JAMVI LA KISPOTI : MO, kabla ya kurejea ungewaomba radhi Simba

Thursday January 16 2020

mashabiki - wanachama wa Simba -Fainali ya Kombe la Mapinduzi- Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba- Mohamed Dewji 'MO' -

 

By Khatimu Naheka

ULITOKEA mshutuko mkubwa kwa mashabiki na wanachama wa Simba baada ya kupoteza mchezo wa Fainali ya Kombe la Mapinduzi. Hayakuwa matokeo hayo, bali ni hatua ya Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Mohamed Dewji 'MO' kuamua kujiuzulu nafasi hiyo.

MO alifikia uamuzi huo akichukizwa na hatua ya timu yake kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Mtibwa Sugar na dakika chache baadaye akatuma ujumbe huo ambao uliwashtua wengi akihusisha maamuzi yake hayo na kile kilichotokea katika Uwanja wa Amaan kwani hakutaka kuona timu yake ikipoteza kirahisi.

MO ambaye pia ni mwekezaji katika klabu hiyo uamuzi uliwaumiza na kuwashtuka kutokana na kile anachkifanya sasa ndani ya Simba. Haipingiki kwamba tangu amechukua uaumuzi wa kuwekeza Simba imebadilika kwa kiasi kikubwa.

Simba imepiga hatua kwa kulikuza jina lake na heshima yake ndani na je ya mipaka ya Tanzania. Haiwezi kuwa bure ni kutokana na mchango wake ndani ya klabu hiyo.

Wapo ambao pia wameuangalia uamuzi huo wa MO kwa jicho la tatu na kuona bilionea huyo kijana hakuwa sahihi katika kuandika ambacho aliandika, hakuonyesha ukomavu katika soka kwa kile alichokitathimini.

MO hakufikiria kwa kina kile ambacho ameamua kinaweza kumpa heshhima gani au kitaishusha kwa kiasi gani thamani yake katika suala la uzoefu wa kimichezo.

Advertisement

Binafsi naungana nao kwani MO kuwekeza Simba haimaanishi kwamba Simba isifungwe. Hakuna namna hata kama aweke na kutumia trillioni lakini Simba itakuja kufungwa tu kama ambavyo Manchester City inapoteza dhidi ya Wolves na klabu nyingine zikipoteza.

Niliwahi kuandika huko nyuma kwamba kuna mambo ambayo viongozi wa soka wanayafanya yanawapotosha mashabiki wengi wa soka na kuwafanya kuamini soka lina matokeo ya aina moja tu, kushinda.

MO hataki kusikia Simba imefungwa sawa, lakini hali hiyo inawezekana vipi katika soka la ushindani ? Simba ikifungwa si ndio ukomavu wa kujua wapi wanakosea kisha wajipange sawa?

Simba ndani yake wapo mashabik wengi ambao wamerejea kuiamini klabu hiyo kupitia dhamira ya MO ambao kupitia andiko lake tena katika mitandao ya kijamii wameumizwa sana hasa wakati huu ambao klabu hiyo inatafuta wanachama wengi kujiunga na mfumo mpya wa usajili wa wanachama wao.

Kama MO anashindwa kuwa mvumilivu unaweza kuona ni jinsi gani anawaanda kisaikolojia mashabiki na wanachama wake kwamba Simba sio klabu ya kufungwa na inawezekana ipo siku watamuandama yeye kama kiongozi mkuu kama Simba ikipoteza.

Hatua mbaya zaidi kwa MO hata kama wapo ambao wanapambana kusema kuwa kuna mtu aliiandika katika akaunti yake, hiyo bado hakuonyesha heshima kwa wanachama wa klabu hiyo ambao walimpa dhamana hiyo sio kwa kiutumia mitandao ya kijamii kwa mkutano rasmi ulioonyeshwa karibu nchi nzima.

Hii ni heshima aambayo mashabiki na wanachama wa Simba waliamua kumpa MO kwa kuona dhamira yake ndani ya klabu hiyo sasa kuamua kwenda kungíatuka katika mtandao ni kuwakosea heshima.

Sidhani kama MO alipaswa kutamka kurejea pekee katika majukumu yake. Nadhani kwanza alipaswa kuwaomba radhi mashabiki na wanachama wake kwa hatua ambayo aliichukua haikuwa na upeo wa kujenga zaidi ya kutoa taswira pana kwamba bado ana safari ya kujifunza zaidi katika uvumilivu wa kujenga kioe nachokusudia.

Inawezekana hapa kwetu bilioni 4 ambazo anadai amezipoteza kwa kugharamia timu hiyo zikaonekana nyingi lakini sidhani kama MO alitaraji mambo kuwa sawa kwa haraka kiasi hiki wakati ambao bado Simba inahitaji utulivu wa kujenga timu baada ya kupata kocha mpya, Sven Vandenbroeck ambaye kwa vyovyote hawezi kusema tayari ameishaijenga timu anavyotaka.

Simba bado ina mapungufu mengi. Nafikiri MO anatakiwa kuelewa yapo ambayo aliwaahidi Wanasimba kuwa ataleta wachezaji wa kutoka katika soka la ushindani wa Ligi za Afrika Caf ngazi ya klabu lakini mambo hayakuwa hayo tukashuhudia wanakuja wachezaji kutoka Amerika kama Brazil na wengine kuanza kutimuliwa lakini bado Wanasimba walimvumilia.na hawakutaka aondoke.

Advertisement