Kwa staili hii, KMC itabaki kuwa juuuu

Friday March 15 2019

 

By CHARITY JAMES

MSIMU huu ni timu sita ndio zimepanda daraja tofauti na misimu mingine iliyopita nyuma. Ligi Kuu Bara ilikuwa na jumla ya timu 16 kabla ya kuongezwa timu nne zilizofanya vyema Daraja la Kwanza na kuifanya Ligi Kuu kuwa na timu 20. Timu sita zilizopanda ni pamoja na KMC, Coastal Union, Alliance FC, JKT Tanzania, Biashara United na African Lyon.

Hata hivyo, katika mchakamchaka wa Ligi Kuu hadi sasa ikiwa ni mzunguko wa pili, kati ya timu hizo zilizopanda daraja, ni mbili tu ambazo zimeonyesha ushindani mkubwa kwenye ligi hiyo, KMC ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga, huku nyingine zikisuasua.

Makala haya yanaiangazia zaidi KMC ambayo kwa msimu huu ikiwa ndio msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu imekuwa moto na hapa Mwanaspoti linakuwekea mambo yaliyosababisha iwe imara hadim kukabana koo na timu kongwe kwenye ligi.

ETIENNE NDAYIRAGIJE

Ndiye kocha mkuu wa KMC. Kabla ya kutua KMC kocha huyo alitoka kufungashiwa virago na Mbao FC ya Mwanza ambao waliamini ameshindwa kuendana na mfumo wa timu hiyo.

Hata hivyo, KMC ni kama walikuwa wanasubiri kujiokotea dodo na mara tu baada ya Ndayiragije kusepa Mbao, walimchukua na kumkabidhi timu. Ni kocha mpambanaji na ameweza kuijenga timu hiyo kwa mfumo mzuri wa kiupambanaji unaoibeba timu hiyo.

Kwa sasa KMC ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 41 nyuma ya Simba yenye pointi 51.

USAJILI MAKINI

Hiki ndi kinachoibeba zaidi KMC. Imefanya usajili wa maana wa nyota wenye uzoefu na chipukizi. Kuhusu mikataba, KMC imewapa wachezaji wake mikataba ya mwaka mmoja mmoja ikiwa ndio utaratibu iliyojiwekea. Hii imesaidia pia kupata nyota wenye majina makubwa wenye uzoefu ambao uwepo wao utasaidia damu changa kutoka kwenye kituo cha kuzalisha vijana cha KMC. Hivyo nyota wote wameendana na soka la ushindani la Ligi Kuu na ndio maana kasi yao imeku wa ku bwa tofauti na timu nyingine zilizopanda daraja msimu huu.

KAMBI INAYOELEWEKA

Achana na Simba, Yanga na Azam FC ambazo kwao kuweka kambi ni sehemu yoyote ndani na nje ya nchi. Zimekuwa zikipishana angani mara kwa mara hasa Simba na Yanga.

Hata hivyo, kwa KMC hiyo sio ishu sana, kwani japokuwa wanaweka kambi yao jijini Dar es Salaam, lakini unaambiwa kambi hiyo sio ya kitoto.

KMC imekuwa ikiweka kambi kwenye hotel kubwa ya nyota tano ili wachezaji wake wawe fiti kimchezo.

Hii ni kutokana na mazingira tulivu kwenye kambi hiyo, ndio maana kasi yao msimu huu imekuwa kubwa na kufanikiwa kuwa top five ya Ligi Kuu japokuwa ni msimu wao wa kwanza.

NIDHAMU

Ndio kitu cha kwanza kwa mchezaji yeyote anayetua timu fulani. Nidhamu ni chachu ya mafanikio na ndio maana KMC kwa sasa inafanya vizuri tofauti na mwanzo ilipopanda daraja.

Mwanzoni mwa msimu iliingia doa baada ya mchezaji wao, Abdulhalim Humud kuhusishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wachezaji wenzake na kocha wa timu hiyo.

Hata hivyo, kwa sasa nidhamu ndio imekuwa chachu ya ushindi wa KMC na imekuwa ikipata matokeo yaliyowaweka pazuri kwenye msimamo.

MISHAHARA KWA WAKATI

Kama kuna kitu kinachowapa morali wachezaji wa KMC kufanya yao kwenye Ligi Kuu msimu huu basi ni bosasi wanazopata kila baada ya mechi. Sio Simba na Yanga tu ambazo zimekuwa zikifanya hivyo kwa wachezaji wao ili kuongeza morali ya kusaka ushindi.

KMC imegundua ili kuwafanya wachezaji wake kuwapa raha mashabiki na viongozi wa timu ni kuwawekea mizigo ya maana mezani kila wanaposhinda. Kwa nini wasijitume?

Pale KMC kulia njaa hakuna kwani hata mishahara yao wanapewa kwa wakati na kuwafanya wakati wote wafikirie tu mchezo unaofuata na namna ya kuondoka na poiti tatu, sio kingine.

WACHEZAJI WALA KIAPO

Kwanza, nyota wa KMC wana umoja na hiyo inasaidia kwenye kupambana kuhakikisha inamaliza ndani ya nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwezekana hata nafasi ya tatu ili kutengeneza rekodi yao tamu mwishoni mwa msimu huu. Wanasema mafanikio yao na siri ya wao kuweza kuendana na kasi ya ligi ni kutokana na kuwa wamoja na kuamini wanaweza kupambana na kufikia malengo yao waliyojiwekea kwa kuweza kuwa nafasi tatu za juu hadi msimu unapomalizika malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu.

Advertisement