STRAIKA WA MWANASPOTI : Hongera Gor Mahia, Simba ijitazame upya

Tuesday February 5 2019

 

By Boniface Ambani

Al Ahly ya Misri juzi Jumamosi iliitandika Simba Sports Club mabao 5-0 jijini Cairo. Ni ndani tu ya wiki mbili tu Simba ilitoka kufungwa mabao 5-0 na Vita Club ya Congo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wakiwa kundi D.

Inatia aibu sana. Hata hivyo, ni lazima tujiulize, shida iko wapi?

Kwa nionavyo mimi Simba imekuwa ikifanya usajili wa hali ya juu, lakini usajili huo umekuwa ni kwa upande wa washambuliaji tu.

Ukweli, ukifanya usajili ni lazima uzingatie nafasi zote na sio washambuliaji pekee. Simba inaonekana imeweka nguvu zao kwenye washambuliaji na kusahau viungo wa kati, mabeki na makipa.

Unaweza ukasajili washambuliaji wazuri lakini kama huna beki, lazima utapigwa tu.

Nikiangalia kwa undani beki ya Simba ina shida. Niliweza kutazama baadhi ya mechi zao kwenye michuano ya SportPesa Super Cup na kugundua kweli wana tatizo la beki na kiungo mkabaji.

Mabao 10 ndani ya michezo miwili? Ilipaswa wajiangalie kwanza shida iko wapi? Kwa nini wanaruhusu mabao mengi hivyo? Ni dhahiri wangepata jawabu shid ni beki. Hakuwa wakabaji.

Hata ukiwa na washambuliaji hodari kama kina Emanuel Okwi, Meddie Kagere na John Boco huku safu yako ya ulinzi ikiwa inavuja itakuwa shida. Utafungwa kila kukicha. Kwenye usajili ujao, Simba wanatakiwa watilie mkazo suala zima la usajili na kwa kuzingatia idara zote huku wakiipa kipaumbele nafasi ya beki.

Huku hayo ya Simba yakitia simanzi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, wnzao Gor Mahia ilileta shangwe na nderemo kwenye nyuso za mashabiki jijini Nairobi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki baada ya kuwatungua Zamalek ya Misri mabao 4-2. Mabao ya Gor yalifungwa kwa ustadi mkubwa na Tuyisenge (2), Kipkirui (1) na Dennis The Manace Oliech alipiga moja lililoididimiza Zamalek.

Ukilitazama bao la Dennis utagundua kitu, ni bao bora sana, alitulia, akampunguza kipa na kumwacha hoi kabla ya kufunga.

Hayo ni matokeo mazuri sana kwa Gor na ni wazi usajili wao umekuwa juu sana na wamesajili kila idara. Japokuwa wamekuwa wakipoteza baadhi ya mechi lakini sio kwa mabao mengi.

Hii inaonyesha imekamilika idara zote na kipa wao, Bonface Oluoch tu ndiye anahitaji kuchangamka. Ni mzuri akiwa lamgoni japo wakati mwingine anafungwa mabao ambayo yanakuacha ukiduwaa.

Hata hivyo ushindi huo ni wa muhimu saana kwa Gor na kujiamini kwao kunachangiwa na mechi za kimataifa ambazo wamekuwa wakicheza kuanzia safari yao ya Ulaya na zile za michuano ya Afrika. Miaka ya nyuma Gor ilikuwa ni vigumu kuzifunga timu kama Zamalek na hata kama wakiifunga sio kwa idadi kubwa ya mabao.

Gor wametuonyesha hakuna kinachoshindikana ila kikubwa ni kujiamini, la sivyo utakuwa unapigwa kila wakati.

Hili ni somo kubwa kwa klabu nyingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa klabu zake hasa zile kongwe kama AFC Leopards, Yanga na Simba ambazo zimelala. Ni timu kubwa kwa majina lakini kivitendo, zinatia aibu. Ni lazima zithibitishe ukubwa wa klabu zao ndani ya uwanja na sio Kenya au Tanzania pekee, bali frika nzima.

Kwa sasa mashabiki wa Afrika wanaifuatilia Gor kujua ni klaya gani hii iliyoweza kuifunga Zamalek, moja ya klabu kubwa Afrika. Hivyo ni wazi Gor imeanza kudhihirika Afrika nzima.

Ni lazima ukanda huu ujitangaze kwa kushinda mechi muhimu kama hizi.

Kongole Gor Mahia, lakini Simba mnayo shughuli ngumu ya kufanya. Kama mtazingatia usajili kwenye dirisha la usajili lijalo kwa kusajili mabeki.

Bila kusajili mabeki na kukimbilia kusajili washambuliaji itakuwa balaa. Nadhani wale washambuliaji wako klabuni kwa sasa wanatosha. Pia izingatie usajili wa viungo wakabaji.

Pia naomba nitumia nafasi hii kumkumbuka ndugu yetu ames Odu Cobra aliyeuliwa na wanamgambo wa Al Shabaab jijini Nairobi. Odu Cobra alizikwa nyumbani kwao Ukwala, Jumamosi. Ilikuwa ni huzuni mwingi. Namtakia Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Hayo ni maoni yangu na nawatakia wiki njema.

Advertisement