IMEBAMBA: Sarri kuiacha Chelsea ni sawa ila si sigara

Muktasari:

  • KOCHA wa Chelsea Maurizio Sarri mara kadhaa amewahi kuhudhuria kwa washauri wa afya kupata njia mbadala za kuachana na uvutaji sigara uliomsababishia uraibu (addiction) lakini bado ameshindwa kuacha.

KOCHA wa Chelsea Maurizio Sarri bado anapata shida na tatizo la uvutaji wa sigara kiasi cha mashabiki kuanza kumdhihaki kwa kumwambia anaweza kuiacha Chelsea lakini si uvutaji sigara.

Wakati anatua Chelsea alikuwa gumzo sana kutokana na tabia yake wakati wa mapumziko hukimbilia kwenye vyumba maalumu na kuvuta pafu kadhaa na kwenda kuendelea na mawaidha ya mapumziko.

Mara kadhaa amewahi kuhudhuria kwa washauri wa afya kupata njia mbadala za kuachana na uvutaji sigara uliomsababishia uraibu (addiction) lakini bado ameshindwa kuacha.

Tofauti na Italia, Uingereza kuna sheria kali dhidi ya uvutaji wa sigara katika maeneo mbalimbali ikiwamo viwanja vya michezo, hivyo sheria hizi zinambana Sarri kushindwa kuvuta akiwa kiwanjani.

Sarri ni mmoja kati ya makocha maarufu wenye tabia ya uvutaji sigara unaojulikana kama ‘Chain Smokers’ hivyo kuwa mmoja wa makocha wasio mfano mzuri kwa wachezaji vijana.

Pamoja na hivyo amekuwa akiwashauri wachezaji wake kutojihusisha na uvutaji na kuwataka kutoiga tabia yake hiyo kwani inaweza kuwaletea shida katika uchezaji.

Leo nitawapa ufahamu juu ya uvutaji sigara na madhara yake kwa jumla.

MWANZO WAKE

Wengi hujitumbukiza kutokana na makundi ya marafiki kuiga mitindo ya uvutaji katika jamii zao. Wanasoka vijana hasa wale wanaobalehe hushawishiwa na marafiki wanaokuwa nao katika mitoko.

Utumiaji wa tumbaku upo wa aina mbalimbali lakini ambao ndio unafanywa kwa wingi sana ni kuvuta sigara za kipande ingawa zipo za aina nyingi ikiwamo siga, shisha, kiko na tumbaku ya kutafuna.

Wengi huvuta sigara kama burudani kwa lengo la kujipa tulizo la kiakili na kuuchangamsha kimwili.

Kwa watu kama Sarri na wavutaji wengine pengine hufanya hivyo kutokana kuondoa msongo wa mawazo au shinikizo la kimaisha ingawa wengine tayari wameishapata uteja au uraibu hali inayowafanya kuwa wategemezi wa uvutaji.

TUMBAKU INA SUMU

Uvutaji sigara ni hatari na kwa kila mtu, sumu zilizopo ndani yake ndizo zinazoleta madhara ya kiafya ikiwamo saratani na matatizo ya mfumo wa hewa. Hatari ya kutumia tumbaku unaotokana na uwepo wa mchanganyiko wa kemikali zaidi ya 7,000 ikiwamo nyingi zinazosababisha saratani mbalimbali na magonjwa mengi. Mvutaji sigara na yule asiyevuta sigara moja kwa moja ambaye huitwa mvutaji wa pili wote hupata madhara ndiyo maana zipo sheria zinazozuia kuvuta sigara katika msongamano wa watu.

Endapo Sarri angelikuwa anavuta sigara kipindi cha mapumziko wachezaji wa Chelsea aliojifungia nao katika chumba cha kubadilishia nguo, nao wangekuwa wavutaji wa pili, hivyo kuwaweka katika hatari ya madhara ya uvutaji.

Kemikali hizi huingia mwilini unapovuta na kuingia katika mapafu baadaye hunyonywa na kusambaa maeneo mbalimbali mwilini na kuleta madhara.

Madhara yake

Madhara makubwa ya kiafya ya uvutaji tumbaku ni pamoja na kusababisha saratani karibu zote ikiwamo ya mapafu pamoja na matatizo ya upumuaji na magonjwa ya moyo. Madhara kama haya ndiyo yanayosababisha mvutaji sigara asiwe salama kiafya, ndiyo maana baadhi ya makocha wa klabu kubwa za kulipwa huwajia juu wanasoka wao wenye tabia za kuvuta sigara.

Tafiti za kitabibu zinaonyesha utimamu wa mwili wa mwanasoka unaathiriwa na uvutaji wa sigara, hii ilitokana na utafiti uliohusisha wanasoka wanaovuta sigara na wasiovuta. Wanasoka walioacha kuvuta sigara walionekana kuimarika zaidi katika utimamu wa mwili baada ya wiki moja ukilinganisha na wale walioendelea kuvuta huku wakifanya mazoezi.

MADHARA ZAIDI

Kwa kawaida kinga ya mwili hujibu mapigo ili kusahihisha madhara yanayoletawa na uvutaji. Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu na kinga inapopambana mara kwa mara na kushindwa ndipo madhara lukuki hujitokeza mwilini ikiwamo magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa mengine.

Kutokana na sumu zilizomo katika sigara kuiharibu mishipa ya damu na tishu za mwili jambo hili hukuweka katika hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi.

Uvutaji wa sigara kwa muda mrefu ni chanzo cha maradhi ya moyo na kiharusi hii ni kutokana na mishipa ya damu kuharibika na kuifanya kuepeleka damu kidogo au kuzipa na kutopeleka kabisa.

Kemikali itwayo ‘Tars’ na kemikali nyingine ambazo hubaki katika mapafu baada ya mtu kuvuta. Mabaki haya huweza kuwa na mwingiliano wa utendaji wa mapafu hasa katika uchukuzi wa hewa safi ya oksijeni.

Hali hii husababisha tishu za mwili kuharibika, hivyo kuathiri utendaji za seli kwa jumla.

Madhara anayoweza kupata mvutaji mwanamichezo ni pamoja na kutokuwa na misuli imara kutokana na athari za kemikali za sumu za sigara, na pia humchangia kupata majeraha kirahisi.

Endapo ikitokea kama amepata jeraha, basi jeraha hilo huchelewa kupona. Ndio mana haishauriwi mwanasoka au mtu wa kawaida kuvuta sigara kipindi anapokuwa na majeraha.

Ukiacha hayo, uvutaji sigara ndio unaongoza kuwa chanzo cha saratani ya mapafu, karibu 90% ya vifo vya saratani ya mapafu vilichangiwa na uvutaji sigara.

Pia, ni chanzo cha saratani mbalimbali ikiwamo ya matiti, shingo ya uzazi, utumbo mpana na kibofu cha mkojo. Vilevile ni chanzo cha maradhi sugu yanayoleta mkwamo katika mapafu na shambulizi sugu la mfumo wa hewa.

Jinsi ya kuepuka

Matumizi ya tumbaku si salama, hivyo ni vizuri kuepukana na uvutaji wa sigara ili kulinda utimamu wa mwili.

Kuacha kuvuta sigara sio kazi rahisi hii ni kutokana na ukweli sigara ndani yake ina kemikali inayokufanya uwe na uraibu (addiction) hivyo hukufanya uwe unahitaji kutumia kila mara.

Unaweza kuikata akili isiwe inawaza uvutaji kwa kutumia vitu kama pipi pale unapopata hamu ya kuvuta.

Ipo njia ya kisasa ambayo mtu kama Sarri mwenye uraibu wa uvutaji siagara inaweza kutumika kuidanganya akili, kuna sigara ya ki-eletroniki ambazo zina kichungi, umbo, harufu na mwali wa moto kama sigara.

Unapoivuta hupata hisia kama unavuta sigara ya kweli kumbe ni bandia, hii pia ni njia inayotumika kukabaliana na uvutaji.

Njia nyingine ya kuachana na sigara ni kuepuka makundi au marafiki wanaokushawishi kutumia tumbaku na nenda katika sehemu za starehe zenye kukataza matumizi ya tumbaku.

Pia, unaweza kuachana na kuvuta sigara kwa kutumia kula vitu vingine kama pipi kila pale unaposokia hamu ya kuvuta.

Kuacha uvutaji ni vigumu sana kutokana na uteja unaosababishwa na viambata sumu vilivyomo katika tumbaku, hii ndiyo sababu ya kuonekana kuwa ni rahisi Sarri kuachana na Chelsea lakini si sigara. Kwa kupata ushauri wa kuachana na sigara unaweza kufika katika huduma za afya.