Amunike apewe ushirikiano ainyanyue Taifa Stars yetu

Thursday August 9 2018

 

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars kuchukua nafasi ya Salum Mayanga aliyeiongoza timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja tu na ushei.

TFF imeamua kuachana na Mayanga baada ya kumaliza mkataba wake tangu Januari na kuendelea kuiongoza timu hiyo na mechi yake ya mwisho akiwa na Stars ni Machi 27, walipovaana na DR Congo na kushinda mabao 2-0.

TFF imempa jukumu Amunike la kuiongoza Stars kama Kocha Mkuu huku pia akizisimamia timu nyingine za taifa za vijana za U-17, U-20 na U-23 kwa muda wa miaka miwili ya kandarasi yake.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo tunamkaribisha Kocha Amunike kuanza majukumu yake, tukimtahadharisha mapema kuwa, ana kibarua kizito cha kuweza kuzisuuza nyoyo za mashabiki wa soka nchini.

TFF na Watanzania kwa ujumla wamemuamini na kumpa kazi ya kuitoa Stars mahali ilipo na kuipeleka mbele, lakini akumbuke kuwa kuna changamoto nyingi ambazo atakabiliana nazo hususani presha za mabosi wake na hata mashabiki.

Tunatambua kuwa, Amunika hana kazi rahisi kama anavyofikiria, lakini bado kwa uzoefu wake katika soka la Afrika na akipewa ushirikiano wa kutosha na waajiri wake pamoja na mashabiki anaweza kuleta tofauti ndani ya soka letu.

Hata kama rekodi zake kama kocha hazisisimui sana, kama enzi za uchezaji wake tangu akiwa Julius Berger ya kwao Nigeria, Barcelona na Spoting ama na timu yake ya taifa ya Nigeria Super Eagles, bado Amunike hawezi kubezwa.

Tunaamini ana kitu ambacho kitaisaidia timu yetu, muhimu ni kwamba aachwe afanye kazi zake bila kuingiliwa ama kupangiwa wachezaji wa kuwateua ndani ya kikosi chake.

TFF na kamati zake ikiwamo Kurugenzi ya Ufundi imesaidie kumwezesha kuviona vipaji vikicheza uwanjani, kisha aamue mwenyewe kuwateua na sio kupewa orodha ya wachezaji wa kuwaita ndani ya Stars.

Amunike alikuwa mchezaji nyota enzi zake na ana uzoefu wa muda mrefu kwa nafasi yake ya ukocha, hivyo ni rahisi kung’amua mchezaji yupi ana ubora wa kuweza kuitumikia timu ya taifa, ndio maana tunataka asiingiliwe katika kazi zake.

Mbali na kuachwa afanye kazi zake kwa weledi na ujuzi wake, pia atekelezewe yale yote ambayo atakuwa anayahitaji kwa ajili ya kufanikisha mipango yake kazini ikiwamo kwa suala la mechi za kujipima nguvu na mengine ya muhimu kwa Stars.

Tunalisema hili kutokana na ukweli kumekuwa na utamaduni wa wasimamizi wa soka iwe ngazi ya taifa ama klabu kuwanyenyekea na kuwaheshimu makocha wa wenye ngozi nyeupe na kuwadharau makocha weusi hasa wazawa.

Amunike sio mzawa, lakini ana ngozi nyeusi kama ilivyo kwa watanzania, hivyo asichukuliwe kwa mnasaba huo na kushindwa kutekelezwa kila anachokuwa akikitaka maadamu ni katika utekelezaji wa kazi zake ndani ya Stars.

Tunaamini hayo yote yakifanyika kwa ufanisi na wachezaji watakaoteuliwa kuunda kikosi cha Stars wakajitoa uwanjani kwa uwezo wao wote ni wazi timu hiyo ina kila sababu ya kupata matokeo mazuri na kusuuza nyoyo za Watanzania.

Kama mipango itaanza mapema kabla ya kuwakabili Uganda The Cranes katika mechi ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zitakazofanyika Cameroon, tunaamini Stars inaweza kufanya maajabu Uganda.

Wachezaji kucheza kwa kujituma, kuonyesha kuwa wanalipigania taifa lao, ni wazi kutampa nafasi mwalimu ya kuwa na moyo wa kufundisha na kuisimamia timu kikamilifu kwa michezo iliyosalia.

Nidhamu pekee ndiyo itakayoleta mafanikio pamoja na kumpa ushirikiano. Tunarejea kuomba ushirikiano huo na ndio maana tunasisitiza kuwa, Kocha Amunike apewe ushirikiano wa kutosha na waungwe mkono na Watanzania wote ili ailetee mafanikio Taifa Stars na kusaidia kurejesha heshima ya soka la Tanzania iliyofifia kwa muda mrefu. Tunaamini hakuna kisichowezekana, muhimu mipango kamambe na utekelezaji tu! Kila la Heri Kocha!

Advertisement