Taifa Stars ina mlima baada ya Uganda

Muktasari:

  • Stars inahitajika kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kisha kuiombea Cape Verde ama iibuke na ushindi au itoke sare na Lesotho kwenye mechi nyingine ya kundi D ili iweze kufuzu kwenye fainali hizo zitakazofanyika Misri, Juni mwaka huu

Machi 22, Taifa Stars itakuwa na mchezo muhimu wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ambao itacheza na Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Stars inahitajika kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kisha kuiombea Cape Verde ama iibuke na ushindi au itoke sare na Lesotho kwenye mechi nyingine ya kundi D ili iweze kufuzu kwenye fainali hizo zitakazofanyika Misri, Juni mwaka huu.

Ikiwa itafanikiwa kwenda fainali za AFCON, Stars itavunja mwiko wa miaka 39 ya unyonge wa kutofuzu kwenye mashindano hayo tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 pale ilipoenda kushiriki kwenye fainali zilizofanyika jijini Lagos, Nigeria.

Hakuna asiyependa kuona Taifa Stars ikifuzu fainali za Mataifa ya Afrika, mashindano ambayo ni makubwa zaidi kisoka barani Afrika kulinganisha na mengine yoyote yale.

Fainali za AFCON ni fursa muhimu ya kuitangaza nchi yetu hasa vivutio vya utalii na rasilimali zake, kujenga uzoefu kwa wachezaji wetu pia ni njia ya kujiweka sokoni kwa nyota wa Kitanzania, kuvutia klabu kadhaa za nje ya nchi ambazo zinaweza kuwachukua ili waende kucheza soka la kulipwa huko.

Wachezaji kama Ahmed Hassan, Dennis Oliech, Seydou Keita, Wilson Oruma ni miongoni mwa idadi kubwa ya nyota ambao fainali za AFCON ziliwaweka sokoni na kuwapatia malisho mazuri sokoni.

Kwa kutambua umuhimu wa mashindano hayo, ndio maana kumekuwa na juhudi kubwa zikifanywa na serikali pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuhakikisha Taifa Stars inakwenda Misri mwaka huu kushiriki fainali hizo.

Hata hivyo, wakati tunaendelea na harakati pamoja na jitihada za kuhakikisha timu yetu inafuzu AFCON, tunapaswa pia kutambua kazi ngumu iliyo mbele yetu ikiwa tutatimiza lengo hilo, kuanzia kwa wachezaji, TFF, Serikali pamoja na wadau wengine wa soka.

Wachezaji wanapaswa kufahamu kwamba fainali za Mataifa ya Afrika sio mashindano mepesi na yanakutanisha mataifa yenye vikosi bora ambavyo vinaundwa na kundi la nyota wenye daraja la juu.

Nyota wetu wanatakiwa kujiandaa kikamilifu kimbinu, kimwili na kiakili tayari kwa kukabiliana na aina ya ushindani tutakaokutana nao huko Misri ikiwa Taifa Stars itafanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Uganda kwenye mchezo huo wa mwisho.

Ndani ya klabu zao, ni lazima wachezaji wetu wahakikishe wanatimiza kwa asilimia mia moja, programu wanazopewa na mabenchi yao ya ufundi kwani ndizo chachu kwao kufikia ubora na ngazi ya kuweza kupambana na wachezjai wa daraja la juu.

Wakumbuke kuwa timu ya taifa hukaa kwa muda mchache tu pamoja hivyo hawatopata nafasi ya kuuimarisha vya kutosha ubora wao kama vile inavyokuwa kwenye klabu zao.

Lakini, kwa upande wa shirikisho linapaswa kufahamu kuwa kufuzu kwa fainali za Afrika ni mwanzo wa safari mpya kisoka kwa nchi kwani baada ya hapo ni lazima kuwe na mwendelezo mzuri wa Taifa Stars kufuzu mara kwa mara kwenye mashindano hayo.

Haitopendeza kuona Stars ikikaa tena kwa muda mrefu bila kushiriki kwenye mashindano hayo kama ilivyo hivi sasa hivyo kuna ulazima TFF ikaanda programu na mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha tunatengeneza vizazi vitakavyonya sual la kufuzu AFCON liwe la kawaida na sio bahati.

Kwa upande wa serikali na wadau kuna haja ya kutoa sapoti hasa katika soka la vijana ambalo ndilo litatupatia wachezaji bora na wa daraja la juu watakaoendeleza kile kinachotarajia kuanzishwa na kizazi cha sasa.

Hakutakuwa na maana kwa Taifa Stars kufuzu kwenye fainali za mwaka huu halafu baada ya hapo inarudi kwenye kundi la wasindikizaji kama ambavyo ilikuwa baada ya kushiriki fainali za mwaka 1980.

Wakati huu tunapojiandaa kuikabili Uganda, ni mzuri pia kwa kutafakari msingi endelevu wa soka letu wakati wa Fainali za Afrika, pia siku za usoni.