Hii ndio njia mwafaka kutatua shida za Yanga

KLABU ya Yanga ni moja ya klabu kongwe kwenye soka hapa nchini, ilianza kuzaliwa kuliko Simba. Yanga ilianzishwa mwaka 1935 wakati Simba wao wakizaliwa mwaka uliofuata 1936. Mwaka mmoja mbele unatosha kabisa kuwa ni kubwa kuliko watani wao ambao sasa wanajivunia mafanikio makubwa waliyoyafikia hata kama bado hayajaanza kuwalipa.
Klabu nyingi zimeingia kwenye mfumo wa hisa na Simba sio klabu ya kwanza hapa nchini kuingia kwenye mfumo huo lakini ni ya kwanza kwa Yanga ambao ni wakubwa kwao, hivyo akili zao zimeona mbele haraka kuliko Wanajangwani.
Baada ya kuona mambo ya uendeshaji wa timu na klabu kwa ujumla unahitaji pesa nyingi, Simba walikaa chini na kujadili kwa mapana japokuwa kulikuwepo na vikwazo vingi vya kuzuia mchakato huo lakini ilifikia hatua wakafanikiwa na sasa hatua iliyofikia ni nzuri.
Kama ni nyumba kwa Simba basi hata bati wamepiga baada ya kufanya uchaguzi na kuwapata wawakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi kwa upande wa klabu ambao wameungana na wale wa upande wa Mwekezaji sasa mambo ni utekelezaji tu.
Bodi nzima ya Wakurugenzi imeundwa ambayo itakuwa chini ya Mwenyekiti wao Mohamed Dewji 'Mo Dewji' ambaye ndiye mwekezaji mkuu kwa kumiliki hisa asilimia 49 huku wanachama wakibaki na asilimia 51.
Kupata mafanikio sio kazi rahisi, utakutana na vikwazo, utakata tamaa lakini ukiwa na nia utafanikisha jambo lako ndivyo ilivyokuwa kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Shughuli kubwa upande wa Yanga, uchaguzi tu huu unaoendelea sasa unanikumbusha uchaguzi wao uliopita ambao ulimuweka madarakani Yusuf Manji maana nao hadi serikali iliingia na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia kamati yake ya uchaguzi iliingia kusimamia na watu walichukuwa fomu TFF ila baadaye ilibidi shirikisho liruhusu Yanga wausimamie wenyewe uchaguzi wao.
Sasa hivi ni kama vurugu tu ndani ya Yanga, bado hakijaeleweka nani atasimamia uchaguzi huo baada ya Yanga kushikilia msimamo wao kwamba watasimamia wenyewe na nafasi watakazojazi ni ya Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wengine waliojiuzulu huku Yusuf Manji wakiendelea kumtambua kama Mwenyekiti.
Manji aliandika barua ya kujiuzulu tangu Mei 20 mwaka jana na imedaiwa kufanyika vikao vingi vya kumbembeleza arejee baada ya wanachama kupinga uamuzi wake wa kujiuzulu ila jitihada za watu mbalimbali ikiwemo serikali na TFF kugonga mwamba.
Sintofahamu iliyopo sasa ni kwamba George Mkuchika aliwatangazia Wanayanga kwamba Manji alijibu barua yake ya kukubali kuendelea kuwa Mwenyekiti wao lakini kinachowachanganya watu ni huo muda wa Manji kurejea kwenye majukumu yake Januari 15 wakati uchaguzi ni Januari 13.
Yakiachwa hayo yote, ni kweli Yanga ina matajiri wengi lakini je, wana moyo wa kujitolea kuisadia Yanga kwa kipindi hiki ambacho imeyumba kiuchumi. Inawezekana ama haiwezekani kuwepo, kikubwa kitakachowasaidia ni kubadilisha mfumo wa uendeshaji tu.
 Hiyo ndiyo njia pekee ya kuikoa Yanga na sio kuendelea na malumbano hayo maana hata Manji akirejea bado wanahitajika kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu yao. Inawezekana pia kumuhitaji Manji kipindi hiki ni ili awalipie hayo madeni hasa kwa wachezaji wao ambao wanadai mishahara na hata pesa za usajili ndipo waingie kwenye mfumo mpya.
Yanga inahitaji mabadiliko makubwa ya kujiendesha kulingana na ukongwe wao katika soka, TFF na serikali wanaweza kukubaliana na Yanga kuwaachia wajisimamie wenyewe uchaguzi wao lakini sio njia ya utatuzi wa kuendesha klabu yao kwa mafanikio. Mabadiliko ndani ya klabu yanahitaji kwani hata huyo Manji ana mambo yake ya kufanya ipo siku atahitaji asimame yeye na familia yake kwa maana ya kuachana na mambo ya mpira, basi na huo ndiyo utakuwa mwisho wa Yanga.