TASWIRA YA MLANGABOY : Kampeni zinakuja wasanii wasipojipanga watapotea

Friday February 28 2020

Kampeni zinakuja wasanii wasipojipanga watapotea,maigizo, muziki na uchekeshaji ,WANASIASA,

 

By Andrew Kingamkono

MSIMU wa mavuno unakuja kuna watu wanapata na wengine wanapotea baada ya mavuno, ndiyo hali ya maisha ya kawaida Tanzania.

Nasema msimu wa mavuno kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na wasanii wengi wamekuwa wakifaidika kutokana na kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani kwa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vya siasa kuwatunia.

Kampeni zinapozinduliwa tumeona wasanii wakitumika katika mikutano mbalimbali ya kisiasa kwa lengo la kutoa burudani kwa watu wanaohudhuria mikutano ya kisiasa.

Katika mbwembe hizo wasanii hao wa fani mbalimbali zikiwemo maigizo, muziki na uchekeshaji hutumika kama kichocheo katika kutoa burudani kwa mashabiki ili kutowachosha na maneno yao ya muda mrefu wakijinadi kuomba kura.

Wasanii hao kwa wakati wa uchaguzi hutumika pia kama sumaku ya kuvuta watu wengi kuhudhuria mikutano hiyo na kusikiliza maneno na ahadi za wanasiasa.

Mikutano hiyo ya kampeni inapofanyika bila kuwa na wasanii wa aina yoyote imekuwa ikipwaya na kukosa watu au wakijitokeza wanakuwa wachache.

Advertisement

Hivyo, kuwepo kwa wasanii katika mikutano hiyo husaidia kuongeza idadi ya watu wanaohudhuria hata kama si wanachama wa chama husika wala wapigakura.

Wasanii wamekuwa wakipata ofa nyingi za kurekodi nyimbo zinazowahusu wanasiasa au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi huku wengine wakipata ahadi za mialiko mingi.

Katika mialiko hiyo na kuandaa nyimbo wasanii wamekuwa wakilipwa fedha na wengine kupewa ahadi ya kulipwa baada ya kumalizika kwa kampeni.

Hakuna ubishi kipindi hiki ndicho wasanii wengi wanapata uhakika wa kuingiza mapato makubwa kwa muda mfupi na hilo ni jambo la kheri kwao.

Natumai na mwaka huu wengi watapata kazi na wafanye kazi kwa moyo mmoja hata kama si wanachama hai wa vyama wanavyovifanyia kampeni ilimradi lengo lao liwe ni kujipatia kipato nalo litakamilika kwa kutumia vizuri taaluma zao na kisha kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Lakini, sijui kama wasanii wamekwishajiuliza kwa nini wakati wa kampeni ndiyo wanaonekana kuwa na umuhimu na wanasiasa wote wanawafahamu tena kwa majina halisi?

Ni swali ambalo wasanii wetu hawana budi kujiuliza wanapokubali kuwafanyia kampeni wanasiasa.

Katika kampeni za mwaka huu nawashauri wasanii kuwa makini na watu wanaojiita mameneja wa kampeni, kwa sababu wakati mwingine wamekuwa wakiwatumia vibaya wasanii kwa kushindwa kuwalipa.

Ninawashauri wasanii wahakikishe wamefikia makubaliano ya kikazi kwa kuwekeana mikataba na kukubaliana kwa muda wote wa kampeni wanapofanya kazi ziwe kwa maslahi ya pande zote mbili na wenye kuwasaidia kujiendeleza katika fani na kupata haki zao bila kusumbuliwa.

Pia, wasanii wanatakiwa kutumia majukwaa ya siasa kuwanadi wagombea nao waeleze matatizo yao ili wananchi waweze kuyafahamu na wagombea nao wasaidie kuyatatua kwani muda huu ndiyo malalamiko yanaposikilizwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Ni wazi kuwa kusubiri watetewe bila kujitetea wenyewe na kutambua matatizo yao kamwe hawatofanikiwa na watabaki kulalamika miaka nenda rudi.

Pia, wasanii wanatakiwa kujua kwamba wanatakiwa kutunga nyimbo tofauti kwa ajili ya kampeni, kwa sababu kitendo cha kutumia nyimbo zao ambazo kwa sasa zinatamba ni kuziua.

Nyimbo hizo zinaweza kufa kwa sababu ukitumia wimbo wako wa kawaida utawagawa mashabiki wako kwa itikadi ya kisiasa na vyama matokeo yake unapotea sokoni.

Tumeshuhudia nyimbo na wasanii wengi wakipotea baada ya kufanya kampeni kwa sababu mashabiki wake wamekuwa na mlengo tofauti hivyo kazi za msanii zinashindwa kutamba.

Wanamuziki na wasanii wanapaswa kujipanga mapema kwa kuandaa nyimbo hizo maalumu kwa ajili ya uchaguzi.

Najua siyo dhambi kwa wasanii kuimba na kupigia watu kampeni, lakini wanapaswa kujipanga na kuhakikisha wanajua mipaka yao katika kipindi kama hiki.

Mwisho nasema hiki ndiyo kipindi cha mavuno kwa Wasanii wakijipanga watafaida na kutoka kimaisha, lakini wakicheza baada ya kampeni wengi tutawashuhudia wakiwa wamepotea katika tasnia hii.

Advertisement