MTAA WA KATI : Emery alivyoweka sukari vita ya kusaka Top Four

Tuesday March 12 2019

 

By Said Pendeza

UKISIKIA ile risasi moja tu chali ndio hii. Wikiendi ni tamu kwa Arsenal. Ushindi mmoja tu dhidi ya Manchester United umewarudisha kwenye Top Four.

Bahati yao sana Manchester United. Pengine kwa sasa wangekuwa wakiishi wiki hii kwenye nafasi ya sita huko kama Chelsea angepeta matokeo ya ushindi kwa Wolves.

Walau The Blues imewaacha Man United kuishi hapo kwenye namba tano wiki hii, pointi mbili nyuma ya Arsenal, mabosi wapya kwenye ile Top Four kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, huku mechi zikiwa zimebaki nane tu kufika ukingoni.

Chelsea wao bado wana mechi tisa, wakishinda kiporo chao dhidi ya Brighton, basi hapo, Man United itakuwa imeporomoshwa hadi kwenye nafasi ya sita huko kama kila mtu atashinda mechi zake.

Lakini, kitu kinachovutia ni kwamba Man United na Chelsea kuna mechi ya wenyewe kwa wenyewe. Man United itaanza kucheza na Man City kwanza kabla ya siku nne baadaye kuwakabili Chelsea.

Bahati nzuri kwao mechi hizo zote zinafanyika Old Trafford. Vita ya Top Four imekuwa tamu. Lakini, Arsenal itakuwa inashusha pumzi, maana mechi zile zinazoonekana kuwa ngumu wameshazimaliza.

Arsenal haina mechi dhidi ya timu yoyote ndani ya Top Six kwa sasa, imeshamalizana nazo zote. Ina mechi za ugenini kwa Wolves, Everton, Watford, Leicester City na Burnley.

Kama itapata matokeo huko, basi tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao itakuwa inaihusu. Shughuli inayo Man United, ukiziweka kando Chelsea na Man City, ina mechi pia dhidi ya West Ham, Everton na Wolves, timu ngumu kabisa.

Kichapo cha Emirates kinafichua matatizo mengi kwa Man United.

Chelsea nayo inahitaji kupambana sana kuingia kwenye Top Four.

Inakabiliwa na mechi nyingi ngumu. Kwenye mechi zake ukiweka kando ya kuwakabili washindani wao kwenye nafasi hiyo Man United, watakuwa na mchezo wa ugenini kwa Liverpool huko Anfield.

Hii mechi imekuja kipindi kibaya kwa Chelsea kwa sababu kwa wakati huu Liverpool akili yao yote ipo kwenye kushinda na kubeba ubingwa. Matumaini ya Man United yapo kwa Tottenham Hotspur.

Mwendo wao kwenye ligi si mzuri sana na ukizingatia bado wana mechi dhidi ya Liverpool na Man United. Ole Gunnar Solskjaer na jeshi lake anaamini, Spurs haiwezi kutoboa kwenye mechi hizo na hivyo wao watatumia nafasi kupenya kwenye hiyo Top Four.

Hivi ndivyo Top Four ilivyo na ubingwa mkali na tamu zaidi kuliko hata mbio za kusaka ubingwa. Kwenye mechi ya Arsenal na Man United, Kocha Unai Emery alihitaji kushinda mchezo huo.

Hakwenda uwanjani kwa akili ya kujilinda. Tazama alivyoanza na washambuliaji wake wote matata, Pierre Aubameyang na Alexandre Lacazette na kumwaanzisha pia mpishi Mesut Ozil. Hawakuikabili mechi hiyo kuioga. Walihitaji kupata matokeo na pengine kurudisha hali ya kujiamini kabla ya kuwavaa Rennes Alhamisi hii. Ushindi umepatikana na sasa mpango wao upo kwenye kuwashusha Spurs.

Man United iliyocheza huko Emirates ilikuwa tofauti kabisa na ile iliyowakabili PSG katikati ya wiki iliyopita. Hawakuonekana kuhitaji kushinda kwa nguvu zote huku Romelu Lukaku akipoteza nafasi kadhaa za kufunga.

Lukaku alishindwa kufunga wakati ubao wa matokeo ukiwa 0-0. Kwenye soka, bao hilo lingekuwa na maana kubwa sana kwa Man United na pengine lingewatingisha Arsenal na kuwatia hofu zaidi hasa ukizingatia wanatoka kupoteza mechi yao iliyopita. Lukaku hakuishia hapo alikosa nafasi nyingine za kuipatia timu yake mabao kabla ya Aubameyang kuja kuimaliza mechi kwa mkwaju wake wa penalti.

Hivyo ndivyo Arsenal ilivyotumia mechi moja tu kubadili matokeo na sasa kuwaachia shughuli pevu Man United kwenye ndoto zao za kuikamatia Top Four.

Emery alitulia na hakika anastahili pongezi kwenye hili. Hakuwaogopa Man United kwa rekodi yao ya siku za karibuni, akacheza kwenye mipango yake na jambo zuri wameingia kwenye mfumo wake, akawatandika.

Advertisement