyingi zisizo na faida zinafuatwa kila mara, hivyo usajili ndani ya mwezi unakuwa hautoshi. Kumbuka wakati dirisha letu la usajili linafungwa Julai 25, wenzetu soka lilikopiga hatua, ndio kwanza usajili unaendelea hadi ulipofungwa mwishoni mwa mwezi Agosti.

Unajiuliza kulikoni sisi tunamaliza mapema wakati ujenzi wa kikosi bora unaanzia kwenye usajili na usajili bora unahitaji umakini mkubwa.

Utashangaa hapa kwetu usajili badala ya kufanywa ligi ikiwa imesimama, dirisha lilifunguliwa na kufungwa huku ligi zetu za ndani hazijamaliza nusu ya kwanza ya msimu, unajiuliza dirisha lilifunguliwa kwa faida ya nani kama si klabu.

Pia wakati dirisha linafunguliwa mwezi Novemba hadi Desemba, kipindi hicho wenzetu hata hawafikirii kufanya usajili, unazidi kujiuliza kwani nchi yetu haifanani na nyingine kwenye mambo haya?

Ndio maana imekuwa kazi kubwa kwa Simba ambayo bila shaka ilihitaji kujiimarisha zaidi kwa kusajili wachezaji wazuri na bora zaidi kutoka nje kama wanavyofanya wenzake kina Al Ahly, Vita Club na JS Saoura.

Ni wazi kwa kanuni ya usajili wa nchi yetu haiwezekani kwani mchezaji akisajiliwa atakosa Sifa kwa kuwa hawezi kucheza kwenye ligi yetu ya ndani, hivyo ni bora kanuni hii ikaangaliwa upya kwa faida ya maendeleo ya soka letu.