TASWIRA YA MLANGABOY : Azam imejificha katika kichaka cha Kombe la FA

Muktasari:

Singida United imecheza michezo mitano, imetoka sare miwili, imefungwa mitatu na ina pointi mbili, huku Mtibwa imecheza mechi tano, imetoka sare mara mbili na kupoteza michezo mitatu.

LIGI Kuu Tanzania Bara imeingia katika mapumziko mafupi kupisha mechi za timu za taifa zilizopo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) zitakazochezwa kati ya Oktoba 14 na 18.

Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ Oktoba 14, mjini Kigali na Oktoba 18 itakuwa jijini Khartoum dhidi ya Sudan na mshindi wa mchezo huo atapata tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN 2020 kule Cameroon.

Wakati ligi hiyo ikiingia katika mapumziko mabingwa watetezi Simba wameendelea kung’ang’ania kileleni mwa Ligi Kuu wakiwa na pointi 12, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi tisa sawa na Kagera Sugar, huku Lipuli, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting zikiwa na pointi nane kila mmoja.

Hadi sasa kuna timu za Mbeya City, Ndanda FC, Singida United, Mtibwa Sugar na Biashara United hazijaonja ladha ya ushindi. Mbeya City ina pointi nne baada ya kutoka sare katika mechi zote nne wakati Ndanda FC imecheza michezo mitano, imetoka sare mitatu na imefungwa miwili.

Singida United imecheza michezo mitano, imetoka sare miwili, imefungwa mitatu na ina pointi mbili, huku Mtibwa imecheza mechi tano, imetoka sare mara mbili na kupoteza michezo mitatu. Biashara imecheza mitano, imetoka sare mara moja na imefungwa minne na kuvuna pointi moja. Pointi 12 za Simba ni sawa na pointi ya timu hizo tano ambazo hazijashinda za Mbeya City (4), Ndanda (3), (Singida (2), Mtibwa (2) na Biashara moja.

Simba imefunga mabao 10, Biashara moja na Mtibwa ndiyo timu iliyofungwa idadi kubwa ya mabao ikifungwa tisa wakati Azam FC nyavu zake zimetikiswa mara moja.

Katika kipindi hiki tumeshuhudi Singida United ikiachana na kocha wake Fred Minziro, kama ilivyokuwa kwa Biashara United ikimtupia virago, Amri Said yote kutokana na matokeo yasiyolidhisha ya timu hizo.

Kwa hali ya ligi inavyokwenda hakuna ubishi msimu huu tutashuhudia makocha wengi wakitimuliwa kwa sababu viongozi wanataka kuhakikisha timu zao zinapata matokeo mazuri katika kuepuka janga la kushuka daraja kwa kuwa msimu huu zitashuka timu nne moja kwa moja, huku mbili zikitakiwa kucheza mtoano.

Hiyo ni moja kati ya sababu iliyofanya Ligi Kuu msimu huu kuanza kwa kasi na ushindani mkali jambo ambalo kila mpenda soka angetamani kuliona linaendelea hivi hadi mwisho wa msimu.

Ushindani wa aina hii utasaidi katika kupatikana bingwa bora anayetokana na kiwango chake uwanjani, pia, timu zinazoshuka zitajitathimini zenyewe kwamba hazikustahili kuendelea kuwepo.

Hata hivyo, pamoja ushindani huo bado kuna nafasi kubwa ya bingwa akatoka Kariakoo kama siyo Simba basi ni Yanga, tumezoea maisha haya.

Yanga imetwaa ubingwa mara 27, ikifuatiwa na Simba mara 20, huku Mtibwa Sugar ikifuatiwa kwa mbali ikiwa imetwaa taji hilo mara mbili.

Timu nyingine zilizowahi kuchukua ubingwa huo ni Cosmopolitans (1967), Mseto Sports (1975), Pan African (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988) na Azam FC (2013-14).

Hata hivyo, tangu Azam ilipochukua ubingwa huo msimu wa 2013-14 ilionekana kama tumaini jipya la kumaliza utawala wa Yanga na Simba, lakini taratibu wamekuwa wasindikizaji katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu. Azam hali inavyokwenda imeanza kuingia katika historia mbaya ya timu zinazotwaa ubingwa kushindwa kurudia mafanikio hayo.

Ukiangalia rekodi za hapa nchini Cosmopolitans baada ya kutwaa ubingwa 1967, Mseto Sports (1975) zote zilipotea na sasa zimekufa kabisa.

Ukingalia Pan African ilitwaa ubingwa (1982), na Tukuyu Stars (1986) kwa sasa zinashiriki katika ligi za mikoa. Wakati Coastal Union (1988) na Mtibwa Sugar (1999, 2000) zinashiriki katika Ligi Kuu, lakini zimeshindwa kutoa ushindani wowote kwa sasa.

Azam imegundua changamoto ya kutwaa ubingwa Ligi Kuu na kujiepusha na presha za Yanga na Simba imeamua kutafuta kichaka chake cha kushiriki mashindano ya kimataifa kupitia Kombe la FA.

Ukiangalia nguvu inayotumia Azam katika Kombe la FA unaweza kujiuliza kwanini inashindwa kufanya hivyo katika Ligi Kuu.

Jibu langu ni rahisi tu kwamba imekubali kuingia katika historia mbaya ya kutwaa ubingwa na kupotea kama Mseto, Pan, Tukuyu na Mtibwa Sugar na nyingine.

Uwekezaji uliofanywa kwa timu ya Azam usajili pamoja na ubora wa kikosi unaacha maswali mengi kwanini inashindwa kuwa mabingwa kila mwaka.

Msimu huu ndiyo kwanza umeanza, lakini siioni Azam kama mshindani wa kweli wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ila naamini itamaliza katika nafasi tatu za juu. Ni lazima viongozi wa Azam wajiwekee malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ili washiriki Ligi ya Mabingwa siyo kuendelea kujificha katika Kombe la FA.