MKEKA WAKO : Hakuna ubishi Barcelona itailiza Valencia kiulaini kabisa

Muktasari:

Kocha wa Barcelona, Quique Setien anawania kupata ushindi wa pili mfululizo wakati miamba hiyo itakapoifuata Valencia kesho Jumamosi.

Kivumbi cha Ligi Kuu England kinasimama wikiendi hii kupisha mechi za Kombe la FA ambazo zipo katika hatua ya raundi ya nne.

Kutokana na hali hiyo utabiri wetu na muongozo wa kutandika mkeka wikiendi hii tunauelekeza kwenye mechi za La Liga.

Mechi kubwa ya La Liga, ambayo itatupiwa macho zaidi na mashabiki wa soka ni ile kati ya Barcelona dhidi ya Valencia.

Kocha wa Barcelona, Quique Setien anawania kupata ushindi wa pili mfululizo wakati miamba hiyo itakapoifuata Valencia kesho Jumamosi.

Valencia, ambayo ni maarufu kwa jina la Los Ches inauvaa moto wa Barcelona baada ya kuwa imepoteza mechi mbili mfululizo za hivi karibuni.

Wanatakiwa kushinda mchezo huu ili kuweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Mara ya mwisho timu hizi zilipovaana kwenye Uwanja wa Nou Camp, Barcelona iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 mwezi Septemba, mwaka jana.

Hata hivyo, mara ya mwisho kwa Valencia kuifunga Barca kwenye La Liga ilikuwa Februari 2014 na ilikuwa kwenye uwanja wa Nou Camp.

Nao Barcelona hawajapoteza mechi katika uwanja wa Mestalla tangu mwaka 2007.

Barcelona imeshinda mechi tano na kutoka sare mara saba katika uwanja huo ingawa Valencia iliwashinda mabao 2-1 kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme, msimu uliopita.

Angalau kumbukumbu hiyo inaweza kuwapa matumaini kidogo mashabiki wa Valencia.

Wenyeji Valencia wanakabiliwa na mtihani mzito zaidi kwani watapaswa wawe vizuri baada ya kufungwa mabao 4-1 majuzi na Mallorca.

Kimsingi Valencia wapo taabani kwani wameshinda mechi moja katika mechi nne za La Liga.

Valencia kwa sasa inakamata nafasi ya saba ikiwa pointi nne nyuma ya Sevilla inayokamata nafasi ya nne.

Maana yake ni kuwa Valencia ikipoteza mchezo huu itazidi kupoteza matumaini ya kutinga nne bora.

Itaingia katika mchezo huu bila ya staa wao, Dani Parejo, ambaye amesimamishwa kucheza mchezo mmoja wakati Cristiano Piccini ni majeruhi.

Mastaa wengine Rodrigo, Ezequiel Garay na Manu Vallejo wapo kwenye hatihati pia kucheza mchezo huu kwa sababu ya kukabiliwa na maumivu.

Ingawa Valencia watakuwa wanapumua kwani Barcelona itaingia katika mchezo huu bila ya Suarez, ambaye anajulikana kuwa mwiba.

Pia winga Ousmane Dembele hatakuwemo katika kikosi cha Barcelona, kutokana na kuwa majeruhi.

Valencia wataingia katika mchezo huo wakimhofia staa wa Barcelona, Lionel Messi, ambaye kwa sasa yupo katika kiwango kizuri na ndio alifunga kwenye mechi na Granada.

Barca kwa sasa ipo chini ya kocha mpya na imeanza kurudia enzi yao ya kupiga soka la pasi.

Katika siku za karibuni Barcelona imekuwa inafikisha ‘ball possession’ hadi asilimia 82% katika mechi.

Kocha mpya Setien ambacho amefanya katika kuimarisha soka la kushambulia la Barcelona, anawatumia mabeki wa pembeni, Jordi Alba na Sergi Roberto.

Barcelona imerudi katika enzi zake za kupiga soka la pasi na kumiliki mpira zaidi na ninawapa nafasi kubwa zaidi ya kushinda.

Sidhani kama Valencia watakuwa na ubavu wa kuwafunga na kumbuka imepita miaka saba tangu timu hiyo kuifunga Barca.

Valencia itakuwa bila ya mastaa wake, Rodrigo na Dani Parejo lakini angalau mfungaji wao tegemeo Maxi Gomez atakuwamo katika mchezo huo.

Kwani watapaswa kumchunga Messi, ambaye amepachika mabao 17 katika mechi 17 alizocheza msimu huu.

Mara ya mwisho kwa Valencia kupata ushindi dhidui ya Barca kwenye Uwanja wa Mestalla ilikuwa mwaka 2007 wakati timu hiyo iliposhinda 2-1.

Barcelona nadhani watapata ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo huu wa La Liga.

Kutokana na ukweli kuwa kwa kiwango cha sasa cha Barcelona, ndio wenye nafasi ya kushinda mchezo huu ukizingatia na kocha Setien amerudisha soka halisi la Barcelona ambalo tumelizoea la pasi za ‘tiki-taka’.