INAWEZEKANA: Juventus ubingwa unanukia, lakini walete kizazi kipya

Muktasari:

Wameshinda Ligi Kuu ya Italia mara sita mfululizo na wapo njiani kushinda kombe hilo kwa mara ya saba mfululizo.

MSOMAJI, Juventus wametawala soka la Italia kwa miaka mingi. Wameshinda Ligi Kuu ya Italia mara sita mfululizo na wapo njiani kushinda kombe hilo kwa mara ya saba mfululizo.

Nchini Italia klabu kongwe kama Inter Milan, Napoli, Roma na AC Milan wote wameshindwa kuwapa Juventus upinzani mkubwa katika Ligi Kuu na Juventus wamepata mafanikio makubwa hata katika Ligi ya Mabingwa. Chini ya uongozi wa Massimiliano Allegri klabu hiyo imefikia fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili katika misimu mitatu.

Hakika Juventus wamekuwa na kizazi cha dhahabu ambacho kimeibeba timu hiyo katika njia ya mafanikio.

Ni wachezaji kama Buffon, Chiellini, Marchisio, Barzagli, na Lichsteiner.

Pia timu hiyo imesajili wachezaji wazuri katika misimu ya hivi karibuni kama Higuain na Khedira ambao wote wamesaidia kuongeza kiwango cha Juventus.

Hata hivyo, wachezaji hawa wote wameshafikia umri mkubwa na msimu huu huenda ni nafasi yao ya mwisho kushinda Ligi ya Mabingwa.

Lakini, wiki iliyopita Juventus walifungwa katika uwanja wao wa nyumbani magoli 3-0 na Real Madrid na wana nafasi ndogo sana kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Kwa mtazamo wangu, Juventus watahitaji kuanza mchakato wa kubadilisha kizazi chao baada ya msimu huu kama watataka kuendelea kupata mafanikio na kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa.

Ni kweli kwamba Juventus wana wachezaji chipukizi kama Dybala na Costa lakini ngome ya timu hiyo itahitajika kubadilishwa kuanzia sasa.

Lakini, soko la wachezaji limebadilika tangu Juventus walipomsajili Chiellini kwa pauni milioni nane mwaka 2005.

Hakika Juventus ni klabu yenye fedha nyingi sana lakini kama wanataka kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuziba pengo la wachezaji kama Buffon, na Chiellini basi watahitaji kulipa fedha nyingi sana kwa kuwa, wachezaji wenye kiwango hicho wanataka kucheza katika klabu kubwa zaidi kama Barcelona au Real Madrid.

Kiwango cha kikosi cha dhahabu cha Juventus kimeshaanza kushuka na nafasi ya klabu hiyo kushinda Ligi ya Mabingwa itaanza kupungua kila msimu.

Juventus bado ni klabu kubwa zaidi nchini Italia lakini sitashangaa kama hatutawaona katika fainali ya Ligi ya Mabingwa tena kwa miaka mingi. Kupata kizazi kipya chenye uwezo wa kuvaa viatu vya akina Buffon.