Ubingwa FA kaa la moto

Friday March 1 2019

 

By THOBIAS SEBASTIAN

TIMU nane zilizofuzu katika hatua ya robo fainali ya Azam Sports Federation Cu (FA), zimesha fahamika na zote zimetokea Ligi Kuu Bara na hakuna hata moja ambayo imetokea katika madaraja la chini.

Timu hizo nane ni Yanga, Azam FC, KMC, Alliance, Kagera Sugar, Lipuli, Singida United na African Lyon na kati ya hizo atapatikana bingwa ambaye ataiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa katika Kombe la Shirikisho ambalo msimu huu Mtibwa Sugar ndio ilikuwa mwakilishi kabla ya kuondolewa katika hatau ya pili dhidi ya KCCA kutokea Uganda.

Ubingwa wa Kombe la ASFC umekuwa kaa la mato kwa timu tatu ambazo zimechukua ubingwa katika misimu mitatu iliyopita kwani hakuna hata moja iliyoweza kutetea au kufika fainali katika msimu uliofata.

YANGA

Msimu wa kwanza wa mashindano haya, ulikuwa ni 2016, ambapo katika mechi ya fainali zilicheza Yanga na Azam katika Uwanja wa Taifa.

Yanga ikaibuka na ubingwa kwa mara ya kwanza kwa ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Amiss Tambwe (mawili) na Deus Kaseke huku la kufutia machozi kwa Azam lilifungwa na Didier Kavumbagu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya nahodha John Bocco.

Fainali hiyo iliyochezwa Mei 25, mbali ya Yanga kuchukua ubingwa lakini haikwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika na nafasi yake ilichukuliwa na Azam.

Sababu ni kwa kuwa Yanga ilikuwa bingwa wa ligi na kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. Msimu uliofuata 2017, Yanga iliondolewa katika mechi ya nusu fainali na Mbao katika mechi iliyochezwa CCM Kirumba Mwanza kwa bao 1-0, ambalo beki Vincent Andrew ‘Dante’ alijifunga dakika ya 27, kipindi cha kwanza.

Mechi hiyo ilichezwa Aprili 30, ilishuhudia Mbao ikiwa chini ya Kocha Ettiene Ndayiragije ikiwang’oa mabingwa hao watetezi na kwenda kucheza fainali na Simba ingawaje Mbao ilipoteza.

SIMBA

Msimu wa pili Simba alifika fainali na kwenda kucheza dhidi ya Mbao Mei 27, na kuchukua ubingwa baada ya kuifunga Mbao mabao 2-1, katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Jamuhuri Dodoma.

Mabao ya Simba yalifungwa na Fredrick Blagnon na Shiza Kichuya aliyefunga kwa penalti dakika 120, baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1, bao la Mbao lilifungwa na Ndaki Robart.

Baada ya hapo Simba ambayo ilikuwa haijacheza mashindano ya kimataifa si chini ya miaka mitano ilikwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika na kuondolewa katika hatua ya pili na Al Masry ya Misri kwa sheria ya bao la ugenini baada ya sare ya 2-2, hapa Dar es Salaam, na kwenda ugenini kutoka suluhu.

Simba baada ya kutoka kuchukua ubingwa msimu uliofuata katika Kombe la ASFC iliondolewa katika hatau ya kwanza dhidi ya timu ya jeshi Green Warriors kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Warriors ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Hussein Bunu kwa kichwa kabla ya John Bocco wa Simba kusawazisha kwa mkwaju wa penalti hata hivyo, Simba iliondolewa kwa peanati na uongozi wa Wekundu wa Msimbazi ukamtimua Kocha Joseph Omog.

MTIBWA

Msimu uliopita Mtibwa Sugar ndiyo iliyoshinda katika mechi ya fainali ya ASFC dhidi ya Singida United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid pale Arusha kwa mabao 3-2.

Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Salum Kihimbwa, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Ismail Aidan wakati yale ya Singida United yalifungwa na Salumu Chuku ambaye kwa sasa yupo katika kikosi cha KMC pamoja na Tafadzwa Kutinyu ambaye naye yuko Azam.

Mtibwa ilikwenda kucheza katika mashindano ya kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika na iliondolewa na KCCA katika mechi ya pili iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex kwa jumla ya mechi zote mbili.

Mtibwa msimu huu imeshindwa kufika katika hatua ya fainali au hata kutetea ubingwa kwani imeondolewa na KMC katika hatua ya 16, kwa penalti 4-3, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao1-1. Kocha wa KMC Ndayiragije anakuwa kocha wa kwanza kuweka rekodi ya kuzitoa mabingwa watetezi wawili wa mashindano haya Mtibwa Sugar na Yanga 2017.

Mbali ya hilo mashindano haya yanaonesha ni ngumu kwa timu iliyochukua ubingwa msimu uliopita kufika fainali au kucheza kutetea ubingwa.

Advertisement