Hivi ndio visa vya makomandoo wao

Thursday September 27 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA THOMAS NG’ITU

KAMA kuna wakati mashabiki na mabosi wa Simba na Yanga wanakuwa kwenye wakati mgumu, basi ni pale unapokaribia mpambano wa wababe hawa wa Ligi Kuu Bara. Simba na Yanga zina historia ya kusisimua ndani na nje ya uwanja. Na zinapokutana mambo huwa mazito kwelikweli.

Kwanza, ni lazima nyasi ziwake moto kutokana na soka la kiufundi na ubabe mwingi huku mashabiki wakipambana kivingine kwenye majukwaani na baada ya mchezo. Katika mabenchi ya ufundi nako mzuka huwa mkubwa kinoma kwani, makocha huwa kwenye presha dakika zote 90 na kuna wakati wanapoteza kazi kama timu ikipata matokeo yasiyotarajiwa.

Lakini achana na ishu ya makocha na mashabiki huko Simba na Yanga kuna kundi lingine la watu ambao wamekuwa na shughuli nzito pindi timu hizo zinapokuwa uwanjani kwa kuvaana zenyewe ama na timu nyingine.

Kundi hili ni lile la ulinzi ambalo limekuwa maarufu kama makomandoo, ambao wamekuwa wakilinda timu zinapoingia uwanjani na zinapokuwa kambini. Ni ngumu sana kupenya kwenye mazoezi ya timu hizi kama makomandoo hawa wakiwa wamesimamia ulinzi wa timu zao. Panachimba.

Sasa wakati zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kipute cha wababe hao, Mwanaspoti limewasaka makomandoo wa Simba na Yanga na kupiga nao stori kuhusiana na majukumu na changamoto zinazowakabili wakati wakitekeleza kazi zao.

RAMADHAN PENTER (YANGA)

Huyu jamaa ni maarufu sana pale Jangwani na kila Yanga inapocheza amekuwa mstari wa mbele kuimarisha ulinzi kwa wachezaji. Hapa anafunguka jinsi alivyoanza kazi na majukumu yake pale Yanga.

“Nimeanza kazi kama Afisa Usalama ndani ya Yanga ni zaidi ya miaka 10 sasa, hakuna faida ambayo naweza kusema nimeipata zaidi ya pointi tatu ambazo natamani kuona timu yangu inapata katika kila mechi.

“Najivunia kuiona Yanga ikipata pointi katika kila mechi ambayo nakuwa kazini. Faida ambayo naweza kusema nimeipata ni kufanya kazi Yanga na kubeba ubingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara,” anasema.

Penter anaeleza mikasa mitatu ambayo amekutana nayo na kamwe hataisahau hadi anaachana na kazi hiyo. Misimu mitatu iliyopita katika Uwanja wa Sokoine Mbeya walikuwa wanacheza na Tanzania Prisons, walikuwa kwenye ugomvi mzito na makomandoo wa Prisons.

“Nakumbuka nilikuwa nikipambana ili kuona Yanga inafanya kweli na tunafanikiwa kwenye kila jambo tunalolitaka, lakini nikaja kushtuka nimelazwa hospitalini,” alisema.

Anafunguka zaidi katika mchezo mwingine dhidi ya Simba, nako alikuwa na kazi ya ziada kabla ya mchezo huo, ambapo pia kukaibuka utata mkali nje ya uwanja.

“Ilikuwa Uwanja wa Taifa msimu uliopita katika mechi ya Simba ambayo walitufunga 1-0 bao la Erasto Nyoni, usiku tulipigana na makomandoo wa Simba waliokuja kufanya imani za kishirikiana, lakini katika kubishana nao wakaenda kuita polisi ambao, walitukamata na wakatuweka ndani pale Chang’ombe kuanzia saa 7:00 usiku mpaka saa 6:00 mchana siku ya mechi.

“Mechi nyingine ilikuwa dhidi ya haohao Simba ambao tuliwafunga 2-0 mabao ya Amiss Tambwe na Malimi Busungu. Nakumbuka walimpasua kamanda wetu mmoja na hatukukubali tukaanza kuwashikisha adabu mashabiki wa Simba, nikajikuta nakamatwa na polisi na kutupwa selo kwa siku tatu, sitasahau tukio hili na nafanya hivi kwa kuipenda Yanga tu na si jambo lingine,” anasema Penter.

SAID COMORO (YANGA)

Hivi sasa ukiingia katika vyumba vya kubadilishia nguo pindi Yanga inapocheza, lazima utakutana na jamaa mmoja mwenye asili ya Kiarabu akiwa amesimama kuhakikisha ulinzi kwa wachezaji.

Comoro kwa kuvuta taswira anafunguka tukio kubwa ambalo hatalisahau ni walipokwenda Shinyanga, ambapo kulizuka vurugu kubwa na kurushiana mawe na makomandoo wenzao.

“Ugenini tumekuwa na changamoto nyingi kwa sababu kule wanalinda uwanja na sisi tunalinda pia. Kuna makomando walikuja sikumbuki wa Stand United au Mwadui, lakini walikuwa na mapanga na sisi tulikuwa na mawe sasa tuliwarushia mawe ili wasitusogelee. Msala ulikuja na wenyewe wakaanza kutumia mawe, basi tukapasuana sana,” anasema.

Comoro anaongeza licha ya changamoto hizo lakini, kubwa zaidi ni pale mashabiki wanapotaka kuzungumza na wachezaji, hapo huwa kimbembe unaambiwa.

Kuhusu kulinda vyumba vya kubadilishia nguo na presha ya mechi ya watani, alisema ni kawaida kwani hata Simba wanalinda wachezaji ili kuhakikisha hawanunuliwi ama kuingia vishawishi.

“Hizo ndio huwa mechi ngumu kwa wachezaji hadi kwetu makomandoo, hatuna imani na baadhi ya viongozi na mambo ya kuhonga hata kishirikina pia, sio rahisi kuona mtu anaingia kambini au vyumbani kwa wachezaji kisha tukamuacha tu. Hatuna masihara unapofika wakati huo, hatulipwi lakini mapenzi yetu kwa timu ndio jambo la furaha zaidi na tuko tayari muda wote. Kuna wakati tunatumia pesa zetu kwa ajili ya kuhakikisha usalama unakuwepo,” anasema.

ABBAS BIG (YANGA)

Ana mwili wa kazi, mbavu nene unaambiwa na ukikutana naye ni lazima ushtuke. Hapo shingoni ni lazima atupie cheni yake ya silva na mkononi kuna pete kadhaa, yaani sio wa kumchukulia poa kabisa jamaa anatisha kimtindo fulani.

Ni kawaida kabisa kumuona pembezoni mwa vyumba vya wachezaji wa Yanga akiimarisha ulinzi. Japo kwa sasa anabanwa na majukumu yake binafsi, lakini humwelezi kitu na ukimuona katuliza hapo ni lazima ujiulize mara mbili kumsogelea.

Abbas anaeleza ni miongoni mwa waliopigwa na makomandoo mkoani Shinyanga, baada ya kutaka kuingia uwanjani na wenzao wa upande wa pinzani kuwagomea.

“Ilikuwa patashika ile asikuambie mtu sitaisahau hata kidogo kwa sababu nilipigwa tofali kabisa, lakini nilikuwa freshi tu,” alisema kwa kifupi.

SHABANI MADOBE (SIMBA)

Ni miongoni mwa makomandoo wanaojitolea maisha yao kwa ajili ya Simba ili kuhakikisha mambo ya nje ya uwanja yanakuwa yametulia.

Madobe alifunguka a mara nyingi huwa anakutana na changamoto pamoja na wakati mgumu wanapocheza mechi ngumu kama ya watani zao, Yanga.

“Muda mwingine najikuta nagombana na makomandoo wa Yanga ambao, huwa tunakutana mara nyingi tu kwenye kazi zetu, lakini sitaki kuelewa hilo na huwa tunashikana mashati.

“Tunapokuwa mikoani huwa tunakutana na kazi nzito hasa kwenye mechi ngumu. Tunapambana sana na makomandoo wa timu nyingine ambao ni wabishi na hawaelewi kitu. Tunalazimika kutumia nguvu ili timu iwe salama,” alisema.

Kuhusu mafanikio anayoyapata kwa kufanya kazi hiyo, Madobe alisema: “Faida kubwa ni kufanya kazi kwa karibu na timu yetu, lakini pia mabosi huwa wanatupa kifuta jasho. Nafanya kazi ninayoipenda, nimepata fursa ya kujuana na watu wengi ambao huwa wanafanikisha mambo yangu,” anasema Madobe.

NGADE NGARAMBE (SIMBA)

Ukizungumzia makamondoo maarufu kwenye soka la Bongo, basi huwezi kuacha kumtaja huyu jamaa. Simba inapokwenda mikoani utamkuta kwenye msafara.

Kuna wakati hushiriki kweye matukio mazito ilimradi tu Simba ipate pointi tatu muhimu hususan kwenye Ligi Kuu.

Ngade anasema tangu alivyoanza kufanya kazi kama komandoo wa Simba kuanzia kuwalinda wachezaji wakiwa kambini hadi uwanjani, amepitia matukio mengi ikiwemo kuchapana makonde na wenzao wa timu za Yanga na Azam FC.

“Siwezi kusahau tukio la kumwaga maji tu ambayo niliweka ubuyu ndani yake katika mechi dhidi ya Azam FC pale Uwanja wa Taifa, yale maji hayakuwa na kitu chochote, bali niliweka ubuyu tu na lengo lilikuwa kuwachanganya wapinzani,” anasema.

Anafunguka tukio hilo hatalisahau kwani lilihatarisha maisha yake mbele ya mashabiki wa Azam ambao walikuwa na uwezo wa kumfanya jambo lolote.

Ngade anaongeza katika mchezo dhidi ya watani wao wa Jadi (Yanga) huwa na changamoto nyingi na huwa kama vita.

“Kuna mechi ambayo tulishinda bao 1-0 dhidi ya Yanga alifunga Emmanuel Okwi bao la mbali kipa wao akiwa Bartez (Ally Mustafa), usiku wa manane kabla ya mechi nilipigana na makomando wa Yanga ambao walikuwa wakilinda uwanja, tulipigana hadi wanajeshi wakaingilia kati na kutupiga, lakini hatukuondoka na tuliendelea kulinda mpaka muda wa mechi,” anasema Ngade.

“Nakumbuka Mbeya pale Sokoine tulicheza na Mbeya City tuligoma kupitia mlango rasmi na tukavunja geti na kuipitisha timu kwa kutumia mlango huo.

“Baada ya tukio hilo polisi walinipa kibano na hata mpira sikuangalia na nilikuja kutolewa na viongozi baada ya mechi. Hata hivyo mechi hiyo tulishinda 2-0 lakini sikubahatika kuona lolote, nilikuwa rumande, “ anasema.

Advertisement