JAMVI LA KISPOTI : Ghafla Kichuya, Ajibu wanakuwa maswahiba walioshibana

Thursday March 19 2020

Ghafla Kichuya, Ajibu wanakuwa maswahiba walioshibana,sIMBA sc,mashabiki wa SImba,Kicchuya atupiwa virago Simba,

 

By Khatimu Naheka

UNAMKUMBUKA yule kijana mmoja mfupi pale Simba anayejua kutumia mguu wa kushoto aliyekuwa anaipiga Yanga mabao ya maudhi kwa kona na krosi kali akitokea kule Morogoro?

Achana na huyo hapa Tanzania kuna fundi mmoja anayejua kuuchezea mpira na akakupiga chenga za maudhi na hata kufunga mabao ya ‘kideoni’ alikuwa nahodha pale Yanga kabla ya kurejea klabu iliyomlea?

Hapa utakuwa ushanielewa nawalenga winga Shiza Kichuya aliyekuwa hashikiki alipokuwa Simba kabla ya kwenda Misri kucheza soka la kulipwa ambaye baada ya maisha kumuwia magumu kule akarejea nyumbani kwake pale Msimbazi.

Hakurejea peke yake akaungana na mtu mmoja Ibrahim Ajibu ambaye baada ya kujiingizia fedha na kulipaisdha jina lake pale Yanga ambako walimpa heshima ya mpaka kuwa nahodha wao sasa alirejea naye klabuni kwake Simba alikolelewa na kutambulishwa katika ulimwengu wa Simba.

Ukitaka kujifunza mambo mawili juu ya ubora wa kutanguliza utulivu katika kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako lakini hata maana halisi ya jinsi ya kujituma na kuweka juhudi basi angalia maisha ya wawili hawa pale Simba.

Wakati Kichuya anarejea Simba akiungana na Ajibu hakuna ambaye alitegemea haya yangeendelea kwamba wangepotea na kuonekana wachezaji wa kawaida.

Advertisement

Hebu fikiria unapigwa mchezo mkali kati ya Simba na Yanga mechi ambayo Kichuya ilikuwa inampatia umaarufu alafu unakuta jina lake halipo hata katika wachezaji 18 ambao walitakiwa kucheza mechi hiyo.

Achana na Kichuya, Simba inacheza na timu dhaifu msimu huu kama Singida inashinda mabao 8-0 alafu katika majina ya wachezaji 18 hakuna fundi Ajibu katika mchezo lakini habari mbaya zaidi ni kwamba hakuna taarifa zozote za wawili hao kuwa majeruhi.

Kuna msemo unasema wazungu hawajawahi kuwa wanafiki kama wapo, basi watakuwa wachache sana kuna elimu kubwa ambayo benchi la Simba chini ya Sven Ludwig Vandenbroeck kwamba hakuna ratiba ya mchezaji kupewa nafasi kutokana na historia yake ya nyuma.

Sio taarifa nzuri kusikia mchezaji kama Kichuya akipotea kwa mazingira kama haya akishindwa kuthibitisha ubora wake, shida kubwa ambayo wanayo wachezaji wetu wanakosa nidhamu nzuri ya kujituma katika kufikia malengo yao.

Wachezaji wengi wanapenda kuishi kwa mazoea wakiwa wepesi wa kukubali matokeo katika kuwania nafasi katika timu zao hawataki kujituma.

Kichuya kurejea Simba lazima atambue nafasi aliyoacha tayari ina mtu na ndio soka lilivyo anachotakiwa sasa ni kuwa na gia mpya katika kutafuta nafasi katika kikosi hicho hatua mbaya zaidi ni kwamba hata makocha waliopo sasa sio wale ambao walikuwa wakati anafanya kazi hapo.

Hatua ya kukumbukwa ni kwamba wachezaji hawa wawili hata hapo kabla ya kurejea Simba kulikuwa na maneno mengi kutoka kwa makocha juu ya mapungufu yao kimbinu wakiwa uwanjani lakini sasa ni wakati wao kujifunza na kujitathimini katika kujijengea ubora zaidi.

Ukiangalia safu ya ushambuliaji ya Simba haupati wasiwasi katika kupata majibu ya kwanini Kichuya na Ajibu wako nje mbele ya Luis Micquissone, Meddie Kagere, Hassan Dilunga, Francis Kahata na hata Clatous Chama.

Kitu cha kukumbukwa hapa ni kwamba katika wachezaji hao wote ni Micquissone na Kahata pekee ambao waliongezeka msimu huu na kila mmoja alikuwa na nafasi sawa katika kumshawishi kocha kupitia ubora wao kuanzia kwenye mazoezi mpaka katika mechi.

Ni wakati wa Ajibu na Kichuya kujipanga upya kwa kujua wapi wameteleza kisha kurudi kwa nguvu katika kuwania nafasi ambazo zitawafufua kutoka huko shimoni walipo sasa bado Simba inahitaji huduma zao.

Simba inahitaji kuona wanazidisha juhudi katika kuwania nafasi hatimaye ubora wa timu yao utazidi kuongezeka na kurudi katika ubora wao ule unaofahamika.

Advertisement