MTAA WA KATI : Ighalo hatakiwi kufanya maajabu makubwa Old Trafford

Muktasari:

Kumbuka, Ighalo alikuwa na maisha yake mazuri huko China. Miaka miwili aliyocheza Changchun Yatai na msimu mmoja Shanghai Shenhua, amekuwa mchezaji tajiri huko Nigeria. Huko Shanghai alikuwa analipwa Pauni 300,000 kwa wiki. Hivyo, amekwenda Old Trafford si kusaka utajiri, amekwenda kucheza timu ya ushabiki wake lakini pia kuweka CV ya daraja la juu kuwahi kuichezea.

IDION Ighalo. Siyo jina geni kwa mashabiki wa mpira wa miguu. Wamepata kuliona kwenye jezi za Watford, Changchun Yatai, Shanghai Shenhua na hata kwenye kikosi cha Super Eagles. Kilichowashtua watu ni jina hilo kwenda kuonekana kwenye jezi za Man United.

Hakuna aliyewahi kufikiria hili. Na ndio maana wanasema kwenye maisha usimdharau mtu, huwezi kujua kesho atakuja kuwa nani.

Kila mtu na bahati yake. Kwenye hilo wala hupaswi kumlaumu Ole Gunnar Solskjaer wala Man United kwa kumsajili mshambuliaji huyo. Wakati mwingine kuna kitu kinaitwa bahati na mambo yanakwenda tu bila ya kusukumwa.

Kwa Ighalo hivyo ndivyo mambo yalivyo. Mambo yake yamekuwa mazuri kwa siku za karibuni hasa kwenye mchezo wa soka. Kuna wanaodai kwamba pengine kuwa chini ya wakala Mnorway Atta Aneke kumechangia kuchukuliwa na Kocha Mnorway Solskjaer huko Old Trafford.

Hilo tuachane nalo, halina nafasi. Ukweli ni kweli Man United ilihitaji straika kwa udi na uvumba. Baada ya kuwakosa wale iliowahitaji, basi hawakuwa na namna. Wanasema Simba hula nyasi anapokosa nyama. Wakati washambuliaji wengine wakionekana kuwa na mlolongo mrefu katika kuachana na timu zao, Man United ilikuwa ikikimbizana na muda. Shanghai Shenhua walimweka Ighalo ubaoni na Man United hawakuwa na namna zaidi ya kwenda kunasa tu saini yake.

Kumbuka, Ighalo alikuwa na maisha yake mazuri huko China. Miaka miwili aliyocheza Changchun Yatai na msimu mmoja Shanghai Shenhua, amekuwa mchezaji tajiri huko Nigeria. Huko Shanghai alikuwa analipwa Pauni 300,000 kwa wiki. Hivyo, amekwenda Old Trafford si kusaka utajiri, amekwenda kucheza timu ya ushabiki wake lakini pia kuweka CV ya daraja la juu kuwahi kuichezea.

Aliondoka Ulaya kwenda China kutafuta utajiri, amepata na sasa amerudi tena Ulaya kuendelea kucheza soka.

Ile siku ya mwisho ya kufunga usajili, Man United walikuwa bize na Bournemouth kumtaka Joshua King. Lakini, Bournemouth wakawa wanahitaji Pauni 20 milioni. Man United halikuwa lengo lao kusajili mshambuliaji kwa pesa nyingi ndani ya Januari.

Walihitaji zaidi mchezaji wa mkopo au hata wa gharama ndogo na ndio maana walihusishwa pia na Edinson Cavani. King akagomewa nafasi ya kwenda Old Trafford, lakini Ighalo akaipokea kwa mikono miwili. Sasa mpira upo kwenye miguu ya Ighalo kuwathibitishia watu wanaombeza vinginevyo.

Man United inahitaji mabao, akiweza kulifanya hilo bila ya kujali amefunga kwa staili gani, jambo hilo litamfanya kuwa salama Old Trafford.

Hakuna atakayemlaumu sana kama Anthony Martial ameshindwa kumaliza tatizo hilo. Alexis Sanchez ameshindwa na hata Romelu Lukaku amefeli kwenye maisha yake ya Old Trafford. Kutokana na hilo, Ighalo wala hahitaji kufunga mabao ya kuwapitisha watu mipira ya tobo kuhesabika amefanikiwa Man United.

Anachopaswa kufanya ni kufunga tu na kuisaidia timu kwenye vita ya kuisaka Top Four. Akiweza kulifanya hilo, basi atahesabika kama mmoja wa wachezaji muhimu. Henrik Larsson alinaswa kwenye dirisha la Januari kama hivi ilivyotokea kwa Ighalo na maisha yake ya Old Trafford yalikuwa matamu kiasi cha kuacha kumbukumbu tamu kwenye kikosi hicho wakati kilipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Ighalo hana ambacho hakijui kuhusu Ligi Kuu England, ametamba kwenye ligi hiyo akiwa na Watford na alikuwa tishio kwelikweli kwa vigogo.

Kitu ambacho hakijui ni presha tu ya kuichezea Man United jambo ambalo lipo wazi hata kama ni Lionel Messi au Neymar bado angekuwa na presha kubwa kuwa mchezaji wa Man United.