Chilunda umri sahihi, wakati sahihi, nchi sahihi

Tuesday July 10 2018

 MCL

SHABAN Idd Chilunda alimlipa Cristiano Ronaldo bao lake la sarakasi siku chache tu baada ya Ronaldo kufunga bao lile jijini Turin.

Yeye, Shaban Idd alilipa katika mechi dhidi ya Yanga siku ya mwisho wakati ligi iliyoisha ilipokata roho.

Watoto wa siku hizi ni watundu, wakati mwingine wanaiga vizuri, Shaban Idd wa Azam FC ni mmojawao. Katika siku za karibuni anafunga sana. anajua kufunga. Anajua lango lilipo. Anafunga mabao ya madaha lakini kitu cha msingi ni kwamba anajua kufunga.

Imetangazwa na imethibitishwa kwamba anakwenda Klabu ya Tenerife ya Hispania. Wao wapo daraja la kwanza pale Hispania.

Kwanza imeshangaza kidogo. Tumezoea kuona wachezaji wetu wanaochipukia wakisubiri kuwa mastaa, kisha wachokwe pale Uwanja wa Taifa, ndipo wanaanza kusaka malisho mema.

Hii hadithi ya Shaban Idd imekuwa tofauti kidogo. Ana umri wa miaka 19. Ameanza kung’ara pale Azam ambapo wote tunafahamu kuwa ni timu ya kitajiri. Kama anaondoka basi ni kwa vile ana washauri wazuri sana. Siamini kama Azam imemuachia kirahisi kama ambavyo inaweza kujaribu kuiaminisha jamii.

Kuna wachezaji wengi ambao waliishi kwa kutamaniana zaidi na Azam. John Bocco ni mmojawapo. Salum Abubakar ni mwingine. Katika ubora wake, Bocco angeweza kucheza kokote nje ya nchi lakini hakuonekana kama ana hamu. Nilidhani Chilunda angeweza kuwa Bocco mwingine pale Azam.

Vyovyote ilivyo, Shaban amefanya maamuzi sahihi. Kwanza kabisa hajatumia nguvu nyingi katika soka letu. Ndio kwanza mbichi. Ina maana amehifadhi nguvu nyingi za mwili ambazo anaweza kwenda kuzitumia kupambana na Wazungu.

Vyovyote ilivyo, kama akidumu soka la Ulaya ambalo wakati mwingine haijalishi kama una kipaji au vinginevyo na linahitaji nidhamu zaidi, basi kuna uwezekano mkubwa wa Shaban Idd kutamba kwa muda mrefu kwa sababu ataingia katika mfumo akiwa bado mdogo. Yeye anaingia na umri wa miaka 19 wakati Mbwana Samatta ameingia akiwa na umri wa miaka 24.

Lakini kitu kikubwa zaidi kuliko vyote ni kwamba Shaban Idd ni rahisi sana kuwatamanisha Wazungu watakaomtazama kuliko wachezaji wa aina nyingine.

Washambuliaji wanauzika kwa urahisi kwa sababu wanapata umaarufu kwa urahisi kutokana na kufunga mabao.

Kama Mbwana Samatta asingeumia kwa muda mrefu katika msimu ulioisha ingekuwa rahisi kwake kuuzika kwa sababu angekuwa na mabao mengi zaidi kuliko aliyomaliza nayo msimu. Shaban ataheshimika kwa mabao yake zaidi.

Ligi aliyokwenda pia itamnufaisha. Soka linalochezwa Hispania ni lile ambalo linatumia zaidi akili na wachezaji wanapata nafasi zaidi ya kuonyesha vipaji vyao.

Siamini kwa mchezaji wa Kitanzania kutoka nchini na kwenda katika soka la Kiingereza au staili ya soka la Kiingereza. Hispania ni sehemu sahihi.

Lakini pia hili ni fundisho halisi kwa wachezaji wengi vijana. Kwa mfano, wachezaji wanaotoka katika soka la vijana wangeandaliwa mazingira ya kukomaa nje zaidi katika mifumo ya kisasa muda mchache baada ya kutamba katika michuano ya vijana.

Leo tuna nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Ubelgiji, katika kikosi cha kinachoanza cha Wafaransa kuna mchezaji mmoja tu anayecheza ndani ya nchi hiyo ambaye mara nyingi anaanza. Kylian Mbappe.

Katika kikosi cha wapinzani wao Ubelgiji kuna mchezaji mmoja tu ambaye anacheza nyumbani. Ni beki, Leander Dendoncker.

Hii inamaanisha kwamba mpira umebadilika. Wakati sisi tukijivunia Samatta kama mchezaji anayecheza soka la kulipwa Ligi Kuu ya Ubelgiji lakini Wabelgiji wenyewe wanaona haifai kutumika kwa matumizi ya soka la kulipwa.

Hapa ndipo tunapogundua tunahitaji kina Shaban Idd wengi kwenda nje kwa maslahi ya timu yetu siku za usoni. Waingereza ndio wanatumia wachezaji wote kutoka ndani haishangazi kuona hata hivi wanavyofanikiwa mashabiki wanaona maajabu.

Lakini hapo hapo sio mbaya kujikumbusha ukubwa wa Ligi Kuu ya England.

Advertisement