NINAVYOJUA : Hivi ndivyo Amunike alivyotuweka njia panda Afcon

Muktasari:

Binafsi najaribu kufikiria licha ya maumivu tuliyonayo, ni kitu gani hasa kilituangusha na kumfanya Kocha Amunike ashindwe kupata matokeo na nini kifanyike kupata matokeo kwenye mchezo dhidi ya Uganda. Nataka tuzijadili sababu hizo na suluhisho lake.

TAKRIBANI wiki yote hii vyombo vya habari vimezungumzia kipigo cha tulichokipata huko Lesotho. Wapo walilalamika tu na kukosoa mbinu za Kocha Emmanuel Amunike.

Na wengine walimtaka aondoke na wapo waliowalaumu wachezaji.

Wengine wanaamini nchi haina wachezaji wenye viwango vya kushiriki mashindano makubwa.

Binafsi najaribu kufikiria licha ya maumivu tuliyonayo, ni kitu gani hasa kilituangusha na kumfanya Kocha Amunike ashindwe kupata matokeo na nini kifanyike kupata matokeo kwenye mchezo dhidi ya Uganda. Nataka tuzijadili sababu hizo na suluhisho lake.

Nagawa sababu hizi katika maeneo matatu;

1. UCHAGUZI WA WACHEZAJI

Kuna tatizo kubwa kwenye uchaguzi wa wachezaji wa kuitumikia timu ya taifa. Makocha wengi duniani hulalamikiwa pengine kwa kumuacha mchezaji mmoja au wawili wanaofaa kwenye kikosi. Hata Amunike alilalamikiwa kuwaacha Hassan Dilunga na Ibrahim Ajibu bila shaka uwepo wao ungesaidia na kumlazimisha kutoka kwenye falsafa ya kutumia viungo wakabaji au wazuiaji wengi na kuwa na chaguo zuri la kuwatumia viungo washambuliaji wengi. Baada ya uchaguzi wa kikosi kinachofuata ni kikosi ambacho kimelalamikiwa sana na kuwa chanzo cha timu kushindwa kufanya vibaya. Ukweli usiojificha hapa Kocha Amunike ndipo aliposhindwa. Kocha alishindwa kuitendea haki moja kati ya kanuni za ukocha, siku zote ukipata kikosi cha ushindi usikibadilishe hadi hapo matokeo mengine yatakapotokea.

Ni wazi Amunike alishaipata timu iliyocheza vizuri dhidi ya Cape Verde jijini Dar es Salaam na kwenye mchezo wa Lesotho walikosekana wawili tu Mbwana Samata na Shomari Kapombe, hivyo alitakiwa kuingiza sura mbili tu au tatu labda kwenye nafasi ya kiungo anapocheza Mudathir Yahya ambaye pamoja na kucheza michezo yote chini ya Amunike bado sijauona ufanisi wake. Matarajio ya wengi ni kumuona Hassan Kessy akianza beki ya kulia. Makosa aliyofanya ni kuingiza sura mbili za wachezaji wageni kwenye kikosi hicho katika nafasi muhimu, Abdallah Kheri na Ali Sonso. Hawa ni wachezaji wapya wakacheza kwenye nafasi ngeni, Kheri akiwa Azam FC na Sonso akiwa Lipuli wanacheza kama mabeki wa kati. Kosa la pili kuwabadilisha wachezaji wanaocheza kwenye nafasi zao sahihi na kuwapeleka mbele, Gadiel Michael alichezeshwa kama winga badala angalau kucheza kama winga beki mfumo ambao aliutumia dhidi ya Uganda na Cape Verde wakati Amunike alipowapanga mabeki wa kati asilia watatu, Agrey Morris, Kelvin Yondani na Abdi Banda

Kosa la tatu lilikuwa kuipanga timu kwa kuwatumia viungo watatu ambao kihasilia ni wazuiaji kitu kilichosababisha kucheza ikiwa chini huku washambuliaji wakishindwa kupewa pasi za mwisho.

2. MAANDALIZI YA SIKU KUMI

Bila shaka viongozi wa TFF walitaka kuhakikisha timu inapata muda sahihi wa kufanya mazoezi na kumsaidia kocha kuona nini anatakiwa kukifanya ndani ya muda ule. Kutengeneza mbinu za ushindi na kuwajenga kisaikolojia wachezaji ndilo lilikuwa tegemeo la wengi lakini kumeibuka makosa ya kiufundi ndani ya mazoezi hayo ya muda mfupi. Kwa jicho la kiufundi, kwanza utagundua inawezekana wachezaji walifanya mazoezi mengi mazito na kwa muda mrefu. Utagundua hilo kwa jinsi wachezaji walivyoonekana kukosa unyumbufu na huku wakifanya makosa mengi. Unaona jinsi uwezo wao wa kukaa na mipira ulivyopungua bila shaka ni kutokana na aina ya mazoezi waliyofanya.

Hakuna umuhimu wa kuwafanyisha mazoezi magumu wachezaji ambao ndio kwanza wanatoka kwenye ligi na miili yao ikiwa imekunjuka kwa ajili ya uchezaji. Ndio maana wapo watu wanahoji kwa nini siku 10 na kuisimamisha ligi! Hayo yote yasingeulizwa iwapo timu ingecheza kwa usahihi zaidi

3. VIWANGO VYA CHINI

Haikuwa ajabu kuona viwango vya chini kwa wachezaji wengi tofauti na kawaida. Aishi Manula alifanya makosa mawili moja likaigharimu timu. Kheri alifanya makosa mengi. Sonso hakustahili kumaliza mchezo. Aggrey Morris alifanya makosa. Nyoni alikuwa mzito huku Mudathir akipoteza pasi nyingi. Simon Msuva hakuwa kwenye kiwango chake na bila shaka timu kama timu haikucheza vizuri.

Ni muda sasa kujipanga kisaikilojia kuelekea mchezo wa kufa na kupona dhidi ya Uganda huku masikio yetu yakisikilizia yatakayokuwa yanajiri huko Cape Verde itakayocheza na Lesotho.