Hii hapa chungu, tamu Ligi Kuu ya Wanawake

Muktasari:

  • Kocha wa JKT Queens, Ali Ali alisema kukosekana kwa motisha ya zawadi kwa bingwa, mchezaji bora, kocha bora, mfungaji bora, kushiriki michuano yoyote ya kimataifa kunaondoa morali ya kuonyesha ushindani mkubwa.

LIGI Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL), tofauti yake na Ligi ya wanaume (TPL) ni bingwa akipatikana kwa wanaume anapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, anachukua kombe, pesa pia zinakuwepo zawadi kwa mchezaji bora na kinara wa mabao.

SWPL mambo ni magumu kwani bingwa akipatikana zawadi kubwa anayopewa ni kombe, hakuna Mfungaji Bora wala Mchezaji Bora, isitoshe hawashiriki michuano ya kimataifa ligi ikimalizika wanasubiri msimu mwingine.

Pamoja na mwanzo ni mgumu, changamoto kubwa iliyotajwa kwenye ligi hiyo ni ukata uliofanya wachezaji waingie uwanjani miguu yao ikiwa imevimba na kusababisha kushindwa kuonyesha uwezo wake kikamilifu.

Baadhi ya viongozi wa timu zilizoshiriki ligi hiyo akiwemo Katibu wa Evergreen, Salim Luheka ‘Nonji’ amefunguka mambo waliopitia mpaka kushuka daraja kuwa ni umaskini.

Nonji anasema ilikuwa inafikia kipindi wakienda kucheza mkoani wanafika siku ya mechi, wachezaji wao wakiwa hawajala, hawajapumzika, miguu imevimba, wanashindwa kufanya mazoezi ya kupasha misuri halafu wanaingia moja kwa moja kucheza mechi.

“Ukitazama mechi ambazo sisi tulishinda ni zile ambazo tulicheza Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, mkoani kwa asilimia kubwa tulichemka kwani tulikuwa tunafika muda wa mechi kwa maana ya kushuka kwenye basi na kuingia kucheza, kuna siku tulikwama njiani halafu ujue hawa ni watoto wa kike, ligi imeisha hatuna budi kujipanga upya,” alisema Nonji.

Kocha wa JKT Queens, Ali Ali alisema kukosekana kwa motisha ya zawadi kwa bingwa, mchezaji bora, kocha bora, mfungaji bora, kushiriki michuano yoyote ya kimataifa kunaondoa morali ya kuonyesha ushindani mkubwa.

“Mfano mzuri msimu uliopita, tuliambulia kupewa kombe bila hata pesa, hii inaumiza hakuna tunachowania, TFF waboreshe vitu hivyo msimu ujao ili kujenga ushindani wa kweli.

“Kifupi kwenye ligi ya wanawake mambo bado kabisa, jambo lingine hata hat-trick ambazo wachezaji wetu walikuwa wanafunga wamewahi kupata mipira watu wawili tu ambao ni Asha Rashid ‘Mwalala’ na alifunga mabao matano kati ya 15, tulipocheza na Marsh Queens Uwanja wa Karume.

“Mchezaji mwingine alipewa mpira ni Fatuma Mustapha ‘Kitu Nini’ tulicheza na Evergreen, alifunga mabao manne, sio kwamba walifunga hat-trick mara moja ni zaidi ya mara tano,” alisema.

Huko Panama ya Iringa, nako walikuwa wanakwama mpaka pesa ya kulala hotelini kuna wakati hata chakula walikuwa wanapewa na wapinzani wao wanaotaka kucheza nao mechi, iliwatokea walipocheza na Kigoma Sisterz na Marsh ya Mwanza.

Kocha Adam Fundi aliweka wazi namna ambavyo walikuwa na changamoto ya kubwa msimu huu

“Ngumu sana kumuomba mpinzani wako msaada wakati mna mechi inapunguza kujiamini kwa wachezaji wetu, jambo zuri hiyo michezo tuliambulia sare, Shirikisho la Soka nchini (TFF) waboreshe udhamini.”

KAULI ZA WACHEZAJI

Staa wa Simba Queens, Mwanahamis Omary alisema wanacheza soka kwa sababu ya mapenzi bila kuangalia changamoto ambazo zingewakatisha tamaa, kuona hakuna wanachoambulia kwa madai kwenye ligi hiyo kuna ukata wa hali ya juu.

“Tuna vipaji, tunaamua kujitoa mhanga ili kutengeneza misingi mizuri kwa wengine, ligi ina ushindani na nzuri, shida ipo kwenye pesa yapo mambo ambayo kwa baadhi ya timu walikuwa wanashindwa kutimiziwa ilikuwa inashusha ari fulani ya kujituma,” anasema.

Nahodha wa Marsh Queens, Elieth Edward Kulwa anasema ligi ina ushindani, isipokuwa ukata uliwafanya washindwe kuonyesha makali ya miguu yao kwa asilimia 100, kutokana na kukosa baadhi ya vitu vya msingi.

“Ili mchezaji afanye vizuri, lazima awe vizuri kiakili kwa maana ya kutimiziwa mahitaji yake ya msingi ambayo yatamfanya akili yake ielekeze kwenye kazi, tulipambana kadri tulivyoweza,” anasema.