Cheki namna Ngassa alivyochemka aisee

Friday June 22 2018

 

By THOMAS NG’ITU

LABDA ubishe tu lakini hapa nchini kuna Mrisho Ngassa mmoja tu. Huyu ni yule winga wa zamani wa Simba, Yanga na Azam aliyetikisa kwa kipaji kikubwa cha kusakata soka.

Ngassa aliyerithi kipaji cha soka kutoka kwenye ukoo wao ukiongozwa na baba yake mzazi, Khalfan Ngassa aliyewika ndani ya timu za Pamba, Simba na Taifa Stars. Alikuwa mtamu, acha tu!

Mchezaji huyu amejitengenezea jina kubwa ndani na nje ya nchi kwa soka lake tamu mguuni na kasi aliyokuwa nayo ya kuwatoka mabeki mbali na umahiri wake wa kutupia kambani.

Hata hivyo, licha ya uwezo wote, mchezaji  huyu ameendelea kusalia katika Ligi Kuu Bara, japo alishatoka kwenda nje kucheza soka la kulipwa na kuchemka kabla ya kurejea nyumbani kuendelea kukipiga.

Hizi hapa ni sababu tano ambazo Mwanaspoti linaamini zimechangia kwa kiasi kikubwa kumkosesha nyota huyo kufika kule waliko wenzake, yaani akina Mbwana Samatta na wengine.

UYANGA WA WAZI

Ni kweli kila mtu ana utashi na uhuru wa kufanya lolote maadamu havunji sheria ya nchi, lakini kwa mchezaji wa soka ni kujitia tabu kuonyesha mapenzi ya wazi kwa klabu, hasa kwa soka la Kibongo.

Kwa kuwa soka ni ajira kwa sasa, inapendeza mchezaji kutumia kipaji chake kucheza kokote bila kuonyesha ule unazi wa kishabiki uliopitiliza kwani inamnyima fursa kuaminiwa kwingine.

Bahati mbaya, Ngassa ni kama alijisahau na kuonyesha mapenzi yake ya dhahiri kwa Yanga kiasi cha kumweka katika wakati mgumu kwa mabosi wake wa zamani Azam FC.

Kitendo cha Ngassa kuvishwa jezi ya Yanga kisha kuibusu huku akiwa mchezaji wa Azam, kiliwakera mabosi wake wa Chamazi na kusababisha mtafaruku ulioishia kupelekwa Simba kwa mkopo.

Azam waliamua kumpelekea kule kama njia ya kumkomoa baada ya kuonekana wazi akili yake ilikuwa Jangwani. Hili mpaka leo limekuwa ni doa kwa Ngassa kama mchezaji wa kisasa.

KULIKACHA DILI LA EL MERREIKH

Winga teleza huyu aliyewahi kujaribiwa West Ham United ya England chini ya Kocha Gianfranco Zola, alionyesha utoto mno miaka michache iliyopita alipolikacha dili ya Wasudani.

Wasudan wa El Merreikh walimtaka Ngassa, lakini winga huyo alikubali kufichwa hotelini na mabosi wa Yanga ili tu kulikwepa dili hilo kipindi na kujinyima fursa ya kuvuna mapesa ya matajiri hao.

Inawezekana ushauri kutoka kwa watu wake wa karibu ulifeli kwani kama angeenda Sudan, leo Ngassa asingekuwa mchezaji wa kucheza Ndanda ama kulilia kurudi Yanga.

Hili lilikuwa kosa ambalo anapaswa kulijutia hata kama yeye na washauri wake walilichukulia poa, kwani kwa sasa Ngassa anaonekana wa kawaida mno, wakati alikuwa awe mbali zaidi.

KUWACHOMOLEA WANORWAY

Klabu ya Lov Ham ya Norway ilikuwa tayari kulipa zaidi ya dola za Kimarekani 100, 000 kama ada ya uhamisho wa winga huyo, enzi akiichezea Yanga iliyokuwa chini ya Imani Madega.

Ngassa aliamua kuipotezea kimtindo na dili hilo likafa likimuacha winga huyo akiendelea kuwa wa hapahapa.

Hiyo ilikuwa safari nyingine kwake kutoka, lakini kutokana na mapenzi yake dhidi ya Yanga alijikuta akiendelea kukaa ndani ya klabu hiyo na kuachana na safari ya Norway.

Angesaini katika klabu hiyo, leo hii angekuwa akihangaika huko huko ulaya kwani tayari angekuwa ameshajitengenezea jina lake.

KUCHEMSHA FREE STATE STARS

Mwaka 2015 Ngassa alisajiliwa Free State Stars iliyopo Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL), lakini akajikuta akichemsha mwaka mmoja tu akavunja mkataba na kurejea nyumbani kujiunga na Mbeya City.

Wengi walishajua mchezaji huyo angetulia nchini Afrika Kusini kutokana na kasi na nguvu alizonazo, lakini uvumilivu na utayari ulikosekana katika akili yake na kuamua kuondoka.

Nafasi ya kucheza alikuwa akiipata ndani ya kikosi hicho, lakini majeraha ya mara kwa mara yalikuwa yakimkumba na kumfanya asicheze kwa muda mrefu.

KUTOKA OMAN HADI MBEYA CITY

Baada ya kutoka Free State aliamua kutimkia Oman katika klabu ya Fanja SC ambayo imekuwa kimbilio la nyota wengi kwani hata Danny Lyanga, Mbuyu Twite wote walikuwa wanakipiga huko.

Ilikuwa ni hatua kubwa kwake kwenda kucheza soka Umangani, lakini ghafla tu tulishtukia winga huyo akirudi nyumbani na kujiunga Mbeya na baadaye kutua Ndanda aliyoichezea msimu uliopita.

Tangu aliporudi nyumbani kwa mara nyingine na kuzichezea Mbeya City na Ndanda mzani wake ukaanza kushuka kabla ya hivi sasa kudaiwa yupo mbioni kurejea klabu aipendayo ya Yanga.

Advertisement