TASWIRA YA MLANGABOY : Bonasi za kumtuza mwali mkoleni hazina tija Yanga

Muktasari:

Tuyaache hayo ya Chalenji, wiki hii Taswira inataka kuzungumzia utamaduni mpya wa Yanga wa kumtunza mwali mkoleni kila timu hiyo inaposhinda.

Mwaka unaondoka kwa kasi ya jet, soka la Tanzania ni mafanikio yake pamoja na vituko vyake ili mradi maisha yanakwenda.

Wiki hii mashindano ya Chalenji yananza kutimua vumbi nchini Uganda, Tanzania Bara ipo kundi C likiwa pamoja na Zanzibar, Kenya na Djibout. Tanzania haijachukua ubingwa katika ardhi ya Uganda kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita hivyo naamini safari hii wanakwenda kwa lengo la kuvunja mwiko huo kwa kurudi na ubingwa.

Tuyaache hayo ya Chalenji, wiki hii Taswira inataka kuzungumzia utamaduni mpya wa Yanga wa kumtunza mwali mkoleni kila timu hiyo inaposhinda.

Mkataba na GSM wa kwanza ni ule wa jezi ambao klabu unapata Sh1300 kwa kila jezi itakayouzwa na lengo ni kuhakikisha jezi milioni mmoja zinauzwa ili klabu ipate Bilioni Moja na milioni 300, pia mkataba unahusisha ukarabati wa Jengo la Yanga, Mkataba wa pili na GSM unahusisha magodoro ya GSM mkataba huu una thamani ya Sh150 milioni.

Yanga kupitia mdhamini wao GSM wamekuwa na utaratibu wa kutoa Sh10 milioni kila timu hiyo inaposhinda lengo likiwa ni kuwapa hamasa wachezaji wao.

Hakuna ubishi wachezaji kupewa bonasi ni jambo zuri linaloongeza morali kwa wachezaji hasa kwa timu yoyote yenye malengo ya kufika mbali.

Unajua katika maisha unaweza ukawa na jambo jema unalifanya, lakini kwa jinsi unavyoliwakilisha mbele ya watu linaweza kuleta picha yenye walakini. Katika dunia ya sasa ni jambo la kushangaza kuona mdhamini anakubali kutoa fedha nyingi kiasi cha Sh10 milioni zinapelekwa mikononi kienyeji kwa lengo la kupewa wachezaji.

Naamini wachezaji wote wa Yanga wanatumia akaunti zao za benki kama hiyo haitoshi basi wanaweza kutumia mitandao ya simu kupokea pesa hizo.

Najiuliza mtu unapotuonyesha fedha hizo hadharani lengo lake nini? Unamlingishia nani? Kwa faida ya nani? Mwishowe utabaini ni uswahili mwingi. Naamini fedha za aina hii zinatengeneza mazingira magumu ya kufanyia ukaguzi wa mahesabu, hasa kuona jinsi gani walengwa zimewafikia kwa uhakika au kuna watu wameanza kuzipunguza hapo kati.

Pia, fedha za kutolewa mikononi hivi ni ishara kwa uongozi wa Yanga hauamini na wadhamini kiasi cha kuamua wenyewe kuzipeleka na kuwakabidhi wachezaji ili kuondoa utata.

Kama hiyo haitoshi fedha za namna hii zinacha swali je ni sehemu ya udhamini au ni mtu ameamua kutoa mwenyewe kwa mapenzi yake.

Kama ni udhamini basi uongozi wa Yanga utakuwa na tatizo, lakini kama ni mtu anatoa tu kwa mapenzi yake pia kuna jambo ambao Fifa inalipiga ya matumizi ya fedha za nje ya mpira kuingizwa kienyeji katika soka kwa kuogopa kashfa za utakatishaji.

Naamini viongozi wa Yanga wanaweza kutafuta njia bora zaidi ya kutoka bonasi kwa wachezaji wao ambayo inawaongezea heshima wachezaji pamoja na kuwafanya wawajibike zaidi. Pamoja na kutolewa bonasi ya jumla pia viongozi wa Yanga watakiwa kuweka kipengele katika mikataba ya wachezaji nyota ya namna wanavyoweza kupata bonasi kila wanavyojituma.

Kwa mfano Arsenal inampa mshambuliaji wake Pierre-Emerick Aubameyang bonasi ya Pauni 300,000 akifanikiwa kufunga mabao 25 pamoja na kutoka pasi za mabao, pia anapata bonasi ya Pauni 50,000 kwa kila mechi atakayoanza na Arsenal ikashinda. Livepool wenyewe wanampa Virgil Van Dijk bonasi ya Pauni 20,000 kwa kila bao analofunga pamoja kila moja ambayo ukuta wake hatoruhusu bao.

Naamini hizi bonasi zikiandikwa kwenye mikabata ya wachezaji na zikatekelezwa kwa vitendo naamini wakina Kelvin Yondani, David Molinga watapambana zaidi uwanjani kuhakikisha wanatafuta bonasi za namna hii kuliko hizi.

Hofu yangu nyingine hizi bonasi zinazotolewa mkoleni hivi zinaweza kutumbaza na kusahau kwamba GMS wamehaidi kuifanyia Yanga mambo makubwa tena ya maana ukarabati wa jengo la makao makuu ya klabu.

Natamani kuona klabu kongwe kama Yanga ikiwa inafaidika na udhamini kwa kuhakikisha uwanja wa Kaunda unakamilika pamoja na jengo linakuwa katika hadhi yake.

Tunahitaji kuona hosteli ya wachezaji wa Yanga ikiwa katika kiwango cha kimataifa na wachezaji wakikaa hapo kama inavyosema katika mikataba ya udhamini.

Ni lazima klabu kubwa na kongwe zionyesha kwa vitendo kwa kuachana na sifa za kijinga za kutuonyesha sisi mashabiki kwamba timu ina fedha wakati wachezaji hawana uhakika wa mishahara yao.