NINAVYOJUA : Bila mpango mkakati, kocha akubali kulaumiwa tu

Thursday January 24 2019Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu

Mwishoni wa wiki iliyopita Jumamosi kulikuwa na michezo miwili tofauti ikizihusisha timu mbili kongwe na kubwa nchini Simba na Yanga.

Wakati Yanga wakipambana kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United huko Shinyanga, wenzao Simba walikuwa nchini Congo wakimenyana na As Vita kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Zote zilikuwa ugenini.

Hata hivyo, timu zote zilipoteza michezo yao Yanga wakifungwa bao 1-0, huku Simba wakifungwa mabao 5-0.

Hali zao kabla ya mechi hizo zilikuwa zinafanana. Ki vipi? Yanga ilikuwa haijawahi kufungwa kwenye Ligi Kuu huku ikifanikiwa kushinda michezo 17 na kuambulia sare moja, hivyo kupoteza mchezo huo kulizua kejeli kutoka kwa watani zao Simba.

Simba waliikejeli Yanga wakisahau usiku wa siku hiyo walikuwa na mchezo wao dhidi ya Vita na walikuwa na furaha ya ushindi wa mchezo wao wa kwanza dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Hivyo waliingia mjini Kinshansa wakiamini watapata matokeo ikizingatiwa Vita wlalitoka kufungwa ugenini na Al Ahly ya Misri.

Unaweza kuendelea na utani lakini kumbuka timu zote zilicheza michuano tofauti.

Kupoteza kwa Simba ni pigo kwa nchi nzima kwani inaliwakilisha Taifa, tofauti na Yanga ambayo ilicheza Shinyanga na kufungwa kwake kulitokana na kucheza michezo mingi bila kupoteza na hivyo, kila mtu alikuwa akiiangalia itafika wapi kabla ya rekodi yao kutibuliwa na Jacob Massawe wa Stand United.

Hizi ndio timu ambazo zimekuwa zikituwakilisha mara kwa mara kwenye michuano ya kimataifa. Zimekuwa zikipishana au zote zikishiriki kwa wakati mmoja. Hivyo, nimeona ni bora kuzijadili kwani ni kama kioo cha soka la nchi yetu.

Wakati Simba inakwenda Congo, bila shaka wengi walijua Kocha Patrick Aussems na benchi lake la ufundi walishaisoma Vita hasa ilipokuwa ikicheza na Al Ahly na bahati nzuri mechi yenyewe ilichezwa siku moja kabla kitu ambacho kingewasaidia sana kuwajua wenzao.

Hata hivyo, bado benchi la ufundi la lilikuwa na muda mrefu wa kuisoma Vita kupitia mikanda kadhaa ya michezo yake kuanzia ile michezo ya msimu uliopita ya Kombe la Shirikisho ya nusu fainali hadi fainali dhidi ya Raja Casablanca na hivyo mategemeo ya wengi tulijua benchi hilo limeshaisoma tofauti na ilivyokuja kufanyika.

Kwanza sikuamini kile alichokisema kabla Kocha Patrick Aussems wanakwenda Kinshansa kushambulia na siyo kujilinda, ni kama vile hawakuwasoma na kuwaelewa wachezaji na timu nzima ya Vita, ni dhahiri mpango mkakati wa timu dhidi ya Vita ‘Game Plan’ ulishindwa kabisa kabla ya mchezo husika, hiyo ni funzo kwa Simba na benchi lake kujipanga kwa mchezo wao unaofuata dhidi ya Al Ahly mwanzoni mwa mwezi ujao.

Hakuna ubishi nchi yetu imekosa kwa miaka ya karibuni wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, huko nyuma haikuwa rahisi kwa wachezaji pengine zaidi ya saba kuwaona wakipangwa kwenye kikosi cha kwanza.

Hii ni kwa sababu nchi ilijaa vipaji halisi vya wachezaji lakini tatizo lilikuwa ni namna gani vipaji hivyo viliweza kuendelezwa.

Kwa mana hiyo Kocha Patrick Aussems alitakiwa alijue hilo kuwa Simba haina wachezaji bora kulinganisha na timu pinzani hasa za Al Ahly na Vita Club hivyo alitakiwa awe na mpango mkakati bora kuhakikisha anacheza kwa heshima dhidi ya wapinzani wake kuanzia hawa aliocheza nao Vita Club hadi watakapo wakabili Al Ahly ya Misri.

Bado pia tunatakiwa sisi kama Watanzania wapenda soka kuondoa ushabiki zaidi badala yake ukweli utawale, hatutakiwi kudanganywa, soka ni mchezo wa wazi ikifika wakati tunauona ukweli, basi tuongee lugha moja.

Mfano ni jinsi wenzetu wanavyojua kuchagua aina ya uchezaji kulingana na aina ya michuano, nchi inakwenda kushiriki kwa kuchagua aina halisi ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa rasmi kushiriki michuano hii.

Unaiona wazi tofauti ya matumizi ya nguvu za wachezaji kwenye michuano hii na aina ya wachezaji wanaotakiwa, tuliona ukubwa wa miili ya wenzetu ukilinganisha na hawa wa kwetu bila shaka hii nayo inatakiwa iangaliwe na makocha hawa kwenye michezo yao ijayo kwa faida ya nchi na klabu husika.

Wakati Simba kupitia benchi lake la ufundi lilionekana kushindwa mchezo wake dhidi ya Vita Club, huku nchini watani na wapinzani wao Yanga walishindwa kuilinda rekodi yao ya kutofungwa na mwisho wake walipoteza mchezo kwa namna hiyo hiyo na mpango mkakati wa Kocha Mwinyi Zahera ulishindwa mapema kabla ya kucheza dhidi ya Stand United kwa kuwa haikuisoma vizuri.

Advertisement