ROHO NYEUPE: Iko wapi ile Yanga yenye jeuri, kiburi cha karne?

Muktasari:

Kama si  vigogo wachache wakubwa kuwa na mapenzi binafsi na Haruna Niyonzima, habari yake ilikuwa imekwisha. 

NINAFURAHISHWA sana na mnyukano unaoendelea baina ya Yanga na staa wake Donald Ngoma. Ni filamu fulani tamu hivi, kama zile za Bongo muvi.

Kwa kifupi Ngoma anaipasua kichwa Yanga. Inadaiwa kuwa aliaga anakwenda kwao Zimbabwe kwa siku kadhaa. Hata hivyo siku hizo zimekwisha tangu mwanzoni mwa mwezi huu lakini bado hajarejea, tena bila kutoa taarifa yoyote.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa ni kwamba kila wakimtumia Ngoma ujumbe, amekuwa akiwachunia. Inashangaza sana. Mfanyakazi anaamua anachojisikia.

Kwa kifupi ni kwamba Ngoma anawasumbua sana Yanga. Tangu Januari mwaka huu Ngoma amekuwa msumbufu kweli kweli. Alianza matatizo hayo wakati wa michuano ya mapinduzi kule Zanzibar.

Baada ya hapo ikawa ni mwendelezo. Kuna wakati uongozi ulidai kwamba haumwi bali hataki tu kucheza. Mwenyewe akajibu kuwa uongozi unadanganya kwani yeye ni mgonjwa. Ni mnyukano kwelikweli.

Ukiutazama mnyukano huu kwa kina ni kwamba kuna sehemu Ngoma anaikosea heshima Yanga. Mchezaji anawezaje kuwa nje ya timu bila ruhusa? Kwanini uongozi unashindwa kuwa na kauli inayoeleweka juu ya utovu huo wa nidhamu? Wanamlealea tu. Kwani Katiba na kanuni na mkataba wenyewe vinasema?

Nimeona majuzi kocha mkuu, George Lwandamina akisema kwamba hamtaki tena mchezaji huyo katika kikosi chake. Amekwenda mbali na kusema kwamba kama atarudishwa, basi yeye anaondoka.

Lwandamina ni kama amenunua vita hiyo baada ya kuona uongozi hauna kauli kwa Ngoma. Uongozi unashindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya utovu wa nidhamu vya staa huyo wakati uongozi hautakiwi kuyumba kwa mchezaji.

Iko wapi ile Yanga yenye kiburi? Yanga haijawahi kusumbuliwa na wachezaji wake. Siku zote watu wa Yanga wanakwambia klabu yao ni kubwa kuliko wachezaji. Wanasema Yanga mbele, nyuma mwiko. Kimekwenda wapi kiburi hiki? Pengine umasikini wa sasa unachangia.

Yanga iliwahi kuachana na kikosi kizima miaka ya nyuma na wala haikujali. Wachezaji hao waliondoka na kwenda kuanzisha timu ya Pan African miaka ya 70, lakini watu wa Yanga wala hawakujali. Iko wapi jeuri hii?

Yanga huwa inampa mkono wa kwaheri mchezaji yeyote anayewasumbua.

Miaka miwili nyuma ilitangaza kuvunja mkataba wa Haruna Niyonzima ambaye alichelewa tu siku chache kujiunga na timu hiyo.

Kama siyo vigogo wachache wakubwa kuwa na mapenzi binafsi na Niyonzima, habari yake ilikuwa imekwisha. Ikumbukwe kwamba Niyonzima alikuwa anaachwa wakati akiwa kwenye ubora wake, siyo huyu wa sasa ambaye uwezo wake umeshuka.

Jeuri ya Yanga iko wapi tena? Kwanini wanakosa kauli mbele ya Ngoma?

Kama siyo Lwandamina kutoa msimamo, pengine mpaka sasa uongozi ungekuwa unambebeleza Ngoma arudi.

Ni kweli kwamba Ngoma ni mchezaji mahiri na muhimu, lakini hawezi kuisaidia tena timu hiyo kwani anafanya kazi kwa kujisikia sana. Hajitumi kama wachezaji wenzake.

Pamoja na kwamba ameifungia timu hiyo mabao zaidi ya 40 kwenye mashindano yote katika miaka yake miwili na nusu Jangwani, bado siyo sababu ya kuitetemesha timu hiyo. Mbona Tambwe amefunga mabao mengi zaidi na wala hasumbui?

Ni kweli kwamba wachezaji wengi wazuri ni wasumbufu, lakini isifikie hatua ya kuigawa timu.

Unafikiri wachezaji wengine wa Yanga wanachukuliaje suala la Ngoma?

Ni wazi kwamba wanamuona kama mtoto wa baba.

Hata akikosea hasemwi wala kukaripiwa. Siyo jambo zuri katika timu ya mpira.

Pia siyo utamaduni wa Yanga kupelekeshwa na wachezaji wake, haijawahi kuwa hivyo miaka yote.

Kwa Simba imezoeleka, mara nyingi wanasumbuliwa na wachezaji wao na wamekuwa wavumilivu.

Huyu Emmanuel Okwi amewahi kuwasumbua sana, lakini kila wakati wanamsajili upya.

Huyo Juuko Murshid amewasumbua sana, lakini bado wako naye. Hamis Kiiza aliwasumbua sana lakini bado waliendelea kuwa naye. Simba wana uvumilivu mkubwa. Huo ndio utamaduni wao. Mwisho wa yote, nasubiri kuona ni kitu gani kitatokea baina ya Yanga na Ngoma. Nasubiri kuona watamrejesha ama la. Nausubiri huo mwisho.