STRAIKA WA MWANASPOTI : Debi la ‘Mashemeji’ limepoteza mvuto kabisa

Wednesday November 13 2019

Debi-‘Mashemeji’- limepoteza -mvuto -Orlando -Pirates - Kaiser -Chiefs -African -UWANJA-NELSON-MANDELA-MWANASPOTISOKA-MWANASPOTIgAZETI-

 

By Boniface Ambani

DUNIA hii kuna Derby zikipigwa kila kitu kinasimama. Ni vile tu serikali za nchi zinashindwa kuifanya siku hiyo rasmi, la sivyo ingekuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa kuipisha debi hiyo.

Achana na derby za Manchester United na Manchester City, Barcelona na Real Madrid na ile ya Boca Junior na River Plate kule Argentina na ile ya hapo Bondeni ya Kaizer Chief na Orlando Pirates, Tanzania kuna bonge moja la debi ambalo huisimamisha nchi nzima.

Debi hiyo huanza mapema tu wiki moja ama mbili kabla ya mchezo wenyewe na hapo nchi nzima huwa gumzo na walio mikoani hupanga ratiba zao kuhakikisha wanahudhuria Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili kushuhudia.

Vyombo vya habari, vitapiga hizo timu msasa kwelikweli. Mabango utayaona kila sehemu. Magari na hasa daladala (matatu) zote zitabandika bendera za klabu hizo. Hii yote ni ishara ya miamba miwili ya nchi hiyo inakutana, tambo kila kona na mwishowe siku ya mchezo ndio mbabe anajulikana huku shughuli zikisimama kupisha shughuli hiyo nzito kwenye uwanja wa Taifa unaoingiza idadi kubwa ya mashabiki takribani 60,000 ambao pia huvalia jezi za klabu zao na kuongeza utamu wa debi hiyo.

Ongezea debi dhidi ya Orlando Pirates na Kaiser Chiefs African kusini. Mambo huwa yaleyale katika Uwanja wa Nelson Mandela Stadium.

Mbona nimeanza makala yangu na hizo klabu? Kumekuwa na shida kubwa sana Kenya wakati mahasidi wa tangu jadi AFC Leopards na Gor Mahia zinapokutana. Kwa miaka ya karibuni mechi yao imekuwa ya kawaida sana.

Advertisement

Juzi Jumapili wababe hao walikipiga kwenye Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani. Ni mechi ambayo haikupigwa msasa pahali popote. Imekuwa ni mechi ya kawaida tu. Haileti shangwe.

Shida kubwa imekuwa ni kwa upande wa AFC Leopards na mara kwa mara wamekuwa wakipigwa na Gor Mahia. Hii ni moja ya mambo yanayoifanya debi yao ipoteze ila ladha yake na hata mashabiki wengi wa Ingwe (AFC Leopards) wameamua kutohudhuria hizo mechi kwani ni aibu kila wakati kupigwa na Gor Mahia.

Takriban misimu minne sasa Leopards haijapata ushindi wowote na juzi ilichapwa mabao 4-1. Ni wazi debi inahitaji ukomavu na kuoinyesha wazi mpinzani wako hakuwezi na hata akikuweza ni kwa bahati sana na si kukuonea kila mara.

Kufungwa zaidi ya mabao mawili kwenye debi ni aibu sana. Ni kuwakosea mashabiki heshima yao na ndio maana imefikia sasa wanashindwa kwenda uwanjani. Tatizo kubwa ambalo nimekuwa nikilisema kwa Leopards ni ishu ya usajili. Wengi waliosajiliwa ni wa kawaida sana. Ni wa mechi za kutoa sare na Western Stima na Kariobangi Sharks na kujisifu lakini sio wa mechi kubwa kama ya debi.

Ni lazima Leopards ifanye juhudi kubwa kuhakikisha inasajili wachezaji wa kuwapa mataji na ama kumaliza ndani ya tatu bora KPL na si wale wa kubahatisha ushindi. Kufungwa kila mara kumechosha mashabiki na wengi wameamua kujitenga na klabu hiyo. Yote hayo nitasema wazi bila kuficha, tatizo kubwa ni ni usajili wa wachezaji.

Mambo ya kusajili wachezaji kiushemeji shemeji yafaa yaishe kabisa. Haifai hata kidogo. Lazima tuheshimu na tuilinde nembo ya klabu hiyo. Nembo Leopards hajatendewa haki kwa muda mrefu. Mara ya mwisho klabu hiyo kushinda taji ilikuwa mwaka wa 1998. Takriban miaka 20 iliyopita.

Wapinzani wao Gor Mahia ndani ya misumu sita iliyopita wameshinda mataji zaidi ya manne. Wamekuwa wakiiwakilisha nchi kila kukicha. Mashabiki wanaumia. Nembo inaumia. Yote tisa wachezaji pia lazima waambiwe ukweli na wajue wakati unapovaa hiyo jezi, ina uzito wake.

Hadhi ya klabu lazima irudishwe. Hakuna kubembelezana na watu katika soka. Ni uongozi ufanye Jambo. Lazima jopo la kusajili wachezaji liundwe. Jopo hilo ndilo litakalo pewa majukumu ya kuunda klabu hiyo, pia kushirikiana na uongozi kuunda benchi la ufundi.

Advertisement