Hao Simba, Yanga wanalijua kwata la kibabe la JKT Queens

Muktasari:

  • Katika mechi 21 ambazo Simba Queens wamecheza wamefanikiwa kuvuna pointi 44 sawa na Alliance Girls, Mlandizi na Panama 42, Kigoma Sisterz 28, Yanga Princess 25, Baobab 20, Tanzanite 19, Marsh 15, Evergreen na Mapinduzi 9.

SIMBA Queens na Yanga Princess pamoja na kuungwa mkono na nyomi ya mashabiki wanaozisapoti timu zao za wanaume, bado wamepigishwa kwata na JKT Queens ambao hawakamatiki kwenye pointi, mabao na vinara wa kuzifumania nyavu.

Inasubiriwa Panama ya Iringa kama inaweza kutibua rekodi ya JKT Queens ambayo haijafungwa katika mechi zao 21 na watacheza nayo Jumapili ya wiki hii itakayokuwa ya hitimisho ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL) kwa msimu huu.

Achana na JKT Queens kuwa mabingwa kwa pointi 63 wanazomiliki na mabao 123, wameziacha mbali sana Simba Queens na Yanga Princess ambazo zinaungwa mkono na timu zao.

Katika mechi 21 ambazo Simba Queens wamecheza wamefanikiwa kuvuna pointi 44 sawa na Alliance Girls, Mlandizi na Panama 42, Kigoma Sisterz 28, Yanga Princess 25, Baobab 20, Tanzanite 19, Marsh 15, Evergreen na Mapinduzi 9.

Pamoja na JKT Queens, kujulikana bingwa kabla ya mechi yao ya mwisho na Panama kupigwa siku ya Jumapili Uwanja wa Mbweni, msemaji wa timu hiyo Elizabeth Buliba alizitaja Simba Queens na Yanga Princess kwamba uwepo wao kwenye ligi ya SWPL, zimenogesha na kuibua ushindani.

“Ni kweli tumechukua ubingwa lakini Simba Queens na Yanga Princess zimetupa ushindani wa hali ya juu, hilo linatufanya tujipangwe kwa mwakani kuona tutakuwa na changamoto zaidi,” alisema.

Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema msimu huu walikuwa na malengo yao matatu, akiyataja ni kumaliza nafasi tatu za juu, kubadili tabia za wachezaji na mpira wa ufundi na yote yametimia.

“Unajua wachezaji wa kike walikuwa wanasemwa vibaya juu ya mavazi yao, hilo kwa Simba tumeliondoa, pia hawakuwa na mpira wa ufundi kwa sasa wapo vizuri, tageti yetu ilikuwa ni ubingwa tukishindwa tumalize nafasi ya pili ama ya tatu, tunasubiri mechi yetu na Marsh ndio itaamua tunamaliza ya ngapi.

“Changamoto ilikuwa ni waamuzi TFF waliangalie hilo kwa manufaa ya kukuza soka la wanawake kwa msimu ujao, lakini pia kutafutwe kucheza mechi za kimataifa kwa bingwa sio wanamaliza msimu ndio inakuwa basi,” alisema.

Kocha wa Panama ya Iringa, Miraji Fundi, alisema wanataka kumaliza msimu kwa kutibua rekodi ya JKT Queens ambao hawajafungwa mchezo hata mmoja kwa 21 ambayo wamevuna pointi 63.

“Tunawaheshimu JKT Queens kwa kuwa tayari wamekuwa mabingwa kwa pointi ambazo wanamiliki hakuna timu ambayo inaweza kufikia kwani tumebakiza mechi moja na Jumapili ndio ligi inamalizika, lakini tutawatibulia rekodi yao,” alisema.