TIMUA VUMBI : Simba bado nafasi ipo kama tu watayafanya haya

Thursday February 14 2019

 

By Mwanahiba Richard

SIMBA juzi Jumanne walimpiga Mwarabu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam bao 1-0, matokeo ambayo wengi hawakuyatarajia kwani walikata tamaa na kipigo cha awali cha bao 5-0 na kikiwa ni kipigo ch amfululizo.

Simba ilifungwa mabao 10 katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, walifungwa na AS Vita ya DR Congo na Al Ahly zote zikiwa mechi za ugenini na mechi za nyumbani hawajapoteza hata moja kwa awali walimfunga JS Saoura bao 3-0.

Kuanzia viongozi, wachezaji hadi mashabiki wao walikata tamaa juu ya mechi yao ya marudiano ingawa walichokuwa nacho ni kujipa moyo kwa watashinda huku wakiwa na hofu zaidi ya matokeo kutoka kwa Waarabu hao.

Mechi hiyo ilipigwa kuanzia saa 10 jioni na ni muda sahihi kwa mujibu wa Caf ambao hutoa ratiba ya muda wa mechi kuchezwa, ni kuanzia muda huo hadi saa nne usiku.

Meddie Kagere ndiye aliyepeleka shangwe Msimbazi dakika ya 64 baada ya kutikisa nyavu za wapinzani wao huku muda uliokuwa umebaki mashabiki waliendelea kuomba matokeo yabaki kuwa hivyo ili wapizani wasisawazishe na kweli ilikuwa hivyo.

Simba sasa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita wakati Al Ahyl wao wakiongoza kundi hilo D kwa pointi saba, JS Sauora wanashika nafasi ya tatu kwa pointi tano huku Vita wakiwa mkiano kwa pointi nne.

Timu zote zimebaki na mechi mbili kila moja na katika mechi hizo ni lazima mechi moja ichezwe ugenini kwa kila timu. Simba watasafiri kwenda Algeria kurudiana na Saoura mwezi ujao, March 8 wakati mechi ya mwisho watakuwa nyumbani wakiikaribisha Vita mwezi huo huo March 15.

Timu nne za Kundi D zina nafasi ya kusonga hatua ya robo fainali ingawa ni timu mbili kila kundi ndizo zitatinga hatua inayofuata.

Mechi zilizobaki zinapaswa kuchezwa kwa mahesabu tu ili kumshusha mpinzani wako na kutengeneza mazingira mazuri.

Hapa msisitizo wangu upo upande Simba kuna mambo ya kufanya kuhakikisha kila kitu kinakwenda sana kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji huku mashabiki wenyewe wakibaki kuwa washangaliaji tu, maana wao jukumu lao kubwa ni uwanjani kuwapa nguvu vijana wao.

Viongozi wa Simba ni wakati wa kuhakikisha sasa wanaweka mambo sawa kwa kuweka nguvu zaidi kwenye michuano hii kwani uwezo wa kufika hatua ya robo fainali unaonekana upo ingawa lengo lao lilikuwa ni kuishia hatua hii ya makundi, hii ni nafasi nzuri kwao kujipima kiwango kwa hatua kubwa zaidi. Hilo linawezekana.

Bodi ya Simba inapaswa kuimarisha kambi ikiwa kwenye ubora wa hali ya juu hata kwa uwekezaji wao huo huo mdogo ukilinganisha na uwekezaji wa timu zilizopo kwenye kundi lao.

Kocha Patrick Aussems ni wakati wake sasa kuimarisha nidhamu ndani ya kikosi chake kwani Simba ina wachezaji wazuri hata kama hawajafikia hatua ya wachezaji wengine wa Afrika lakini kwa uwekezaji wao wanastahili tu kuitwa wachezaji wazuri lakini nidhamu yao imeanza kushuka na ndiyo maana husababisha kiwango chao kinapanda na kushuka kwa nyakati tofauti.

Kocha pekee ndiye anayeweza kulimudu hili na kulisimamia ipasavyo kama alivyokua ameanza ajira yake huku kila mchezaji alionyesha hofu juu ya ajira yake na ubora zaidi ulionekana.

Wachezaji walio wengi ndani ya Simba ni watu wazima wanapaswa kujitambua hatua iliyofikiwa ni kubwa na ya kujitoa zaidi, maana pesa ambayo Simba itavuna ikitinga hatua inayofuata ni kiasi kikubwa mno ambacho pia kitakuwa ni faida ya wachezaji na sio klabu pekee, hivyo nidhamu binafsi ipewe kipaumbele kwa manufaa ya pande zote mbili, klabu na mchezaji kwani mafanikio siku zote hayaji pasipokuwa na nidhamu ya ndani na nje.

Kwa pamoja ndani ya Simba kila kitu kinawezekana bila kusahau ligi kuu kutetea taji maana haitakuwa na maana ya kuweka malengo ya kuchukuwa ubingwa wa Afrika kama jinsi mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ alivyojiwekea malengo hayo ya muda mrefu.

Niwapongeze Simba kwa hatua hii na mtambue kila kitu kinawezekana na nafasi ya kusonga mbele bado ipo.

Advertisement