Breaking News
 

Azam FC ni kubwa, lakini hatuyaoni mambo yake makubwa

Thursday September 13 2018Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By JOSEPH KANAKAMFUM

Nikiiangalia Azam hii wala siimalizi, najaribu kuingiza fikra za watu wengi hasa kipindi wawekezaji hawa kutoka makampuni ya Bakhresa walipoamua kuingiza pesa zao kwenye soka, matarajio ya watu yalivyokuwa siimalizi hata kidogo.

Nachukua picha za mawazo ya wapenda soka nchini tulivyokuwa tukiona maendeleo ya uwekezaji kuanzia ndani hadi nje ya uwanja, kwa maana ya kuwa na vikosi bora vyenye ushindani, ndani ya uwanja wakijenga msingi wa soka toka chini kwa kuwa na vikosi vya vijana kuanzia miaka 15, 17 na 20.

Wamejenga kiwanja kizuri cha kuchezea chenye vigezo vyote vya soka la kimataifa, wamejenga hosteli za kuishi wachezaji na kutengeneza ofisi nzuri wakiweka Gym ya kisasa na kutengeneza maeneo mengi ya kufanyia mazoezi.

Baada ya kufanya uwekezaji huo matajiri waliacha wataalamu wafanye Kazi yao ili kuifanya klabu ya Azam kuwa kubwa, ili zile ndoto za kuiona Azam ikifanana na kina TP Mazembe, Al Ahly, Kaizer Chief, Mamelodi Sundown, Etoile du Sahel na nyinginezo zikitimia.

Zile ndoto za kuiona Azam inatawala soka la Tanzania kwa kunyakua vikombe vingi nchini na nje ya nchi nayo inatimia huku ikitandaza soka la kiwango cha kuvutia, hapa ndipo ninaposhikwa na mshangao huku nikijiuliza kunani Azam hii.

Unaweza kuanza kujiuliza hivi kwa nini Azam kama timu haina jicho la kuvumbua vipaji vya hali ya juu kwa wachezaji waliopo ndani ya nchi, kwa nini Azam hawajawahi kutuletea kipaji maridhawa cha mchezaji mzuri wa soka.!

Wakati kina Mazembe wana rundo la wachezaji wenye vipaji vizuri vya kuzaliwa vya soka, mbona kina Simba na Yanga pamoja na kuwa wana macho mengi nchi nzima kiasi ambacho mchezaji mzuri akionekana huko mikoani ni rahisi kupatikana kwa sababu nchi hii imegawanyika Kisimba na Kiyanga, lakini bado kwa Nguvu za kiuchumi ilizonazo Azam ilikuwa rahisi kuvipata vipaji hivi.
Mfano huko nyuma Azam ilishawahi kuchukua vipaji vya wachezaji kama Ramadhani Chombo, Mrisho Ngasa, akaja Ramadhani Singano lakini hawa wote hawakuvumbuliwa na Azam kama Azam.

Azam hawajawahi kutuletea kipaji halisi cha mchezaji hasa wa ndani mwenye kipaji kikubwa, na si mchezaji tu bali wachezaji ambao wangeweza kuja kuwa na faida kubwa kwa nchi yetu, hata hii miguu miwili mitatu ya kina Kichuya , Ajibu hatujawahi iona ndani ya Azam.

Unajiuliza wataalamu wote hao waliopita na waliopo pale Azam kwa miaka yote hii wameshindwaje kutuletea vipaji halisi vya wachezaji wakati kichwa kimoja tu kilichokuwa pale Makongo Sekondari enzi hizo Kanali Mstaafu Idd Omari Kipingu kilikuwa kikituletea vipaji vya kumwaga vya wachezaji vijana, wanashindwaje hawa wenzetu?
Kipingu alituletea kina Haruna Moshi` Boban`, Juma Kaseja, Jerrison Tegete na wengineo wengi ambao wakilikuwa tegemeo la Taifa kwa muda mrefu.

Bila shaka wengi wa wataalamu walio ndani ya klabu ya Azam bado hawatambui kuwa Azam Fc ipo tofauti na klabu nyingine, wanashindwa kuitambulisha klabu kwa kuwa na jicho zuri la kuitengeneza klabu kuwa kubwa inaonekana wengi wanaishi na kutenda kienyeji zaidi, badala ya kuweka kitu cha baadaye kwa kumbukumbu na historia ya kwao kwa vizazi vijavyo vya Azam.

Angalia jinsi Stars ya juzi iliyokuwa na wachezaji wengi waliokuwa ndani ya kikosi cha Azam kwa pamoja miaka nyuma na bila shaka Azam ingeijaza Stars kutokana na ubora wa wachezaji wao, kulikuwa na Aishi, Aggrey Morris, Mwantika , Gadiel Michael, Frank Domayo, Mudathir Yahaya, Himid Mao, Shaban Chilunda na Farid Mussa achana na wachache ambao waliondolewa kina Erasto Nyoni na John Boko hawa wangekaa kwa muda mrefu pamoja ndani ya Azam wangeipa mafanikio timu.

Ilitokea huko nyuma wachezaji wengi waliokuwa bora wakikaa ndani ya kikosi cha timu kwa muda mrefu ni faida kwa klabu na Taifa, mfano Simba mwaka 2002 waliizaja Taifa Stars kuanzia golini hadi Mbele nakumbuka Stars ikicheza dhidi ya Zambia pale Uhuru kikosi cha Stars kilikuwa na Juma Kaseja, Mecky Mexime, Abdul Mtiro, Bonifas Pawasa, Victor Costa, Matola, Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe, Emanuel Gabriel, Joseph Kaniki na Yahya Akilimali, hiki ni kikosi cha wachezaji bora kilichokwenda kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali ya klabu na Taifa.

Advertisement