Emery, Mourinho wasingekuwa na meno Simba

Muktasari:

Hapa kwetu Tanzania ilikuwa ni saa 4 usiku, wakati wenyeji Mashetani Wekundu chini ya Jose Mourinho walipoikaribisha Leicester City kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 74,000.

IJUMAA ya Agosti 10, 2018 pazia la Ligi Kuu ya England, lilifunguliwa pale kwenye Old Trafford, mjini Manchester.

Hapa kwetu Tanzania ilikuwa ni saa 4 usiku, wakati wenyeji Mashetani Wekundu chini ya Jose Mourinho walipoikaribisha Leicester City kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 74,000.

Mashabiki wa Man United walikuwa hawajui kipi kitaitokea timu yao, kwani kabla ya kuanza kwa msimu Kocha Mourinho alikuwa akiwalalamikia mabosi wao juu ya kutopewa fungu la kufanya usajili wa maana kuimarisha kikosi chake.

Pia alikuwa na mzozo na baadhi ya nyota wake, kiasi cha kuaminika huenda timu isingepata matokeo mazuri mbele ya Leicester.

Bahati nzuri bao la penalti la Paul Pobga la dakika ya 3 na jingine la beki Luke Shaw dakika ya 83 yaliipa timu hiyo ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya ufunguzi.

Mechi iliyofuata Man United ilienda ugenini kuumana na Brighton & Hove Albion, Vijana wa Mourinho wakapigwa 3-2, kisha ikarudi tena Old Trafford kujiuliza kwa kuikaribisha Tottenham Hotspur katika mechi yao ya tatu ya ligi hiyo.

Spurs ikamharibia Mourinho kwa kuwakandika mabao 3-0, lakini hakuna hata kopo lililorushwa kwa Kocha huyo, zaidi ya kebehi ambazo katika maisha ya soka ni kawaida, hasa kama mashabiki hawakukubali.

Mrithi wa Arsene Wenger pale Emirates, Unai Emery alianza kazi Arsenal kwa mguu mbaya, timu ilipoteza mechi mbili mfululizo za awali za msimu huu dhidi ya Manchester City na Chelsea.

Hata hivyo Mhispania huyo hakutupiwa japo ganda la yai achilia mbali chupa za maji kama tulivyoshuhudia katikati ya wiki hii pale CCM Kirumba, Mwanza.

Mashabiki wa Arsenal walitambua soka ndivyo lilivyo, lina matokeo matatu ya kushinda, kufungwa na kutoka sare kwani baada ya mechi hizo, Ze Gunnerz haijapoteza tena katika mechi za ligi hiyo na hata zile za kimataifa.

Juzi tu imetoka kuisambaratisha Vorskla Poltava ya Ukraine katika Europa Ligi, lakini siku moja kabla ya Arsenal haijapata ushindi wa 4-2 kwa Poltava, pale Kirumba, watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba ilikufa mbele ya Mbao FC.

Simba ilipoteza mchezo wake wa kwanza katika Ligi Kuu Bara kwa bao 1-0 na katika aina ya kustaajabisha, mashabiki waliojitoa fahamu na ambao huenda wameanza kuipenda Simba juzi tu, walimrushia chupa Kocha Patrick Aussems.

Mashabiki hao ambao hawajui hata gharama ya mshahara wa mchezaji mmoja ama kocha ndani ya klabu hiyo wanajifanya wana hasira kwa timu yao kufungwa.

Kasumba ya kuamini timu yao ni bora na isiyofungika ikichagizwa na ushamba wa kulipenda soka ukubwani waliamua kufanya uhuni ule usiokubalika ambao unajiuliza hivi Aussems angekuwa ndiye Unai halafu akainoa Simba si hata tindikali angemwagiwa? Mechi moja tu Aussems kapigwa chupa, vipi zikiwa tatu!

Hatuwezi kwenda kwa ushabiki huu wa kishamba wa kutaka kuona baadhi ya timu tu ndizo zinapata matokeo mazuri na wengine ni kosa la jinai. Mbao wamekuwa wakiifunga Yanga wakatavyo CCM Kirumba, lakini mbona hakuna shabiki wa Jangwani aliyewahi kuwatusi wachezaji ama makocha wa timu hiyo?

Pia timu zote zilizopo katika Ligi Kuu zina haki ya kupata matokeo matatu yanayojiri katika soka yaani ama ifungwe, ishinde au kulazimishwa sare.

Mbeya City ilifungwa mechi tatu mfululizo ikiwamo na Simba, mbona mashabiki hawakumtukana Kocha Ramadhani Nswazurimo? Mechi zao mbili zilizopita zote imeshinda na kuondoka mkiani ilpokuwa mwanzoni. Ndivyo soka lilivyo.

Halafu mashabiki wanamshambulia kocha Aussems kwa sababu gani? Kwanini isiwe wachezaji wanaocheza uwanjani kama kweli mashabiki walichukizwa na matokeo ya Mbao? Lakini ni timu gani isiyotaka kufungwa ama kupata sare?

Ligi ya hivyo hakuna na hata Arsenal ilivyofanikiwa kuweka rekodi England 2003-2004, ama Simba na Azam zilivyofanya hapa nyumbani kwa msimu tofauti, ilitokea tu kama bahati, ila huwa haidumu milele jambo hilo! Mashabiki wabadilike sasa!