ETI GUNDU! Bale akipangwa tu dhidi ya Barca Bernabeu, Madrid inakufa

Friday March 1 2019

 

MADRID, HISPANIA

UMESHAWAHI kusikia kitu kinachoitwa gundu? Basi Gareth Bale ana gundu.

Ndiyo, Bale ana bahati mbaya fulani hivi anapokabiliana na Barcelona kwenye Uwanja wa Bernabeu.

Staa huyo wa kimataifa wa Wales, amekabiliana na Barcelona uwanjani Bernabeu mara tano na mara zote hizo, amekuwa kwenye majonzi tu, timu yake ikichapwa.

Usiku wa juzi Jumatano, ilikuwa mara yake ya tano kukabilisha na Barcelona kwenye Uwanja wa Bernabeu na ilikuwa mara yake ya tano kufungwa na timu hiyo kwenye mechi za El Clasico zilizofanyika kwenye uwanja huo wa nyumbani wa timu yake, Los Blancos.

Rekodi hiyo chafu kwa Bale iliendelea baada ya kikosi chake kuchapwa Tatu Bila na Barcelona, shukrani kwa mabao mawili ya Luis Suarez na lile moja la kujifunga la Raphael Varane yalitosha kuifanya Real Madrid kusukumwa nje ya michuano ya Copa del Rey.

Gundu. Basi bana, Jumamosi, yaani kesho, Barcelona itarudi tena Santiago Bernabeu kukabiliana na Real Madrid kwenye El Clasico na safari hii itakuwa mechi ya La Liga.

Basi bana, mashabiki wa Real Madrid hawamtaki Bale acheze mechi hiyo, kwa sababu ana gundu. Akicheza tu, lazima wafungwe.

Bale, alitua Real Madrid akitokea Tottenham Hotspur kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo, Pauni 85 milioni mwaka 2013. Lakini, tangu atue kwa wababe hao wanaofahamika kama Los Blancos amekwenda kuwatia gundu tu kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao hao wakubwa.

Mechi alizocheza Bale dhidi ya Barcelona na kushinda zile za ugenini, lakini alizocheza nyumbani zote, kichapo kiliwahusu Madrid.

Katika msimu wake wa kwanza, Barcelona ilishinda mechi zote za ligi, nyumbani na ugenini, ambapo Lionel Messi alipiga hat-trick kwenye ule ushindi wa 4-3 uwanjani Bernabeu.

Msimu wa 2015/16, Real Madrid ilichapwa 4-0 uwanjani Bernabeu, Bale akiwamo uwanjani, lakini alikwenda kulipa kisasi, huko Nou Camp alipotoa asisti kwenye ushindi wa 2-1 baadaye msimu huo.

Misimu miwili ya mwisho iliyopita kwenye La Liga, Barcelona ilishinda mara mbili Bernabeu, 3-2 Aprili 2017 – ambapo Messi alifunga bao la ushindi katika dakika 92 na ule ushindi wa 3-0, Desemba mwaka huo huo.

Inaonekana gundu kwa sababu, Real Madrid mechi zake mbili ilizoshinda dhidi ya Barcelona uwanjani Bernabeu, zote Bale hakucheza.

Hiyo ilikuwa kwenye mechi ya ligi msimu wa 2014/15 na kisha kwenda mechi ya marudiano ya Supercopa mwanzoni mwa msimu uliopita, ambapo Marco Asensio alifunga bao matata kabisa.

Usiku wa juzi Jumatano alicheza na kikosi chake kikakumbana na kipigo. Hapo dhahiri ikathibitisha kwamba supastaa huyo ana gundu dhidi ya Barcelona wanapokwenda kucheza Bernabeu, akicheza Real Madrid lazima ichapwe. Kiwango chake cha usiku wa juzi kimekuwa kituko tu huko kwenye Mtandao wa Twitter, watu wakikejeli shuti lake alilopiga na kupaa juu.

Mabao yake yote mawili aliyofunga Bale dhidi ya Barcelona, amefanya hivyo kwenye uwanja mwingine na sio Bernabeu.

Alifunga bao la ushindi kwenye fainali ya Copa del Rey mwaka 2014 alipomvuruga beki Marc Bartra kwa zile mbio zake uwanjani Mestalla. Kisha bao lake jingine alifunga kwenye sare ya 2-2 iliyopatikana uwanjani Nou Camp msimu uliopita.

Kwa ujumla wake, rekodi ya mechi zake zote alizocheza dhidi ya Barcelona ni 13, ameshinda tatu, sare mbili na kupoteza nane. Kesho, Jumamosi, Barcelona itacheza na Real Madrid kwenye mechi ya pili ya El Clasico ya La Liga msimu huu, hivyo huo ni wakati wa Bale kumaliza gundu lake, kipute hicho kitakapopigwa uwanjani Bernabeu nyumbani kwa Madrid.

Advertisement