Hizi ndizo Friikiki bora Ligi Kuu Bara 2017-2018-2

Saturday June 9 2018Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

WIKI iliyopita tuliyaona frikiki bora za Ibrahim Ajibu alipocheza dhidi ya Njombe Mji, Kevin Sabato na Azam na Singida United, David Luhenda na Simba. Pia, Nassoro Kapama na Azam FC na Enock Atta Agyei dhidi ya Mtibwa.

Awesu Awesu (Mwadui 2 Njombe Mji2)

Inawezekana kipa David Kisu wa Njombe Mji akawa kipa aliyekutana faulo nyingi za moja kwa moja kutoka kwa nyota kadhaa wa timu pinzani za Ligi Kuu Bara. Kuanzia ile faulo ya Ibrahim Ajibu na faulo hii ya kijana Awesu Awesu kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.

Awesuu aliungalia ukuta uliopangwa na kipa huyu wa Njombe, kisha akafumua shuti lililopita ukuta kwa juu na kwenda kuingia juu kidogo karibu na kipa huyo na kuipa bao la pili la kusawazisha kwa Mwadui.

Etienne Ngladjo ( Mwadui 2 Njombe Mji2)

Mchezo uliokuwa unaamuliwa na faulo za moja kwa moja huku Awesu kule Etienne, raia wa Burundi alifunga faulo hii akiipa timu yake bao la pili baada ya kuipiga faulo nje ya 18 huku mabeki wa Mwadui wakidhani kipa wao ameudaka mpira, lakini ulienda moja kwa moja langoni na kuiokoa timu yake na vipigo mfululizo.

Erasto Nyoni (Simba 5 Mbao 0)

Siku ambayo Simba iliamua kulipiza kisasi kwa timu hiyo ya Kanda ya Ziwa ambayo imekuwa na rekodi ya kuvisumbua vigogo vya soka nchini na kweli iliikomesha kwa kuipiga mkono.

Wakati ubao tayari ulishasomeka mabao mengi, bado beki Erasto Nyoni aliamua kwenda kuonyesha ubora wake baada ya kupiga faulo ya moja kwa moja nje kidogo ya mabeki wa Mbao waliokuwa wamejipanga mita 10 kutoka kwake na kuupitisha mpira juu ya vichwa vyao.

Yusuf Ndikumana ( Mbao 2 Mbeya City 2)

Lilikuwa bao la mapema sana katika Uwanja wa Kirumba, jijini Mwanza mchezo uliowakutanisha makocha kutoka nchi moja ya Burundi, Etienne Ndayiragije wa Mbao na Ramadhani Nzwazurino wa Mbeya City.

Mbao ilitangulia kupata mabao yao mapema kipindi cha kwanza na kuufanya mchezo uonekane ungemalizwa hivyo, lakini baadaye haikuwa hivyo. Faulo ilitokea mwanzoni mwa mchezo, huku mabeki wa Mbeya wakiwa hawajajipanga vizuri, Ndikumana aliupindisha mpira na kuingia wavuni ukimuacha kipa, Owen Chaima asijue la kufanya.

Adam Salamba (Lipuli 2 Ndanda 1)

Moja kati ya mabao bora ya faulo ni hili lililopigwa na straika huyu wa Lipuli ya Iringa ambaye kwa sasa ni mali ya Simba.

Timu zote zikiwa zinashambuliana kwa zamu ilitokea faulo mita kama 25 kutoka langoni mwa Ndanda na kipa, Jeremia Kisubi akiwa na uhakika kuwa mpira hautawapita wachezaji wake, lakini shuti kali la Salamba lilipenya ukuta na kuingia moja kwa moja wavuni.

Baraka Mtuwi (Ruvu Shooting 1 Mtibwa 1)

Hili nalo ilikuwa moja kati ya faulo za mapema zilizozipa timu mabao, ikiwa imepatikana faulo karibu na goli la Mtibwa. Kipa Benedict Tinoco aliye mmoja ya makipa waliofanya vizuri msimu huu waliopitiwa na kufungwa mabao ya faulo, alifungwa bao hili kama yalivyotokea mabao mengi ya faulo.

Baraka Mtuwi alilichungulia vizuri lango la Mtibwa na kugundua anao uwezo wa kuuvusha mpira kwenye vichwa vya wachezaji wa Mtibwa na kufanikiwa kufunga bao la kuongoza.

Asante Kwasi (Simba 1 Lipuli 1)

Lilikuwa ndilo bao zuri zaidi. Tunaweza kusema ndilo lililompeleka Asante Kwasi Msimbazi, hakukuwa na kitu kingine sana cha ajabu licha ya pia jitihada zake za kukaba hadi kivuli washambuliaji wa Simba siku hiyo. Ilikuwa ni moja kati ya faulo bora ambazo makipa bora kama Aishi Manula wanatakiwa kupigiwa na kufungwa. Adhabu hii iliyotokea mita chache kutoka golini kwa Simba pembeni kiasi kwa eneo la 18 kulia kwa Manula. Kwasi aliona jinsi wachezaji wa Simba walivyojipanga na hakutoka mbali aliupiga mpira kuuchinja kuelekea kona ya juu kabisa na Manula aliyejitahidi kuufuata bila mafanikio.

Emmanuel Okwi (Simba 1 Mtibwa1) Ilikuwa faulo muhimu kwenye mchezo, kwani ilitokea dakika za nyongeza Mtibwa ilifanya faulo ndani ya 18, huku ikiongoza kwa bao moja. Ilikuwa ni faulo iliyoiokoa Simba, kwani iwapo Okwi angekosa, basi ingekuwa imepoteza pointi zote tatu.

Okwi aliupiga mpira huo baada ya kuona ukuta wa Mtibwa umekaa vizuri huku kipa Tinocco ambaye ameonja mabao mengi ya faulo. Mpira huo ulisogezwa kidogo mbele pembeni na Erasto Nyoni na Okwi aliupiga mpira chini chini na kujaa wavuni huku kipa Tinoco aliyekuwa kama nyota ya mchezo baada ya kuokoa michomo mingi siku hiyo akiusindikiza kwa macho.

Advertisement