Simba Dakika hizi tishio

Muktasari:

  • Simba na AS Vita wanacheza mechi ya sita ya kukamilisha hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Kundi D, likiwa pamoja na timu za JS Saoura na Al Ahly.

SIMBA inacheza na AS Vita ya DR Congo kesho Jumamosi lakini tatizo kubwa kwa Wekundu hao wa Msimbazi ni kufungwa mabao ya mapema na rekodi inaonyesha, ukiwakosa hapo huwapati tena kwani kipindi cha pili wanakuwa vizuri sana.

Lakini wapinzani wao AS Vita rekodi zao zinaonyesha wako vizuri zaidi kipindi cha kwanza huku cha pili wakipoteana.

Simba na AS Vita wanacheza mechi ya sita ya kukamilisha hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Kundi D, likiwa pamoja na timu za JS Saoura na Al Ahly.

Katika kundi hilo, vinara ni JS Saoura wana pointi nane, Al Ahly ya pili ikiwa na pointi saba ambazo sawa na AS Vita huku Simba ikishika mkia ikiwa na pointi sita.

Mpaka sasa timu yoyote kati ya hizo ina nafasi ya kufuzu robo fainali endapo itashinda katika mechi yake ya mwisho.

Katika mechi tano ilizocheza Simba, imefungwa mabao 12 na imefunga manne. Simba imefunga bao moja kipindi cha kwanza na matatu kipindi cha pili na imefungwa mabao tisa kipindi cha kwanza huku cha pili ikipachikwa matatu.

Wapinzani wao, AS Vita wamefunga mabao manane na kati ya hayo matano yakipachikwa kipindi cha kwanza huku matatu yakifungwa dakika za lala salama.

Wacongo hao wamefungwa mabao matano, moja likiwekwa kimiani kipindi cha kwanza na cha pili manne.

MABAO YALIVYOFUNGWA

Simba ambayo iliyaanza vizuri mashindano hayo kwa kuifunga JS Saoura mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, yalifungwa na Emmanuel Okwi dakika za nyongeza baada ya 45, kumalizika na mawili yalipachikwa na Meddie Kagere dakika ya 52 na 67.

Mechi ya pili Simba ilifungwa na AS Vita mabao 5-0, kati ya hayo matatu yalifungwa dakika za mwanzo na mawili za lala salama.

Jean Makusu alifunga mawili dakika ya 14 na 74, Botuli Bompunga dakika ya 19, Fabrece Ngoma (45) na Makwekwe (71).

Simba ilipigwa tena 5-0 na Al Ahly na mabao yote yakipachikwa dakika za mwanzoni na Emr Elsilia dakika 3, Ali Maaloul ya 23, Junior Ajayi 31, Karim Waled 33 na 40.

Simba ilirudi nyumbani na kuifunga Al Ahly bao 1-0, likipachikwa na Meddie Kagere dakika ya 64, lakini ilipoteza tena dhidi ya JS Saoura ilipofungwa mabao 2-0, yakipachikwa na Sid Cherif dakika ya 18 na Mohamed Hammia ya 51, ukiwa ndio mchezo wake wa tano.

Kwa upande wa AS Vita ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0, dhidi ya Al Ahly yaliyofungwa na Nasser Maher dakika 5 na Ali Maaloul ya 79, iliifunga Simba 5-0 nyumbani, ikatoka sare 2-2 na JS Saoura katika uwanja wake wa nyumbani.

Mabao ya AS Vita yalipachikwa na Kazadi Kasengu dakika ya 14 na Jean Makusu ya 37 wakati ya JS Saoura yakitupiwa na Mohamed Hammia dakika ya 45 na Sid Cherif ya 88.

Mechi yake ya tano iliifunga Al Ahly bao 1-0 uwanja wa nyumbani, lililopachikwa na Tuisila Kisinda dakika ya 84.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga ambaye ni Mcongo, Patrick Katalayi alisema: “Ubora wa AS Vita ni dakika za mwanzo timu inayofanikiwa kumaliza vizuri kipindi cha kwanza cha pili inafanikiwa na hii ni kutokana na mipango yake katika mechi husika.”

Kocha wa Mlandege ya Zanzibar na wa zamani wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohammed ‘Bares’ amesema:

“Kufungwa mabao mapema na kushinda kipindi cha pili ni mipango tu kulingana na mechi husika kwani mwishowe kuna ushindi na kufungwa.”

Acha tuone kesho Simba itafanya nini nyumbani.