NINAVYOJUA : Hakuna aibu Ruvu Shooting kuiheshimu Simba

Thursday November 1 2018Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu kanakamfumujoseph@yahoo.com

MOJA ya kauli za kishabiki ambazo huongelewa na makocha wanapohojiwa na Waandishi wa Habari ni ile inayosemwa kuwa tunacheza na wapinzani wenzetu ambao wana miguu miwili kama sisi wenzetu wapo kumi na moja kama sisi na misemo mingine mingi ambayo haifuati misingi ya ufundi wa mpira wa miguu.

Kauli kama hizi ndizo huchukuliwa na makocha wa kitanzania na kuingia nayo kichwani dhidi ya timu zilizo bora kuwazidi na matokeo yake ni udhalilishaji ndani ya uwanja.

Haya ndiyo yamekuwa yakiitokea Ruvu Shooting kwa muda mrefu kila wanapocheza dhidi ya Simba, unaweza kuhesabu toka msimu wa 2013 hadi Leo Ruvu shooting imekutana na Simba si chini ya mara tisa hakuna ushindi hata mmoja zaidi ya sare iliyotengenezwa na aliyewahi kuwa kocha Mkuu, Charles Bonifas Mkwasa, kinachoendelea ni vipigo vya mbwa mwizi tena mara nyingi bila hata moja kupata bao.

Pamoja na kufungwa kila wakutanapo na Simba hata Yanga huwezi sikia lolote lile la kiufundi au kuliona limerekebishwa kwenye michezo inayofuatia, hali hii huwa inachosha na kukinaisha kuufuatilia mpambano mwingine unapozikutanisha timu hizi.

Bahati mbaya zaidi imekuwa ikimuangukia kocha wa sasa, Abdul Mutik Haji ambaye amekumbana na vipigo vya aibu ambapo kwa ujumla wake kesha fungwa goli si chini ya kumi na tano na Simba hao hao ambao wamekuwa si wageni kwake wala kwa wachezaji wake.

Huwezi kuona tofauti ya uchezaji wa timu yake jinsi iivyocheza msimu uliopita kwenye mchezo wa kipigo cha goli saba na huu wa juzi wa kipigo cha goli tano unaona kinachokosekana ni heshima tu mbele ya Simba.

Ndiyo, kwa nini usikubali tu kuwa Simba ina kikosi kizuri zaidi yangu, kwa nini kocha, Mutik anashindwa kuwa mkweli kwa kuongea bali kwa vitendo ndani ya uwanja, anaona aibu nini kukubali kuwa Simba ikicheza dhidi yao inajiamini kuliko kawaida, anashindwaje kukubali kuwa Simba kwa sasa ni bora ukilinganisha na timu nyingi nchini.

Unaiona picha hii ya kutokubali ubora wa mpinzani wake Simba toka timu inapoandaliwa, sidhani kama kocha, Abdul Mutik huwa anawaweka darasani wachezaji wake kuisoma Simba sidhani kama Kocha mwenyewe huwa anajifungia chumbani na kuchukua mikanda ya Simba ili kuwasoma kabla ya kukutana nao.

Unaiona mbinu ya Mwalimu, Abdul ikiwa haibadiliki, ni ile ile timu inafanya makosa kila mara tena yale yale yaani wala haibadiliki.

Timu inacheza mchezo wa wazi mno mbele ya timu bora kama Simba, kocha halioni hili, wachezaji wake wamecheza na Simba vikosi vikiwa havibadiliki sana hasa aina ya uchezaji ndani ya uwanja, lakini kwa Kocha Abdul huwezi kuiona mbinu mpya zaidi ya kukimbia kimbia kwingi kwa wachezaji wake bila mpangilio.

Nje ya uwanja unamuona msemaji wa klabu, Masau Bwire akiendelea kuleta sanaa kwenye mechi kubwa kama hiyo bado anaufanya mchezo huo kuwa kama maigizo hataki kuufanya mpambano huo kuwa muhimu anaamini kwenye kuongea ndiko kunakoweza kuwavuta watazamaji kuliko matokeo.

Anasahau kuwa jinsi timu inavyofungwa hivyo kila mara na Simba ndivyo ushindani unavyopotea ndivyo watazamaji wanavyopungua uwanjani, nani anapenda kuona ushindani mdogo ndani ya uwanja? nani anayependa kwenda uwanjani huku matokeo ya ushindi kwa Simba yako wazi?

Kuongea kwa Masau si kwamba kuna leta hamasa, badala yake kunaonyesha uongozi wa timu bado hauko sawa na mchezo unaowakabili, anawafanya wachezaji waendelee kudhani wapo sawa kiuwezo dhidi ya Simba na kuingia bila nidhamu ya mchezo.

Imefika wakati timu aina ya Ruvu Shooting kurudisha nidhamu ya ushindani ndani ya ligi.

Hata hivyo Ruvu Shooting inahitaji kubadili timu kuangalia kizazi kipya cha wachezaji wataokuja kuifanya tishio uwanjani kuliko jinsi inavyojulikana kwa mashabiki nchini, wanamjua zaidi msemaji wao kuliko wachezaji, hawaiheshimu timu bali wanaidharau.

Mafanikio ya timu yanaanza nje ikiwa pamoja na kujua uwezo na mapungufu ya wapinzani wake ili iwe njia ya kujiimalisha zaidi na mwisho inajipanga na kuonyesha ushindani wa Ligi Kuu na sio ushiriki.

Mbwembwe katika soka ni jambo jema kama linalofanywe na Bwire lakini isizidi uhalisia wa mambo yaliyopo kwenye timu kwani itakuwa faida kwao na mashabiki wao.

Advertisement