Kagere kwa Simba tumhesabie siku tu

STRAIKA mpya kutoka Gor Mahia, Meddie Kagere kaanza na mguu wa bahati Simba. Kabla ya mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame, straika huyo mkongwe tayari alikuwa na mabao mawili, nyuma ya vinara Adam Salamba na Shaaban Idd wenye mabao matatu kila mmoja.

Huenda na leo pia akatupia kwani timu wanayocheza nao sidhani kama wana ubavu wa kuzuia pilikapilika zake.

Jamaa ni fundi wa kutupia. Akili yake uwanjani huwa haiwazi kitu kingine zaidi ya kucheka na nyavu.

Gor Mahia wanadai hawajaachiwa pengo, lakini ni wazi bado wanamtamani.

Mabao yake saba katika misimu miwili mfululizo yameisaidia Kogal’O kubeba Kombe la SportPesa, hapo ni mbali na mabao yake katika Ligi Kuu Kenya na hata Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, nashindwa kusema lolote kwa sasa mustakabali wake ndani ya Simba kwa vile rekodi zinaonyesha, ni nyota wachache wa kigeni waliong’ara walikotoka wakaweza kutamba Msimbazi.

Dan Sserunkuma alitua Simba akitokea pia Gor Mahia akiwa kinara wa mabao, lakini aliondoka kwa aibu akisitishiwa mkataba wake, Laudit Mavugo alisakwa kwa udi na uvumba Msimbazi kutoka Burundi, mwisho wake umekuwaje?

Paul Kiongera, Amissi Tambwe na wengine je? Sijajua kama Kagere ambaye ukiangalia katika pasipoti yake inaonyesha anakaribia miaka 32, lakini sura yake ikonyesha amevuka zaidi ya umri huo atamalizana vipi na klabu yake ya sasa.

Ni Emmanuel Okwi tu ndiye anayeyajulia maisha ya Msimbazi, wengine mara nyingi wamekuwa wakibahatisha tu na kama vipi Kagere lazima ajipange, la sivyo ataishia mkumbo ule ule Simba! Muda utaongea, tusubiri tuone.