Amunike na Waafrika wengine waliocheza Barcelona

Thursday August 9 2018

 

HATIMAYE Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imemtangaza staa wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa timu hiyo. Amunike anatua Tanzania akiwa kama mchezaji wa zamani mwenye jina kubwa na ni miongoni mwa mastaa saba wa Afrika waliowahi kucheza klabu maarufu ya Barcelona ya Hispania.

Jorge Alberto Mendonca (1966-1969)

Katika historia anaingia kama Mwafrika wa kwanza kabisa kuvaa jezi ya Barcelona. Staa huyu wa Angola aliichezea Barcelona kwa miaka mitatu kati ya mwaka m1966 mpaka 1969. Muda mrefu wa maisha yake ya soka staa huyu aliyezaliwa Jiji la Luanda kwao Angola aliutumia kucheza Hispania.

Alitua Hispania kukipiga klabu ya Derpotivo la Coruna halafu Atletico Madrid kisha akatua Barcelona na mwishowe kumalizia soka lake Real Mallorca. Mendonca aliichezea Barcelona baada ya miaka 67 tangu kuanzishwa kwa timu hiyo.

Emmanuel Amunike (1996-2000)

Miaka 30 baada ya Mendonca kuachana na Barcelona, hatimaye staa wa Nigeria, Emmanuel Amunike aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa pili kuvaa jezi ya Barcelona. Aliivaa jezi hiyo kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2000, kwanza chini ya kocha wa Kiingereza marehemu, Sir Bobby Robson kisha chini ya kocha maarufu wa Kidachi, Louis van Gaal. Alitwaa mataji sita na Barcelona katika kipindi chake cha miaka minne klabuni hapo.

Samuel Okunowo (1998-2001)

Staa mwingine wa Nigeria ambaye aliwahi kucheza Barcelona. Katika historia anachukuliwa kama mchezaji wa tatu kutoka Bara la Afrika kuvaa jezi ya Barcelona. Alicheza mechi 14 tu kwa Barcelona akitokea klabu ya Shooting Stars ya kwao Nigeria lakini hata hivyo, baadaye Barcelona ilimtoa kwa mikopo miwili. Kwanza ni kwenda Benfica ya Ureno, lakini pili akapelekwa CD Badajoz ya Hispania ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza. Mwaka 2002 aliachwa na Barcelona na kuanzia hapo akazurura katika timu mbalimbali za Ugiriki, Romania, Albania na Ukraine.

Samuel Eto’o (2004-2009)

Mchezaji wa Afrika mwenye mataji mengi zaidi barani Ulaya. Eto’o alikuwa Mwafrika wa nne kukipiga Barcelona wakati alipowasili klabuni hapo kutoka Real Mallorca mwaka 2004. Staa huyu wa kimataifa wa Cameroon aliichezea Barcelona mechi 199 akifunga mabao 130 na kupika mabao 42 kwa wenzake. Katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote Barcelona anasimama katika nafasi ya nane huku akiwa ametwaa mataji manane katika kipindi chake alichocheza Barcelona. Anabakia kuwa Mwafrika aliyepata mafanikio zaidi katika jezi ya Barcelona na angeweza kupata mafanikio zaidi kama Kocha Pep Guardiola asingemuuza kwenda Inter Milan ambako pia alitwaa mataji matatu kwa mpigo katika msimu wake wa kwanza tu.

Yaya Toure (2007-2010)

Staa huyu wa kimataifa wa Ivory Coast ambaye kwa sasa anasaka timu ya kuchezea aliweka historia ya kuwa Mwafrika wa tano kukipiga Nou Camp wakati aliposaini Barcelona mwaka 2007 akitokea Monaco ya Ufaransa. Alikuwa mmoja kati ya mastaa wa Barcelona chini ya Pep Guardiola ambao walitengeneza msingi wa mafanikio ya sasa ya Barcelona katika zama hizi. Alitwaa mataji ya ndani lakini pia akatwaa taji moja la Ulaya chini ya Guardiola mwaka 2009. Mwaka uliofuata aliuzwa kwenda Manchester City ambako alipata mafanikio makubwa.

Seydou Keita (2008-2012)

Staa wa kimataifa wa Mali ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa sita wa Afrika kukipiga Barcelona. Aliwasili klabuni hapo akitokea Sevilla ya hapohapo Hispania mwaka mmoja tu baada ya kutua kwa Toure. Na yeye alikuwepo katika kikosi cha Kocha Guardiola kilichotwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2009 pale Rome kwa kuichapa Manchester United mabao 2-0.

Kwa jumla staa huyu alitwaa mataji 14 na wababe hao wa Nou Camp kabla ya kutimia Dalian Yifang ya China mwaka 2012.

Alex Song (2012-2016)

Mwaka ambao Keita aliondoka Barcelona ndio mwaka ambao alipishana na mchezaji wa mwisho kutoka Afrika kuichezea Barcelona. Alexandre Song aliingia Barcelona akiwa mchezaji wa pili kutoka Cameroon kuichezea Barcelona baada ya Eto’o. staa huyu alitwaa mataji mwili na Barcelona katika misimu yake miwili ya kwanza huku akicheza mechi 65 kwa klabu hiyo. Hata hivyo, mara mbili alitolewa kwa mkopo kurudi katika Ligi Kuu ya England kukipiga na West Ham baada ya hapo awali kukipiga na Arsenal. Baadaye Barcelona iliachana naye jumla na akaenda zake Rubin Kazan kwa uhamisho huru.

Advertisement