WINO MWEUSI : Kamati tuzo za Mo Simba ina maswali ya kujibu

Wednesday May 22 2019

 

By Thobias Sebastian

HADI kufikia sasa, ni wazi Simba ndio mabingwa wa Ligi Kuu Bara. Hilo halina ubishi hasa kutokana na pointi walizonazo na michezo iliyosalia nayo.

Hakuna haja ya kupiga hesabu. Simba kwa ubora wake msimu huu, apewe tu taji lake la pili mfululizo.

Simba ilijipanga mapema hivyo, suala la ubingwa kwao halishangazi sana. Ilifanya usajili wa maana na kujihakikishia kikosi kipana kitakachoweza kupambana. Hakika kimepambana si tu kwenye michezo ya Ligi Kuu bali hata kimataifa.

Ni Simba hii hii iliweka rekodi ya kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kwenda kutolewa na TP Mazembe.

Hata hivyo, kwa uongozi wa timu hiyo, pamoja na mafanikio hayo, kwa sasa hawatakiwi kubweteka bali kuangalia sehemu yenye mapungufu na kurekebisha ili kutengeneza tiumu bora zaidi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.

Tukiacha hayo, kwa mara nyingine tena Simba itafanya hafla ya utoaji wa tuzo kwa klabu hiyo kwa wale waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali.

Advertisement

Tuzo hizo zilizopewa jina la ‘Mo Simba Awards’, chini ya Mohamed Dewji mmiliki wa timu hiyo, mwaka huu zitakuwa ni msimu wake wa pili tangu kuasisiwa kwake na zitafanyika Mei 30, ikiwa ni siku mbili baada ya Simba kutoka kucheza mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Katika tuzo hizo kamati imeweka vipengele 12, ambayo ni kipa bora, beki bora, kiungo bora, mshambuliaji bora, mfungaji bora, mchezaji bora mdogo, mchezaji bora wa msimu, shabiki bora, tuzo ya heshima, mchezaji bora wa kike kutoka Simba Queens ambayo ilimaliza ligi ya Wanawake ikiwa nafasi ya tatu na pointi 47.

Hata hivyo, tuzo hizo zinaacha maswali mengi kuliko inavyodhaniwa na wengi kutokana na vipengele vinavyoshindaniwa.

Nadhani kamati inaweza ikawa ina majibu yake ili msimu ujao iweze kufanya vizuri kwenye kuandaa tuzo hizo.

Kwa mfano katika kipengele cha kipa pora, wanaoshindania tuzo hii ni Aishi Manula na Deo Munishi ‘Dida’.

Hapo ndipo maswali yalianza kuibuka, inawezekana vipi Manula aliyecheza mechi nyingi akashindanishwa na Dida ambaye amecheza michezo michache.

Ilipokosea kamati hiyo ni kuweka kipengele hicho ikiwa ni wazi hakina ushindani kama ilivyo kwa mfungaji bora. Chukulia kama kutakuwa na mchakato wa mshindi kuchaguliwa kwa kura, ikitokea wamemchagua Manula, Dida atakuwa si mshindani wake kutokana na michezo michache aliyocheza, lakini wakimpigia kura Dida, Aishi atakuwa hajatendewa haki kutokana na inadi ya mechi alizocheza. Katika kipengele kingine ambacho kimeubua maswali ni kiungo bora wa mwaka. Kuna Jonas Mkude, James Kotei na Mzamiru Yassin. Swali hapa ni, Cletous Chota ‘Chama’ anakosekanaje?

Chama anacheza nafasi ya kiungo na msimu huu ameonyesha kiwango kikubwa akiwa ndio nguzo ya mafanikio Simba kwenmye mashindano yote.

Binafsi labda ningewaelewa wangekitambukisha kama kiungo bora mkabaji wa mwaka, lakini kama ni kiungo bora wa msimu Chama ndio ilikuwa kipengele cha kwanza kuwania hapa. Hapa kamati hiyo ina la kujibu.

Si jambo la kushangaza kumuona Chama katika kipengele cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwani ana stahili lakini alitakiwa kuwepo kwanza kwenye nafasi ya kiungo bora.

Kipengele kingine kilichoibua maswali ni bao bora la mwaka. Haijulikani ni vigezo vipi vilitumika kuyaacha bao alilofunga kiungo mpole, Said Ndemla dhidi ya KMC, Simba wa kishinda mabao 2-1, bao la kusawazisha la Jonas Mkude la Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya mtoano dhidi ya Nkana Red Devils na lile ambalo alifunga Maddie Kagere dhidi ya Al Ahly. Katika kipengele cha bao bora la mwaka yamewekwa matatu ambayo ni Chama dhidi ya Nkana, Kagere dhidi ya Yanga na John Bocco dhidi ya Biashara United.

Mabao ya Chama na Bocco katika kipengele hiki wala hayana shaka kutokana na ubora wake lakile lile la Kagere dhidi ya Yanga halikuonekana kuwa bora kama Kagere dhidi ya Ahly, Ndemla dhidi ya KMC na Mkude dhidi ya Nkana.

Kamati ya tuzo inatakiwa kuwa na majibu sahihi kwenye hili ili kuondoa maswali kwa wengi kuhusu vipengele hivyo.

Advertisement