Bao la ugenini barani Afrika bado linahitajika

Saturday November 9 2019

 

By Ally Mayay

Wiki iliyopita tumesuhudia mechi mbalimbali za mashindano makubwa ya klabu bingwa barani Ulaya na kuona baadhi ya timu zikifanikiwa kupata matokeo katika viwanja vya ugenini, huku nyingine zikipata katika viwanja vya nyumbani ikiwemo Liverpool ambayo ilipambana na KR Genk anayochezea Mtanzania Mbwana Samatta inayotokea Ubelgiji.

Miongoni mwa mechi hizo ni pamoja na ile ya Chelsea dhidi ya Ajax Amsterdam iliyoisha kwa sare ya magoli 4-4 katika uwanja wa nyumbani wa Chelsea, Stamford Bridge; mechi kati ya Barcelona dhidi ya Slavia Prague iliyoisha kwa suluhu katika uwanja wa nyumbani wa Barcelona, Camp Nou.

Nayo timu ya RB Leipzig kutoka Ujerumani ilipata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Zenit St Petersurg ugenini nchini Urusi katika jiji la Saint Petersburg, hivyo katika michuano hiyo timu kupata ushindi ugenini ni kitu cha kawaida, ndio maana timu kubwa kama Barcelona au Chelsea zinahangaika kupata sare katika viwanja vya nyumbani.

Lakini sio matokeo hayo tu ya mechi za mzunguko wa nne, pia katika mzunguko wa pili wa mechi hizo za klabu bingwa barani tulishuhudia Tottenham Hotspurs ikipata kipigo cha magoli 7-2 kutoka kwa Bayern Munich katika uwanja wa nyumbani jijini London.

Nayo Ajax Amsterdam ilipata matokeo ya ushindi wa 3-0 ugenini dhidi ya Valencia ya Hispania, huku Olympic Lyon ya Ufaransa ikipata ushindi wa magoli 2-0 ugenini dhidi ya RB Lepzig, hivyo matokeo yote hayo kuendelea kuonyesha kutokuwepo kwa tofauti ya viwango vya wachezaji nyumbani na ugenini.

Miaka ya hivi karibuni wajumbe wa Shrikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), waliwahi kujadiliana na kusema kuwa kwa kasi ya maendeleo ya mchezo wa soka barani humo na duniani kwa ujumla, na namna ambavyo unavyoendeshwa katika mazingira ya uwazi kwa kwa kila mtu, huko mbele ya safari wanaelekea kubadilisha kanuni ya faida ya goli la ugenini.

Advertisement

Hii ni kwa sababu tofauti kati ya timu mwenyeji na ngeni ina mchango mdogo katika kufanikisha timu ya nyumbani kunufaika moja kwa moja kwa kucheza nyumbani, huku timu ngeni ikiathirika na kupoteza mechi tu kwa sababu ya kucheza katika uwanja wa ugenini ambao viwango vyake havina tofauti na vya uwanja wanaoutumia nyumbani kwao, hivyo kuwa katika viwango sawasawa.

Hali hiyo ukiiangalia kwa kulinganisha soka la Ulaya na la kwetu Afrika unaweza kuona kuwa na mantiki kwa kanuni hiyo kuwepo hapa Afrika kwa kuwa tofauti kati ya uwanja wa nyumbani na uwanja wa ugenini ipo, tena ni kubwa wakati katika soka la Ulaya unaweza kukubaliana nao kuwa tofauti ya uwanja wa nyumbani na ugenini ni ndogo kiasi cha kutoathiri moja kwa moja viwango vya wachezaji uwanjani.

Hivyo, hata kama kanuni za soka barani humo zikibadilika na kusababisha timu kutokuwa na faida ya goli la ugenini baada ya kuthibitika kutokuwepo kwa tofauti kati ya uwanja wa nyumbani na wa ugenini kuanzia katika maeneo ya miundombinu na kimazingira kutoka taifa moja kwenda jingine.

Lakini pia ubora wa miundombinu ya usafiri ni miongoni mwa vitu vinavyosababisha kutokuwepo kwa tofauti hiyo. Wakati huku Afrika tofauti kati ya nyumbani na ugenini ni kubwa kiasi cha kuonekana moja kwa moja kuathiri uwezo wa wachezaji uwanjani, hivyo kanuni hiyo kuwa na mantiki.

Nazungumza hivyo kwa sababu siyo kila kanuni inatakiwa kuigwa kwani hata ukiangalia ukubwa wa Bara la Afrika kwa kulinganisha na la Ulaya utaona kuwa Afrika ni kubwa mara tatu zaidi ya Ulaya, hivyo ni kazi rahisi sana kwa timu kusafiri kutoka Ulaya ya Kaskazini kwenye Kusini.

Hiyo ni tofauti na Mamelody Sundowns inapotaka kusafiri kutoka Afrika Kusiki kwenda kucheza na Raja Casablanca nchini Morocco iliyo Kaskazini mwa Afrika kutokana na umbali ulipo baina ya nchi hizo. Bara la Ulaya lote lina ukubwa wa kilomita za mraba milioni 10.1 wakati la Afrika lina ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya milioni 30.2.

Na hata kwa kigezo cha ukubwa wa eneo hilo kijiografia, ukichukulia mfano wa mechi za ndani ya nchi, kwa mataifa mengi ya Afrika ukiachilia mbali machache ambayo yana maeneo madogo, lakini mengi kama vile DR Kongo, Nigeria na kadhalika hayajafanikiwa kuwa na miundombinu wezeshi ya usafiri wa haraka na rahisi kama ilivyo katika yaliyopo barani Ulaya.

Hata tunapokuwa tunafananisha siku wanazotumia kusafiri wachezaji wanaocheza katika Ligi Kuu England kwa kulinganisha na wanaocheza nchini ni vyema tukajua kuwa Tanzania ni kubwa mara nne zaidi ya muunganiko wa mataifa ya Uingereza, Scotland, Wales na Ireland Kaskazini huku ikiwa ni kubwa mara saba zaidi ya Uingereza peke yake.

Hivyo ni rahisi sana kwa timu kusafiri kutoka Cardiff kwenda kucheza mechi London na kurudi siku hiyohiyo kuliko mchezaji kutoka Bukoba- Kagera au Musoma - Mara kwenda kucheza mechi Songea (Ruvuma), Mbeya au Sumbawanga (Rukwa) na kurudi siku hiyohiyo.

Advertisement