UCHAMBUZI; Hili la Zahera na Kokolanya limalizwe kibusara zaidi

KIPA wa Yanga Beno Kakolanya yupo yupo tu kwa sasa. Yupo kwenye wakati mgumu baada ya kocha wake Mwinyi Zahera kutomhitaji kwenye kikosi chake kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Kakolanya alijiondoa kikosini akishinikiza kulipwa pesa yake ya usajili Sh15 milioni pamoja na mishahara yake lakini baada ya mdau wa Yanga kujitokeza na kumlipa Sh2 milioni kipa huyo alirejea ingawa kocha alimtimua.

Msimamo wa Zahera unajenga kikosi imara kwa sababu baadhi ya wachezaji kudaiwa kuwa na utovu wa nidhamu achana na kudai pesa zao kwa wale wenye matatizo kama haya, lakini baadhi wanakuwa na nidhamu mbovu ya kutaka kuwapanda hata makocha wao.

Baadhi yao wamekuwa wakichelewa kujiunga na timu zao mara wanapopata mapumziko bila kuwa na sababu za msingi huku wengine wakitumia ukubwa wa majina yao ili kuogopwa na benchi la ufundi kama tu litakuwa dhaifu.

Wachezaji wa aina hiyo ni wale walio wengi kubebwa na viongozi fulani hivyo huchukulia hawawezi kupewa adhabu yoyote kwa utovu huo wa nidhamu.

Kwa Yanga, Zahera amekuwa kocha wa kipekee kulinda nidhamu ya wachezaji wake huku akiwa mkweli kwa yule anayefanya vibaya ama kwenda tofauti na hata yule anayefanya vizuri humwambia kile anachostahili.

Zahera haishii kwa wachezaji peke yao bali hata viongozi, kwani hivi karibu baadaya ya dirisha dogo la usajili kufungwa na viongozi walishindwa kusajili wachezaji aliowapendekeza nao aliwapa ukweli hajafurahishwa na wamesajili mchezaji ambaye hajamhitaji akiwemo kipa Ibrahim Hamid.

Kwa misimamo ya Zahera, hakuna shaka kipa huyo kuwa kipa wa jukwaani kwani huenda asimtumie kabisa kwa sababu hakuwemo kwenye mipango yake ya usajili.

Yaachwe hayo ya usajili wa kipa huyo na nidhamu mbovu kwa baadhi ya wachezaji katika timu mbalimbali, lakini Yanga bado wanahitaji kuwa na Kakolanya kutokana na kikosi chao jinsi kilivyo.

Awali Kakolanya ndiye alikuwa kipa namba moja wa Zahera kutokana na umahiri wake lakini hivi sasa bado lango la Yanga halina mwenyewe kati ya Ramadhan Kabwili na Nkizi Kindoki ambaye imani kwa wanayanga ni ndogo kutokana na mechi zake za nyuma alizofungwa kizembe.

Katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya African Lyon, Kabwili aliumia na mechi ya Kombe la FA langoni alisimama Kindoki napo walishinda. Ushindi wa mechi hizo mbili haumaanishi Yanga ipo vizuri langoni.

Viongozi wa Yanga wanapaswa sasa kukaa na kocha wao baada ya kurejea nchini ili kulimaliza tatizo la Kakolanya ambaye hajaidakia timu yao kwa zaidi ya mwezi sasa tangu ajiondoe kikosini.

Busara zaidi zinatakiwa kutumika ili kuisaidia timu yao ambayo inaonekana kuwa na malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi, masilahi watakayofikia juu ya tofauti zilizopo kati ya kocha na Kakolanya yatakuwa na faida kwa klabu.

Ikumbukwe kwenye timu hakuna mtu aliye juu zaidi ya kocha, hivyo kwa vyovyote vile hata kama Kakolanya alikuwa na madai yake alipaswa kufuata taratibu za madai kwani ni wazi walio wengi ndani ya timu hawajalipwa.

Madai ya mtu ni haki yake, Kakolanya na wengine wana haki ya kudai ila mfumo unaotumika wa kudai ndiyo umekuwa tatizo kwa wachezaji wengi wa Tanzania.

Kakolanya anahitaji kucheza na anapaswa kutambua hilo kwamba ili afanikiwe zaidi ni lazima apitie changamoto bila kukata tamaa na kuzivumilia, ukata wa Yanga sasa ni muda mrefu labda siku zijazo, hivyo ni kujishusha na kufanya kazi, maana haki ya kulipwa itakuwepo tu hata iweje watalipwa tu.

Kikubwa Kakolanya ni kujali kipaji chako kwanza, mengine baadaye hata kama yanaumiza na hili la kukaa nje ya uwanja wakati si majeruhi litakuwa limekufunza sana, maana timu za Tanzania zinapokezana ukata hata ukienda sehemu nyingine napo kuna siku watakwama kukulipa kwa wakati, ukiwa mvumilivu unatengeneza uaminifu ndani ya klabu na benchi la ufundi.

Tatizo limekuwa sugu kwa timu nyingi achilia mbali kwasasa ambapo ni timu chache ikiwemo Simba, Azam, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na timu za majeshi ndizo zenye uhakika wa mishahara ya kila mwezi na pesa za usajili, zingine hali zao kiuchumi ni mbaya.

Zahera kama kocha anapaswa pia kuvaa uhusika wa mzazi kwa mchezaji, Kakolanya amefanya kosa ila unapaswa kumwadhibu kama mzazi na sio kumwondoa kabisa kikosini wakati kama huu ambao unahitaji ubingwa. Mwadhibu kipa huyo adhabu ambayo haitaithiri timu kipindi hiki.

Mwisho, kazi itakayobaki baada ya Zahera kumsaheme mchezaji wake na kumrudisha kundini ni viongozi kupambana kuhakikisha wanapata pesa za kuwalipa wachezaji wao ili mambo kama haya yasijitokeze kwa mchezaji mwingine ndani ya timu.