Brazil wausahau kabisa ufalme wa soka

Tuesday July 10 2018Olle Bergdahl Mjengwa

Olle Bergdahl Mjengwa 

MSOMAJI, Brazil walikuja Russia na lengo moja, kurudisha heshima yao. Tangu Brazil walipofungwa mabao 7-1 na Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, timu hiyo imejua kuna njia moja tu kurudisha heshima ya nchi yao. Ni kushinda Kombe la Dunia.

Brazil kuna msemo mmoja maarufu, ‘Gonhar ou perder a copa de mundo” -kushinda au kulipoteza Kombe la Dunia.

Kwa Wabrazil kufika fainali bila kunyakua kombe si mafanikio na ni sawa na kulipoteza Kombe la Dunia na hakika kutolewa katika robo fainali ni aibu kubwa kwa Wabrazili.

Sawa Ubelgiji ni timu yenye kiwango kikubwa lakini kwa Wabrazil nchi yao ni nchi bora zaidi duniani kimpira katika historia na walitegemea kabisa Brazil ingekuwa na uwezo wa kuifunga timu yoyote katika michuano hii ya Kombe la Dunia.

Tangu Brazil walipopoteza Kombe la Dunia katika uwanja wao wa nyumbani mwaka 2014, mashabiki wengi wa nchini humo wameacha kufuatilia na kuishabikia timu yao ya taifa kama zamani.

Katika baadhi ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Chama cha Soka Brazil kilipata tabu sana kuuza tiketi za mechi za nyumbani kitu ambacho miaka 10 iliyopita haingewezekana.

Ujerumani walipowafunga Brazil mabao hayo saba, si tu waliwavunja moyo mashabiki waliokuwepo uwanjani, bali mashabiki nchi nzima ambao walikuwa wakifuatilia michuano hiyo na kwa uhakika wakiamini timu yao itafanya makubwa kwenye ardhi yao ya nyumbani.

Ni wazi Brazil bado haijapona kutoka kipigo hicho na hii inaweza ikawachukua muda sana hadi kuweza kurudisha heshima yao kwenye michuano hii mikubwa.

Ushindi katika Kombe la Dunia huko Russia ungeweza kurudisha amani na upendo wa washabiki wa Brazil katika timu yao ya taifa.

Pia uchumi wa Brazil katika miaka ya hivi karibuni umekwenda vibaya na wabrazili wengi sasa wanaishi katika mazingira magumu.

Soka ni zaidi ya mchezo na wabrazil wengi walikuwa na matumaini ushindi katika Kombe la Dunia ungewapa furaha na nguvu mpya katika wakati huu mgumu ambao nchi yao inapitia.

Hata hivyo, hata baada ya michuano hii ya Kombe la Dunia, Brazil itabaki kuwa nchi pekee duniani ambayo imeshinda Kombe la Dunia mara nyingi zaidi, mara tano.

Kwa mtazamo wangu kwa sasa, Brazil si wafalme tena wa soka.Miaka ya nyuma Brazil ilipata mafanikio ambayo ni kama yalikuja kugota mara ya mwisho wakiwa na kikosi cha dhahabu kikiwajumuisha mastaa kama Ronaldode Lima, Ronaldinho Gaucho, Rivaldo, Roberto Carlos, Kaka na wenguine.

Kikosi hiki ambacho kilifanya makubwa mwaka 2002 kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Korea Kusini na Japan, ni wazi hakitakaa kijirudie na kama kitarudi ni miaka mingi ijayo, sio kwa wachezaji wa sasa wa Kibrazil wakiongozwa na bishoo wao Neymar. Kizazi cha kina Ronaldo walikuwa wanajielewa na walikuwa wanaangalia zaidi taifa lao kuliko pesa.

Brazil kwa sasa inategemea wachezaji wawili watatu. Si sawa na awali, timu nzima kuanzia goli kipa hadi washambuliaji walikuwa wanajituma.

Kama unakumbuka kikosi cha mwaka 1994 kilichochukua ubingwa wa dunia na kisha baadaye mwaka mwaka 1998 kikifika fainali na kufungwa na Ufaransa, baadhi yao walikuwepo kuanzia 1994 na baada ya kuona 1998 wameanguka kidogo, mwaka 2002 walikirejesha kikosi chao katika makali na kuweza kurudisha heshima yao.

Kwa sasa sidhani kama hilo linawezekana, Brazil mwaka 2006 ilikuwa ndio mwisho wa zama, iliishia hatua ya robo fainali kama ilivyokuwa mwaka 2010 ikiishia hatua hiyo hiyo.

Baada ya hapo, mwaka 2014 kidogo tukaona ikicheza soka tukiamini inarudi lakini kwenye fainali hizo za nchini kwao, iliishika nafasi ya nne wakifungwa na Uholanzi kwenye kuwania nafasi ya tatu.

Ni wazi Brazil inazidi kupotea zaidi, ule ufalme ulioanzia kwa Mfalme wa soka duniani, Pele ameishia kizazi cha kina Ronaldo. Mvuto wa Brazil unakwisha, watu wengi duniani walikuwa wanaishabikia Brazil hata wasiojua inatokea bara gani, kila mtu alijivunia kuishabikia Brazil kwa uhakika kila fainali itachukua ubingwa.

Hata hivyo, kwa sasa wengi wameikimbia, hata wale ninaowajua walikuwa kifua mbele kujivunia Brazil nawaona wamehamia England, Ubelgiji, Ufaransa na wengine Argentina na Ureno.

Brazil imeshajichokea zake, hawana tena burudani uwnjani.

Naamini tutapata fursa ya kuwaona Neymar, Philippe Coutinho, na Roberto Firmino katika fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2022 zitakazofanyika huko Qatar falme za Kiarabu, lakini enzi za Brazil kufika mbali katika kila Kombe la Dunia zimekwisha, labda tu kama kile kizazi cha kina Ronaldo kitarudi tena, lakini kwa Brazil hii ya mabishoo, tugawane tu timu nyingine tusife kwa presha.

Advertisement