Asante Salah, Aubameyang, Mane kwa kuibeba Afrika

Tuesday May 14 2019

By Boniface Ambani

Ligi Kuu England msimu wake 2018/19 umefikia kikomo Jumapili ya wikiendi iliyopita, huku mabingwa watetezi, Manchester City wakilihifadhi taji lao kwa mara nyingine baada ya kushinda mechi yao ya mwisho kwa mabao 4-1 dhidi ya Brighton & Hove Albion.

Kwa upande mwingine vita ya kuwania taji hilo ilikuwa kule Anfield wakati Liverpool ikicheza mchezo wake wa mwisho na Wolverhampton Wanderers walioshinda mabao 2-0.

Kwa matokeo hayo ya ushindi wa Liverpool waliishia tu kujipatia pointi tatu huku ubingwa ukienda kwa Man City ya Pep Guardiola kwa mara nyingine tena ikiwa ni taji lao la nne mpaka sasa.

Nawapa pole Liverpool kwani walistahili kubeba taji hilo hasa kwa sababu ya kikosi chao bora msimu huu lakini ni kuzifdiwa tu ujanja na kikosi cha Pep ambao wanastahili pongezi kwa kutetea taji lao.

Hata hivyo, makala ya leo yanaangazia zaidi wachezaji wa kiafrika ambao wamekuwa moto kweli kwenye ligi hiyo msimu huu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England, wachezaji watatu kutoka Bara la Afrika wamenyakua tuzo ya ufungaji bora.

Advertisement

Tuzo hiyo ya Kiatu cha Dhahabu imewaendea mastaa Mohamed Salah, Pierre Aubameyang na Sadio Mane, wote wakilingana kwa mabao 22 na hivyo kugawana tuzo hiyo. Ilikuwa ni furaha isiyo na kifani.

Ingawaje wowte hao hawakushinda taji la Ligi Kuu, hata hivyo ni furaha kwa sababu tuzo ya Kiatu cha Dhahabu imekuja Afrika na si kimoja tu, bali vitatu, tunastahili kufurahia mafanikio hayo ya wenzetu Waafrika.

Hii inaonyesha Afrika tuna vipaji vizuri mno. Ni sisi wenyewe tunafaa kuvikuza kwani hadi kuwa mfungaji bora sio kazi rahisi. Ni lazima upambane kweli.

Kwa miaka miwili mfululizo Salah anabeba tuzo hiyo, baada ya msimu uiopita pia kufanya hivyo kwa kufikisha mabao 30, akiwa ni mchezaji pekee kutoka Afrika tofauti na msimu huu wakigawana tuzo hiyo.

Ni wazi msimu huu Salah amekwama kutokana na majeraha aliyoyapata na kupunguza makali yake kwani ni yeye kwa kipindi kirefu amekuwa akiongoza kwa ufungaji msimu huu.

Lingine lililomponza msimu huu ni kutokufunga kwanye mchezo wa mwisho walioshinda mabao 2-0.

Aubameyang alifunga mabao mawili dhidi ya Burnley na Sadio Mane akafunga mawili dhidi ya Wolves.

Nafurahi kuona vijana wetu wa Afrika waking’ara.

Changamoto kwa wachezaji wetu bara hili. Ni lazima mtie bidii. Hawa wote mkumbuke nidhamu ambayo wako nayo ni ya hali ya juu.

Waangalie wakati wowote wapo uwanjani. Hawashughliki na kubishana na wachezaji pinzani ama marefa uwanjani. Wametulia kutulia.

Shughuli ni kufunga mabao. Napenda hiyo kazi wanafanya. Changamoto kwenu wafungaji ama kwa ufupi washambulizi.

Wakati huo huo nampongeza Sergio Kun Aguero wa Man City ambaye alimaliza nyuma ya watatu hao akiwa na mabao 21.

Jamie Vardy wa Leicester City alipiga mabao 18, Raheem Sterling wa Man City mabao 17, Harry Kane wa Tottenham 17, Hazard wa Chelsea mabao 16.

Ningependa kuona mbio kama hizi Ligi Kuu Kenya, Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Advertisement