Kama hamjui, Stars ni zaidi ya Simba na Yanga

Thursday September 6 2018Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By JOSEPH KANAKAMFUM

HATUWEZI kukaa kimya bila kukosoa yale ambayo hayapo sawa kwenye michezo hususansoka, hasa katika kuweka mbele mapenzi kwa Simba na Yanga.

Tukumbuke miaka kadhaa iliyopita hasa kabla ya ujio wa Kocha Marcio Maximo Stars ilipocheza watazamaji walihesabika

Stars ilikuwa imegawanyika kwa Usimba na Uyanga. Mashabiki waliwahesabu wachezaji wao, Simba wangapi na Yanga wangapi. Wale ambao idadi ya wachezaji wa timu yao iliyokuwa kubwa, basi hao ndio waliojazana uwanjani kuishangilia huku wengine wakijitoa!

Kocha Mbrazili, Maximo ambaye alikuja wakati mwafaka na nchi ikampata kocha aliyekuwa na saikolojia ya kuwajua watu wa nchi hii wanataka nini na yeye awape nini. Maximo aliibadili taswira ya nchi hii na kuifanya Stars kuwa ni zaidi ya kila kitu.

Timu ya taifa ni muhimu kwa maendeleo ya soka letu, Maximo akatuelewesha kwa nini tunatakiwa kuwa na furaha kuishabikia na kuipigania nchi yetu na kuipa thamani jezi na bendera ya Tanzania.

Haikuwa kwa mashabiki tu, bali hadi kwa wachezaji waliiona thamani hiyo. Maximo akaingiza utu kwa wachezaji wanaochaguliwa kuitumikia timu hiyo. Wachezaji wa Stars wakapata posho nzuri wakakaa kwenye hotel nzuri. Matokeo yake ndani ya uwanja yakaanza kuwa mazuri kiasi, timu ikawa inacheza mechi nyingi kubwa dhidi ya mataifa makubwa. Ikaanza kufanya vizuri kwenye michuano mikubwa na hata kama ilipoteza si kwa kufungwa mabao mengi tena, bali ilitolewa au kufungwa kwa tabu kiasi.

Ingawa kikubwa ikawa ni jinsi Watanzania tulivyoanza kuipenda timu ya taifa pengine kwa ulinganifu sawa na ule wa Simba na Yanga. Ikawa fahari kuwaona watu wakivaa jezi za Stars, kubeba bendera zenye rangi ya taifa, kuvaa skafu na kubeba vipeperushi vya Stars .

Kwa upande wa wachezaji wakaanza kuona umuhimu wa kuitwa Stars kwa sababu thamani zao zilipanda maradufu. Wachezaji wakawa na nidhamu ya kumsikiliza kocha. Wakawa na nidhamu hasa pale walipoitwa na kuripoti kambini. Nidhamu ikawa kubwa Watanzania wakasahau ule Usimba na Uyanga hata kama wachezaji wa timu mojawapo walikuwa wengi ndani ya kikosi cha Stars.

Hili ndilo ambalo Kocha Maximo alilijenga Taifa Stars. Huku nje kocha huyo akajenga na kuitangaza Stars kuwa kubwa zaidi ya kitu chochote, Stars ikawa kubwa.

Jumamosi Septemba 8, Taifa Stars inaenda jijini Kampal akucheza dhidi ya Uganda katika mchezo wa pili ili kupata nafasi moja kati ya mbili ya kwenda kwenye fainali za Afrika kule Cameroon mwakani.

Ni mchezo muhimu ambao Watanzania tunatakiwa tuwe pamoja kuhakikisha tunashinda. Wachezaji wetu wanatakiwa kuvaa uzalendo nakuipenda timu yao ya taifa na kupigana sana watakapokuwa uwanjani. Hawana budi kujitoa ili kumfanya kocha wetu mpya, Emanuel Amunike aendelee kuipenda Stars yetu ili atoe nguvu zake zote kuelekea michezo tunayokwenda kuikabili .

Siku hizi mbili kabla ya Taifa Stars kuingia kambini kulitokea msuguano usiokuwa na tija baada ya wachezaji sita wa Simba kuchelewa kujiunga na wenzao mapema kama walivyoamuliwa kitendo kilichosababisha Kocha Amunike kuwaengua katika timu hiyo. Hilo likaleta mtafaruku mkubwa kwa viongozi mashabiki na wapenzi wa Simba dhidi ya shirikisho na Kocha Amunike.

Ikawa kila mashabiki wa Simb anawatetea wachezaji wake licha ya ukweli kuwa walikuwa na makosa ya kinidhamu tena mbele ya kocha mpya. Kocha aliyekuja akiwa na morali kubwa ya kuisaidia Stars kwa hali na Mali.

Haikuwa inaingia akilini tuliposikia na kuona utetezi wapenzi wa Simba kuwa wachezaji hawakuwa na makosa na badala yake wakaanza kushusha shutuma nyingi kuelekea kwa kocha, ikafikia hadi baadhi ya mashabiki hao kusema hadharani kuwa wataishabikia Uganda badala ya Stars.

Ni aibu kwa Watanzania wa aina hiyo ambao mtazamo wao umekuwa wa kishabiki zaidi wanatakiwa kuelezwa Taifa Stars ni kubwa zaidi ya Simba.

Na wachezaji wao, wajue kuwa Taifa Stars ni utambulisho mkubwa kwao ni nembo kubwa. Unapokuwa mbele ya watu wa nchi nyingine, timu hizi zinaweza kufutwa na kufungiwa lakini Stars haiwezi kufa wala kupotea!

Advertisement