Kindoki, Coulibaly ndio wamefufuka!

Friday March 1 2019

By CHARLES ABEL

Klausi Kindoki na Zana Coulibaly hawakuwa na mwanzo mzuri ndani ya vikosi vya Simba na Yanga kwenye msimu huu wa ligi.

Ndani ya kikosi cha Yanga, Kindoki anayetoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alijikuta akisotea benchi licha ya wengi kuwa na matumaini kama ndio angekuwa chaguo la kwanza kusimama kwenye lango la timu hiyo.

Sababu ni moja tu kua alikuwa akifungwa mabao ya kizembe ambayo yalikuwa yakiiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu katika baadhi ya mechi zake.

Kwa upande wa Coulibaly aliyesajiliwa na Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo, naye alikuwa akicheza chini ya kiwango na kufanya makosa hasa ya kutokuwa makini kwenye ukabaji huku kasi yake ikionekana kuwa chini.

Unaweza kusema kuwa ndio wachezaji ambao wameonja shubiri ya lawama kutoka kwa mashabiki wa timu zao au hata wale wa timu nyingine.

Lakini katika mechi za hivi karibuni wawili hao wameonyesha kiwango bora ambacho kimsingi kinatusuta wote ambao tulikuwa tunabeza uwezo wao ndani ya uwanja.

Je ilikuwa kosa kuwabeza wachezaji hao wakati ule walipokuwa wanafanya vibaya?

Kimsingi sio dhambi kwa shabiki au mdau wa soka kumkosoa mchezaji pindi anapofanya vibaya kwa sababu soka ni mchezo wa matokeo. Pale shabiki anapoona mchezaji anashindwa kutimiza wajibu wake ndani ya uwanja, ni haki ya msingi kwake kumkosoa na ikibidi hata kumzomea.

Wakati mwingine ukosoaji wa watu ndio unawafanya wachezaji wajitazame na kufanyia kazi udhaifu wao ili wawe na viwango bora kama ambavyo inatokea kwa Kindoki na Coulibaly.

Pongezi kwa Coulibaly na Kindoki kwa kuanza kuonyesha matumaini kwenye timu zao lakini pia wale waliokuwa wanawakosoa hawapaswi kunyooshewa vidole kwa sababu ndio wamewaamsha usingizini.

Ni bora mtu anayekuambia ukweli wakati unafanya vibaya kuliko yule anayekusifu.

Advertisement