Ben Pol ishu ya Ebitoke wala haikua kiki mjue

Thursday September 6 2018

 

By RHOBI CHACHA

HAKUNA anayebisha juu ya uwezo mkubwa alionao Ben Pol. Pia hakuna anayekataa kama jamaa ni mkali wa R&B kwa waimbaji wa kiume. Ngoma zake kadhaa kama Moyo Mashine, Sofia, Nikikupata na nyingine zimetengenezea ufalme katika miondoko hiyo.

Ben Po ambaye majina yake kamili ni Bernard Paul kwa sasa anatamba na ngoma yake mpya iitwayo Gusa, amebambwa na Mwanaspoti na kupiga naye stori mbili tatu ambapo amefunguka mambo kadhaa nje ya sanaa yake na muziki.

Mkali huyo aliyewahi kuhusishwa na mchekeshaji Ebitoke, ameweka bayana ishu yao nzima na kusisitiza hakuwahi kutoka naye, lakini pia haikuwa kiki kama wengi walivyodhani bali ilikuwa mpango maalum. Kivipi? Tiririka naye...!

Mwanaspoti: Habari yako?

Ben Pol: Nzuri, habari ya siku?

Mwanaspoti: Salama. Hivi bado tu hujafikiria kuoa kama ulivyowahi kuahidi?

Ben Pol: Haahaaa...Ebwana ee kiukweli bado nina safari ya kupambana na maisha ili nifanikishe malengo yangu ya kimaisha niliyojiwekea, ila nini ujue huwa natamani sana maisha ya ndoa pindi ninapohudhuria harusi za washkaji zangu.

Mwanaspoti: Hivi maisha yako ya kila siku yakoje, ukiachana ishu za muziki?

Ben Pol: Ni ya kawaida sana, yaani kama yalivyo ya watu wengine, hakuna tofauti kabisa, ndio maana nashindwa kuyatofautisha.

Mwanaspoti: Vipi maisha yako tangu umekuwa maarufu na kabla hujawa maarufu kuna tofauti gani?

Ben Pol: Aisee tofauti ni kubwa sana, maana nikijiangalia kutoka Bernad hadi Ben Pol ni moja ya hatua kubwa tofauti. Nashukuru umaarufu umenisababishia kujuana na watu wengi na kupata dili za kimaendeleo.

Mwanaspoti: Kwanini huonekani na mpenzi wako?

Ben Pol: Unajua mpaka uanze kutembea na mtu kwenye jumuiya ni mpaka ujiridhishe vitu fulani fulani na labda muwe kuna hatua fulani mmefika, lakini uchumba na ndoa, sio unatembea na mtu na kumuonyesha kumbe mna migogoro. Hivyo lazima vitu muhimu vifanyike kwanza, mambo ya uchumba na pete na baadaye ndoa inakaribia ndio mnaweza kufanya hivyo.

Mwanaspoti: Kuna baadhi ya watu wanadai unaringa na kujisikia vipi kuhusu hilo?

Ben Pol: Unajua mtu ambaye hajawahi kukaa nawe hawezi kukujua vyema, maana akisema unaringa ni kwa sababu huwezi kukutana na kila mtu njiani, lakini mimi sina tabia ya kuringa kwa watu wanaonifahamu na kunizoea.

Mwanaspoti: Kitu gani kimebadilisha maisha yako?

Ben Pol: Ni baada ya kupata mtoto. Hiki ni kitu kikubwa sana kwangu, kwani amebadilisha maisha yangu sana.

Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani siku ukiwa huna mishemishe unapenda kufanya nini?

Ben Pol: Napenda kuangalia runinga hasa muziki na kucheza na mtoto wangu tu.

Mwanaspoti: Hivi ulishawahi kuumizwa na mapenzi?

Ben Pol: Weee tena usinikumbeshe kabisa. Ndio maana nimejifunza kutokukurupuka hadharani kuonyesha mwanamke wangu. Kifupi nimeshaumizwa sana na nilichukulia kama mapito tu.

Mwanaspoti: Hivi ni kweli ulikuwa ukitoka na Ebitoke kimapenzi?

Ben Pol: Sikuwahi kuwa na mahusiano naye kwanza, ila lile tuki wala halikuwa kiki kama wengi walivyodhani. Ebu ngoja nililiweke huili wazi kwa ufupi. Unajua kilichotokea ni kwamba hatukufanikiwa kuwa na uhusiano, ila Ebitoke alikuja kwangu baada ya kupitishwa na mashabiki ili awe mpenzi wangu. Mashabiki waliamua kunitafutia mpenzi na kumtaja Ebitoke, lakini wakati huo mie sikuwahi kumuona wala kujua yukoje. Ilifikia hatua hadi familia yangu wakanipigia simu na kuniambia tumemuona mkwe wao kwenye Televisheni, yaani hadi familia nikaona nao wamemshabikia jambo hilo.

Mwanaspoti: Mbona sasa Ebitoke alikuwa akitamba wewe ni wake?

Ben Pol. Kwa hali ilivyokuwa, Ebitoke alijiaminisha kuwa mimi ni mpenzi wake, watu wote waliompitisha na kuungwa kwake na familia ilimpa ujiko sana, nami kwa kutokata kuwaangusha waliompitisha, nikakubali na msimamowa wao, lakini hapo katikati kuna vitu vingine nilikuwa naviona kwenye tv na mitandao, ambavyo alikuwa hawezi kuniambia ndipo nikashindwana naye. Lakini kwa kuwa tulikuwa tunataka watu kuwapa kitu wanachotaka kusikia sisi ni wapenzi nasi tulikubaliana kufanya hilo, ila ukweli kabisa ni kwamba hakukuwa na mapenzi.

Mwanaspoti: Asante sana kwa ushirikiano Ben Pol

Ben Pol: Nashukuru sana, karibu tena!

Advertisement