TIMUA VUMBI: TFF inatumia nguvu nyingi kupambana na mtu mmoja

Muktasari:

  • Karia na Kamati yake ya Utendaji ilipoingia madarakani mara moja ilianza kufanya kazi kwa jinsi utaratibu wao walivyojiwekea huku akimteua Katibu Mkuu, Wilfred Kidao na Cliford Ndimbo kuwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo akichukuwa nafasi ya Alfred Lucas ambaye mkataba wake ulikwisha.

UONGOZI wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia tangu uingie madarakani Agosti 12 mwaka jana, una zaidi ya mwaka mmoja yaani mwaka na miezi mitatu sasa.

Karia na Kamati yake ya Utendaji ilipoingia madarakani mara moja ilianza kufanya kazi kwa jinsi utaratibu wao walivyojiwekea huku akimteua Katibu Mkuu, Wilfred Kidao na Cliford Ndimbo kuwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo akichukuwa nafasi ya Alfred Lucas ambaye mkataba wake ulikwisha.

Uteuzi huo ulienda kwa muda ambapo baadaye, Kidao alitangazwa rasmi kuwa sio kaimu wa nafasi hiyo bali ni Katibu Mkuu wa kuajiliwa akichukuwa nafasi ya Selestina Mwesigwa lakini upande wa Ndimbo walisema anafanyakazi hiyo kwa kujitelea na huenda hadi sasa ni Ofisa Habari wa kujitolea. Ni jambo zuri kwani kujitolea ni maamuzi ya mtu mwenyewe.

Lakini ndani ya uongozi huo huo wa Karia mambo mengi yamekuwa yakitokea ikiwemo kushindwa kupata udhamini wa Ligi Kuu ambapo sasa maisha ya timu hata kama awali yalikuwa magumu ila sasa ugumu umezidi zaidi.

TFF imeshindwa kuwashawishi wadhamini kutoka kampuni mbalimbali kudhamini ligi tangu Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom kumaliza mkataba wake ingawa kulikuwepo na mazungumzo na kampuni hiyo ila tatizo lililopo ni kiasi cha pesa ambacho Vodacom walikuwa tayari kukitoa.

Habari za ndani zinasema Vodacom walikuwa tayari kuwapa TFF Sh 500 milioni ili wawe wadhamini washiriki jambo ambalo klabu zilipinga kwamba ni kiasi kidogo kulingana na mahitaji ya timu, huku TFF wao wakidaia ligi yao inathamani kubwa hivyo kukubali kiasi hicho ni kutojitendea haki na kutoithamini ligi yao.

Timu nyingi sasa ambazo hazina udhamini maisha yao ni ya shida, dhiki kubwa wala hayafai, wachezaji wanavumilia mateso kwani hiyo ndiyo kazi yao na wengi wao wanatafuta jinsi ya kutoka kimaisha kupitia vipaji vyao vya soka, hii yote ni kwa vile walizoea kuwa na angalau na pesa kidogo kutoka Vodacom pamoja na Azam Tv basi maisha yao yangelainika kidogo.

Achana na hilo la udhamini, maana timu lazima zikubali kujipanga ili maisha yaende, wajitahidi kushawishi kampuni ili kuwalinda katika kipindi hiki kigumu.

Kuna jambo moja kubwa ambalo sasa linakuwa sugu ndani ya TFF, kuna Kamati hii ya Maadili ambayo mtuhumiwa ukiingia huko basi nusura yako ni kifungo cha kuanzia mwaka mmoja ama miwili ila kwa asilimia kubwa ni kifungo cha maisha.

Ni kamati ambayo uamuzi wake sasa unaanza kutia hofu kana kwamba wanafanya kwa kuagizwa kuwa kosa la mtu huyu adhabu yake iwe ni kifungo cha maisha.

Alianza aliyekuwa Makamu wa Rais, Michael Wambura, akaja Dastun Mkundi baadaye Mbasha Matutu na sasa Wakili Revocatus Kuuli hawa wote wamefungiwa kujihusisha na soka maisha yao yote.

Wakati kikao cha kamati hiyo kikikaa wikiendi iliyopita, Wakili Kuuli alisema hana muda wa kwenda kuwasikiliza kwani tayari alijiuzuru hivyo haini sababu ya kamati hiyo kumjadili mtu ambaye si mwanafamilia yao, ingawa kamati ilisema itakaa na kutoa uamuzi hata kama hatafika ndivyo ilivyotokea.

Hawa waliofungiwa sio kwamba ndiyo wamefunga, hapana, kamati hiyo ipo kazini kwani tutawasikia wengi wakifungiwa na inatoa picha kwamba wanasoka sasa hawapo huru na hii ni baada ya kudaiwa kwamba hata wakiitwa kwenye hiyo kamati wanaambiwa ‘Kaa hapo ushughulikiwe’ na kwamba ukisikia kauli hiyo basi ujue kwamba safari ya kwenda kufanya shughuli zako zingine nje ya soka imefika.

Ila TFF itambue kwamba kuna maisha mengine nje ya TFF, hao watu wanaendelea na maisha yao kama kawaida kwani waliowengi wana kazi zao ama biashara zao zinazowaingizia pesa zaidi ya kuwepo hapo TFF. Wanawapa hatua zaidi ya kufanya majukumu yao kikamilifu na kwa muda mwingi.

TFF na kamati zao wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, kuna watu wanafanya madudu kuliko hata hao waliohukumiwa ila wapo wanaendelea na maisha kwa sababu tu ya uswahiba. TFF ifanye zaidi mambo ya maendeleo kuliko kupoteza nguvu nyingi kupambana na mtu mmoja mmoja.