Nimewaelewa vizuri Serengeti Boys

Muktasari:

  • Serengeti Boys walistahili kupokea kichapo kikubwa zaidi cha mabao kutoka kwa Uturuki na walilazimika kufanya kazi kubwa hadi wakafungwa mabao hayo 5-0 kwenye mechi hiyo ambayo walionekana kuzidiwa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho ya mechi hiyo.

Baada ya kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Uturuki katika mchezo wa mashindano maalumu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yaitwayo ‘UEFA Assists’, vijana wawili wa timu ya Tanzania ya umri huo ‘Serengeti Boys’ walijirekodi video wakitoa maoni yao juu ya kipigo hicho.

Walionekana wakikiri kustahili kupokea kipigo kile kwenye mechi hiyo ya mashindano hayo ambayo huratibiwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) na kujipa sifa wamejitahidi vilivyo hadi wakafungwa idadi hiyo ya mabao huku wakiwa wanatabasamu.

Kiufupi walimaanisha walistahili kupokea kichapo kikubwa zaidi cha mabao kutoka kwa Uturuki na walilazimika kufanya kazi kubwa hadi wakafungwa mabao hayo 5-0 kwenye mechi hiyo ambayo walionekana kuzidiwa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho ya mechi hiyo.

Ikumbukwe mbali ya kipigo hicho kutoka kwa Uturuki, Serengeti Boys ilifungwa mabao 2-1 na Guinea kwenye mechi ya kwanza na katika mchezo wa pili iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Australia ikilazimika kupata ushindi huo kwa jasho baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-1.

Ni Serengeti Boys hiyo ambayo hadi inakwenda Uturuki ilikuwa ni bingwa wa makombe mawili ambayo ni lile la Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wa umri huo pamoja na lile la nchi za Kusini mwa Afrika.

Baadhi ya wadau wa soka nchini wameonyeshwa kukerwa na video ya wachezaji wale wa Serengeti Boys wakidai kuwa hawakuonyesha kuumizwa na kipigo walichokipata cha mabao 5-0 kutoka kwa Uturuki lakini ukitafakari kwa umakini, utagundua kuwa vijana wale walikuwa wamefanya jambo la maana kwa video ile.

Hupaswi kuwalaumu wachezaji wa Serengeti Boys kwa kutoumizwa na kichapo cha idadi kubwa ya mabao mbele ya timu ambayo wachezaji wake wamekulia na kuandaliwa katika mfumo bora wa soka chini ya klabu tofauti na wetu ambao wanatokea mitaani na kulelewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kimsingi klabu za soka ndizo zenye jukumu la kusaka vipaji vya watoto na kuvilea badala ya shirikisho la soka la nchi lakini kwa hapa nyumbani mambo ni kinyume ambapo TFF ndio imekuwa ikifanya jukumu hilo.

Isingewezekana kwa Serengeti Boys kupata matokeo mazuri mbele ya timu yenye wachezaji kutoka katika vikosi vya vijana vya klabu kubwa na zilizofanya uwekezaji unaoeleweka katika soka la vijana kama Besiktas, Fenerbahce, Galatasary na kadhalika.

Kilichotokea kilikuwa ni mavuno sahihi kwa mbegu ambayo tumeipanda wenyewe kwa kuruhusu klabu zetu zizadharau uwekezaji katika soka la vijana.

Tulihitaji kichapo kama kile kutoka kwa Uturuki ili kitufungue macho na upeo wetu na kuanza kuweka msisitizo wa kuwekeza katika soka la vijana.

Video ile ya vijana wetu wa Serengeti Boys, tuipokee kwa mtazamo chanya na kuitumia kama darasa badala ya kuwajengea chuki wale watoto.