Ubingwa Liverpool, Man City uko hapa

LONDON ENGLAND, MBIO za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu zimezidi kunoga huku Liverpool ikikomaa mwanzo mwisho kileleni kwenye msimamo wa ligi.

Kikosi hicho kinachonolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp imelinda pengo lake la pointi moja baina yake na Manchester City katika mchakamchaka wa kusaka ubingwa huo baada ya ushindi wao mkubwa dhidi ya Watford juzi Jumatano.

Mabao mawili ya Sadio Mane kwenye kipindi cha kwanza na mengine mawili ya Virgil Van Dijk yalinogesha ushindi wa 5-0 kwenye mechi hiyo na hivyo kuendelea kuwa juu ya Man City, ambao wenyewe walishinda 1-0 dhidi ya West Ham United uwanjani Etihad hiyo hiyo juzi usiku.

Mkwaju wa penalti wa straika Sergio Aguero ulitosha kwa kikosi hicho cha Pep Guardiola kuandikisha pointi tatu muhimu zinazowaweka hai kwenye mchakamchaka wa mbio hizo za ubingwa. Man City watarejea kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo kama watashinda ugenini kwa Bournemouth huko kwenye Uwanja wa Vitality kesho Jumamosi.

Liverpool wao watashuka uwanjani Jumapili watakapokwenda kuwavaa mahasimu wao wa Goodison Park, Everton mchezo ambao Man City wanapiga sala za kutosha kuona wapinzani wao hao katika mbio hizo za ubingwa wanateleza.

Tottenham Hotspur wamechapwa na Chelsea na jambo hilo linazifanya mbio hizo za ubingwa kuwa rasmi za timu mbili, Liverpool na Man City.

Kila timu imebakiza mechi 10, ambazo ndizo zinazoshika hatima ya mbio hizo za ubingwa. Cheki hapo, nani mwenye mteremko kwenye mbio hizo za ubingwa?

Ratiba hiyo inaweza kubadilika muda wowote kutokana na mambo mbalimbali ikiwamo dili za televisheni. Liverpool wanaonekana kuwa na mechi ngumu kadhaa ikiwamo dhidi ya Everton na ile dhidi ya Newcastle United, zote za ugenini. Watakuwa na mechi nyingine ngumu nyumbani wakimenyana na Chelsea na Tottenham na hivyo kumfanya kocha Klopp kukuna kichwa namna ya kupata matokeo kwenye mechi hizo.

Mtihani unaanzia kwenye mechi inayofuata tu, kwani wapinzani wao Man City wataanza kucheza kisha deni linabaki kwao watakapokwenda kuwakabili Everton huko kwao Goodison Park.

Manchester City nao wana shughuli pevu, ambako kocha Guardiola atakuwa na kazi zito kuhakikisha anavuna matokeo kwenye mechi zilizobaki, ikiwamo ile ya mahasimu wao Manchester United itakayopigwa Old Trafford, mwezi ujao.

Manchester City wana kasheshe la kuwakabili Tottenham kwenye ratiba yake ya mechi 10 zilizobaki na kufanya vita hiyo kuwa kazi zaidi. Kwa maana hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa makocha hao wawili, Klopp na Guardiola katika vita yao ya kuwania ubingwa huo wa Ligi Kuu England msimu huu.