HISIA ZANGU: Hivi huyu Tshabalala, kwanini asitolewe kwa mkopo

Tuesday April 10 2018

 MCL

MAISHA ya Mohamed Hussein Tshabalala pale Simba yananikumbusha maisha ya Nadir Cannavaro pale Yanga. Waende wapi? Hakuna.

Simba na Yanga ndio kila kitu katika soka letu. Bahati mbaya kuna tofauti kubwa kati ya Simba na Mtibwa Sugar kuliko tofauti iliyopo kati ya Manchester United na Southampton.

Katika hali ya kawaida, maisha yakiendelea hivi hivi kwa mchezaji anayeitwa Tshabalala pale Simba, hasa msimu ujao, basi akili ya kawaida inakutuma kuamini kwamba Tshabalala anastaili kwenda kwa mkopo sehemu nyingine kwa ajili ya kucheza.

Kwanini? Kuna sababu nyingi. Kwanza mchezaji wa kulipwa kama yeye lazima awe uwanjani na sio katika benchi. Hasa kwa mchezaji ambaye amevuka katika hatua ya kuwa mchezaji chipukizi na kuwa mchezaji mkubwa. Mchezaji chipukizi anaweza kusubiri nafasi yake.

Lakini pia alikaribia kuitawala nafasi ya kushoto katika timu ya taifa kabla ya kuibuka kwa Gadiel Michael wakati Mwinyi Haji akiwa anazembea. Namuona Tshabalala yupo mbele kwa hatua kadhaa mbele ya Gadiel.

Fahari ya mchezaji anayejitambua ni kuichezea timu yake ya taifa.

Kwa sasa Tshabalala asipoitwa hakuna anayelalamika. Ni kwa sababu hachezi.

Mashabiki siku hizi sio wendawazimu. Kama huchezi katika timu yako hawasimami nyuma yako.

Nyuma ya yote haya kuna ukweli umesimama. Mtu anayecheza katika nafasi yake, Asante Kwasi hawezi kuachwa nje kumpisha Tshabalala kwa sababu kuna michuano michache katika soka letu.

Katika soka letu kuna Ligi Kuu na FA. Bahati nzuri kwa Simba msimu huu inashiriki michuano ya Afrika.

Katika soka la Kiingereza kuna Ligi Kuu, FA, Kombe la Ligi, na ukichezea timu yenye hadhi ya Simba pale England basi utashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa au Europa.

Hapo ina maana Kwasi angeweza kupumzishwa katika baadhi ya michuano.

Ni ngumu kwa kocha kumpumzisha Kwasi katika mechi ya Ligi Kuu au ya kimataifa hasa ukizingatia kwamba timu ilitolewa mapema katika michuano ya FA. Mchezaji mahiri hawezi kupumzishwa katika mechi muhimu za Ligi Kuu wakati timu inasaka ubingwa.

Lakini kwanini Tshabalala hawezi kwenda kwa mkopo kwingine?

Jibu ni kama kwanini Cannavaro hawezi kwenda kwa mkopo kwingine wakati angeweza kucheza zaidi kuliko kukalia benchi Yanga. Kuna mengi ya wazi nyuma yake. Kama umaarufu uliupatia Yanga au Simba basi ukiondoka thamani yako inashuka. Maisha yanaanza kuwa mashakani. Raha za mjini zinatoweka. Ndege haupandi tena.

Lakini zaidi ni kwamba klabu nyingi za Ligi Kuu haziwezi kumudu mshahara wako.

Kuna wachezaji wengi ambao ni bora wakalie benchi Simba au Yanga kuliko kwenda kuishi maisha ya tabu Njombe Mji huku ukiwa na uhakika wa kucheza. Pengo la wakubwa hawa ni kubwa kuliko pengo la Manchester United na Southampton.

Ukitoka Manchester ukapelekwa kwa mkopo Southampton kuna mambo yanabadilika lakini hali haiwi mbaya kama ukitoka Simba kwenda Mbao kwa mkopo.

Maisha yanabadilika kwa kiasi kikubwa mithili ya Samaki aliyepelekwa nchini kavu.

Pamoja na yote hayo, naweza kuelewa kwanini Cannavaro aligoma kuondoka Yanga. Alitarajiwa hadi uzeeni.

Lakini kwa Tshabalala mkopo nahisi hauhepukiki. Ameanza kukalia benchi wakati damu inachemka.

Kuna baadhi ya mashabiki wanaweza kusema kwamba atacheza pindi Kwasi akiumia. Hapana.

Mpira wa kisasa hauna muda wa kusubiri mwenzako aumie. Unahitaji kucheza karibu kila mwisho wa wiki kwa ajili ya kuimarisha kipato.

Mchezaji anayehitaji kusubiri ni yule chipukizi. Mchezaji aliyefikia hatua ya kuwa mchezaji bora wa msimu hawezi kusubiri kucheza pindi mtu aliyechukua nafasi yake akiumia.

Hakuna kitu kama hiki katika soka. Walio karibu na Tshabalala wanaweza kumshauri vizuri zaidi.