MTAA WA KATI : Sare zilivyoikatili Liverpool kumaliza ukame EPL

Muktasari:

  • Dakika 10 baadaye, huko Amex zilikuja taarifa kwamba mahasimu wao Man City wameshafungwa bao moja, Glenn Murray wamewatanguliza Brighton. Shangwe zilikuwa kubwa Anfield.

MAISHA ndivyo yalivyo. Kuna wakati yanakuwa mepesi kupata unachokitaka, lakini nyakati nyingine mambo huwa magumu na usipate unachokitaka. Hicho ndicho kilichowatokea Liverpool. Maisha yamefanya ukatili dhidi yao.

Kwenye Ligi Kuu England walipigana kwa kila vita waliyoiweza kubeba ubingwa wa taji hilo, walau iwe kwa mara yao ya kwanza tangu lilipoanzishwa miaka 29 iliyopita. Kwenye mchezo wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Wolves uwanjani Anfield, kuna nyakati zilikuwa za matumaini ya kubeba ubingwa huo.

Baada ya kutambua kwamba wanahitaji ushindi kubeba ubingwa huo, huku wakiomba mabaya kwa wapinzani wao Man City, jambo hilo lilielekea kufanyika na lilitokea ndani ya dakika 90 za mechi za kumaliza msimu hiyo juzi Jumapili.

Wakiwa Anfield, dakika ya 17 tu, Sadio Mane akapiga bao dhidi ya Wolves, bao hilo liliwafanya kuwa na pointi 97, ambao kwa wakati huo zilikuwa zikiwafanya kushika usukani wa ligi.

Dakika 10 baadaye, huko Amex zilikuja taarifa kwamba mahasimu wao Man City wameshafungwa bao moja, Glenn Murray wamewatanguliza Brighton. Shangwe zilikuwa kubwa Anfield.

Hata hivyo, furaha yao hiyo ilimalizika ndani ya dakika moja tu, Sergio Aguero akawasawazishia Man City. Hata hivyo, hadi hapo, Liverpool bado walikuwa wanaongoza ligi, hadi ndoto zao zilipokuja kuzimwa dakika 38, wakati Aymeric Laporte alipokuja kufunga bao la pili kwa Man City, kwani hapo timu ya Guardiola sasa ikawa inashika usukani wa ligi.

Ndoto za Liverpool zilikuja kuzimika kabisa baada ya mabao ya Riyad Mahrez na Ilkay Gundogan.

Baada ya hapo maisha ya Liverpool yalianza sifuri tena kwenye harakati zao za kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Itabidi waanze upya msimu ujao kulisaka taji hilo.

Ni bahati mbaya sana kwao. Timu ambayo imepoteza mechi moja tu katika msimu, inashindwa kubeba ubingwa. Pointi moja inawakatili.

Ikumbukwe kuna wakati Liverpool ilikuwa imeweka pengo la pointi saba kileleni dhidi ya Man City. Ikaja mechi yenyewe kwa wenyewe, Man City ikashinda na kupunguza pengo hilo la pointi kuwa nne na baada ya hapo, Man City ilishinda mechi zote 14 zilizokuwa mbele yao. Wakati Man City ikipoteza mechi nne kwa msimu wote, Liverpool walijiharibia kwenye sare nyingi, wakimaliza msimu kwa sare saba, ambao kimsingi ni pointi 14 zimepotea.

Man City wao wametoka sare mbili, pointi nne hizo na ukijumlisha vipigo vinne ina maana wamepoteza pointi 16 kwa msimu wote. Liverpool wao kwa sare saba na kipigo kimoja wamepoteza pointi 17, hicho ndicho kilichowagharimu.

Lakini, yote kwa yote pongezi kubwa kwa Liverpool kujaribu kuupandisha upinzani kwenye Ligi Kuu England kuwa juu zaidi. Kitu kibaya wamekuwa kwenye ubora mkubwa katika kipindi hiki cha Man City ambao wamefanya uwekezaji mkubwa sana na bila ya shaka wataendelea kuwekeza.

Msimu ujao hakuna ubishi Man City itatengeneza timu yake kwa ajili ya kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu huu watabeba mataji yote matatu ya ndani ya England, wakibeba Kombe la Ligi, Ligi Kuu England na wametinga fainali ya Kombe la FA, ambalo watamenyana na Watford, msimu ujao, Man City watatoa macho zaidi kwenye michuano ya Ulaya.

Kwa kuijenga timu ya Ulaya bila ya shaka watakuwa wameupandisha juu sana upinzani kwenye Ligi Kuu England.